Korogwe. Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza kufanywa tathimini ya mashamba makubwa yasiyoendelezwa wilayani Korogwe mkoani Tanga, ili kujua taarifa zake na hatimaye yatumiwe na wananchi.
Chimbuko la agizo hilo ni hoja iliyoibuliwa na Mbunge wa Korogwe Vijijini, Timotheo Mzava aliyesema kuna mashamba mengi makubwa katika eneo hilo na hayaendelezwi.
Rais Samia ametoa agizo hilo leo, Jumatatu, Februari 24, 2025 alipohutubia wananchi wa Korogwe, katika ziara yake ya kikazi mkoani Tanga.
Amemtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi kufanya tathimini ya mashamba makubwa yasiyoendelezwa
Tathimini hiyo, amesema ilenge kujua taarifa za mashamba husika na kwamba anafahamu baadhi yameshakopewa fedha nje ya nchi.
“Lakini hatuwezi kumridhisha mtu mmoja aliyekopa akaweka mashamba yetu dhamana, kwa sababu ardhi haihami anaeleza kuweka dhamana huku bado yanaendelea kuzalisha,” amesema.
Baada ya tathimini hiyo, ametaka apelekewe taarifa ili kwa pamoja waone kinachopaswa kufanywa kwenye mashamba hayo.
Hata hivyo, Ndejembi amesema wizara hiyo imeshalifuta moja ya shamba lililokuwa na ekari 5,000 na limegawiwa kwa wananchi na lililobaki mchakato wa kulikabidhi kwa halmashauri unaendelea.
Mbali na hilo, Rais Samia amezungumzia mradi wa Bwawa la Mkomazi alilosema Sh18.2 bilioni zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji.
Iwapo mradi huo utakamilika, amesema wakulima wataweza kuvuna mara mbili kwa mwaka badala ya mara moja.
Amesisitiza kuwepo kwa mradi huo ni ukombozi kwa wakulima.
“Nimepata faraja huko nyuma nilikuwa kila nikiuliza nilikuwa naambiwa bado kuna watu hawajaridhika ule mradi uwepo.
“Lakini nikawa mkali sana nikamwambia waziri hatuwezi kuwasikiliza wachache, tukawakosesha wengi kutonufaika na mradi huu,” amesema.
Amesema amefarijika kuona imewezekana mradi huo umeanza kutekelezwa na anaamini utakamilika kama ilivyopangwa.
Dhamira ya Serikali, amesema ni kumuinua mkulima na kinachofanyika ni kuongeza tija, ikiwemo kuwa na uhakika wa kulima wakati wote.
Amesema kiu ya Serikali ni kuhakikisha wakulima wa Tanzania wanamudu kula na hatimaye kuuza mazao ndani na nje ya nchi.
Amesema kwa sasa nchi ina uwezo wa kujitosheleza kwa chakula takriban asilimia 128 lakini mataifa ya jirani yanakabiliwa na uhaba wa chakula, hivyo kupitia ujenzi wa mabwawa itasaidia kuongeza kiwango cha uzalishaji na kuuza nchi za jirani.
“Hili bwawa ilikuwa ni ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere lakini haikutimizwa kutokana na hali za kifedha na awamu nyingine hivyo hivyo, lakini awamu hii tumeweza kupata afueni ya kifedha na tumeweza kutekeleza mradi huu ” amesema Rais Samia.
Kuhusu changamoto ya kukosekana kwa mnunuzi wa zao la chai, amesema tayari Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ameshalichukua na anaamini suluhisho litapatikana.
Ameambatanisha hilo na suala la mashine za kuchakata mkonge, akisema tayari zimeagizwa na zimeshafika nchini na nyingine zitaletwa baadaye.
Amemtaka Waziri wa Afya, Jenista Mhagama kuchukua sehemu ya fedha kati ya zilizopatikana hivi karibuni, kwa ajili ya maboresho ya ukarabati wa Hospitali ya Magunga iliyojengwa tangu mwaka 1952.
Katika hotuba yake hiyo, ameweka wazi mapenzi yake kwa walimu, akisema baba yake ni mwalimu hivyo anayajua madhila yaliyomo ndani ya taaluma hiyo.
“Walimu nawapenda sana, na nawapenda kwa sababu wanatusaidia kuelimisha umma wa Watanzania, wana kazi nzito sana.
“Kwa wale wasiojua mimi pia baba yangu ni mwalimu kwa hiyo nayajua mazito ya walimu. Walimu Oyee… Walimu juzi mmenisikia?… Haya fanyeni kazi mama yupo na ninyi,” amesema na kuibua shangwe kutoka kwa walimu.
Rais Samia amewashukuru wananchi mkoa wa Tanga kwa upendo waliounyesha tangua aanze ziara jana, akisema pia amejiona utekelezaji mzuri wa ilani ya uchaguzi ndani ya mkoa huo.
“Kwa kuwa nipo hapa kwa wiki nzima, nitaendelea kuzunguka na kuona, kwa kiasi fulani niseme Tanga matumizi ya fedha siyo kwa asilimia 100 kwa kiasi kikubwa yametumika vizuri.
” Miradi imetekelezwa vizuri hoja ukimleta mkaguzi hapa haziachi kuwepo, lakini kwa kiasi kikubwa fedha zimetumika vizuri hadi sasa hivi. Bado nipo wiki nitaendelea kuzunguka, kwenda kuona maeneo mengine, nimuombe Mkuu wa Mkoa (Dk Batilda Buriani) na watu wako simamieni fedha zinazoshushwa chini kwa wananchi,” amesema Rais Samia.
Jana wakati akianza ziara eneo la Mkata, Rais Samia alizindua hospitali ya wilaya ya Handeni, iliyogharimu Sh7.3 bilioni akisema imejengwa vizuri na kwa viwango kama hospitali ya mkoa.
Vivyo hivyo leo Jumatatu Februari 24,2025 mkuu huyo wa nchi alizindua jengo la halmashauri ya Bumbuli wilayani Lushoto ambapo alipongeza ujenzi wake na kuwataka wananchi wa eneo kulitunza.
Mbunge wa Korogwe Mjini, Dk Alfred Kimea amemwomba Rais Samia awezeshe kupatikana kwa Sh900 milioni kwa ajili ya maboresho ya Hospitali ya Magunga iliyochakaa.
Amesema hospitali hiyo ilijengwa tangu mwaka 1952, kwa sababu ya ukongwe wake, imechakaa na haikidhi mahitaji ya sasa.
Ameliambatanisha ombi hilo na lile la kupatikana Sh9 bilioni za ujenzi wa Bonde la kwa Msisi, lakini hadi sasa hakuna hatua iliyofikiwa.
Ombi lingine, amesema ni ujenzi wa kiwango cha lami katika barabara ya Old Korogwe ili kuwarahisishia usafiri wakazi wa Korogwe Mjini.
Kwa upande wa Mbunge wa Korogwe Vijijini, Timoth Mzava amesema uchaguzi mkuu upo kama kawaida na wanaosema ‘no reforms no election’ wamechemka na wamekosa la kufanya.
” Hawa wanaosema maneno hayo wamekosa la kufanya, hawana ajenda kwa sababu Rais Samia ni kiongozi aliyekubali kufanya mabadiliko katika sheria za uchaguzi, vyama vya siasa na tume ya uchaguzi zilizojibu kilio cha namna ya kupata wasimamizi wa chaguzi.
“Mheshimiwa Rais watu wa Korogwe tunakuambia uchaguzi upo, mgombea wetu ni Samia na Rais wetu ni Samia,” amesema Mzava.
Imeandikwa na Bakari Kiango, Juma Issihaka na Rajabu Athumani