Rais Karia ana kazi kubwa CAF

Zimebaki siku 17 kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) huko nchini Morocco.

Uchaguzi huo utafanyika Machi 12 ambapo nchi wanachama wa Caf watapata fursa ya kuchagua Rais wa Shirikisho hilo pamoja na wajumbe wa kamati ya utendaji.

Kwenye Urais hapo hapana vita sana kwani Patrice Motsepe ndiye mgombea pekee wa nafasi hiyo akiitetea nafasi hiyo ambayo anaitumikia hivi sasa tangu alipochaguliwa mwaka 2020.

Vita kubwa ipo katika kinyang’anyiro cha nafasi za ujumbe wa kamati za utendaji ambayo inahusisha wagombea tisa wanaowania nafasi sita.

Katika kundi hilo yumo Rais wa TFF, Wallace Karia ambaye pia ni Rais wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Ikiwa Karia atafanikiwa kupata nafasi hiyo, atakuwa na uhakika wa kuvuna kiasi cha Shilingi 130 milioni kwa mwaka.

Fedha hizo ni mgao ambao kila Mjumbe wa kamati ya utendaji ya Caf analipwa na shirikisho hilo kwa mujibu wa uamuzi uliofanywa Septemba mwaka jana.

Caf iliamua kuwepo na ongezeko la Doła 10,000 katika malipo ambayo awali wajumbe wa kamati ya utendaji ya shirikisho hilo walikuwa wanapata.

Wakati wajumbe wa kamati ya utendaji ya Caf kila mmoja akipata Doła 50,000, Rais wa Shirikisho hilo atakuwa anapokea kiasi cha Doła 70,000 (Sh182 milioni) kwa mwaka.

Lakini Karia ikiwa atafanikiwa kushinda nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji ya Caf, atavuna kiasi kikubwa cha fedha kuliko wajumbe wenzake.

Karia atapata ongezeko la Doła 25,000 (Sh52 milioni) kwa vile yeye ni Rais wa Cecafa.

Wagombea wengine na nchi wanazotoka ni Mustapha Raji (Liberia), Elvis Chetty (Shelisheli), Sadi Walid (Algeria), Sobha Mohamad (Mauritius), Kurt Okraku (Ghana), Feizal Sidat (Msumbiji), Alfred Randriamanampisoa (Madagascar) na Bestine Kazadi wa DR Congo.

Related Posts