Berlin. Matokeo ya awali katika uchaguzi wa kitaifa nchini Ujerumani yanaonyesha chama cha Conservatives kikiongozwa na mgombea wake, Friedrich Merz kimeshinda uchaguzi huo dhidi ya vyama vingine kikiwemo cha Kansela wa sasa, Olaf Scholz.
Katika matokeo ya uchaguzi huo yaliyotangazwa leo Jumatatu Februari 24, 2025, chama cha mlengo wa kulia cha Altenative for Germany (AfD), kimeshika nafasi ya pili dhidi ya Conservatives katika uchaguzi huo.
Tovuti ya ABC News, imeripoti kuwa Merz, tayari amehutubia taifa na kuahidi kuiunganisha Ulaya ili kuiwezesha kukabiliana na mataifa kama Russia na Marekani. Kutokana na ushindi huo Merz atakuwa kiongozi mpya wa nchi hiyo akichukua mikoba ya Scholz.
Merz, katika uundaji wa serikali yake huenda akashirikiana na chama cha Kisoshalisti cha mrengo wa kushoto, ambacho kilipata pigo baada ya muungano wao kuvunjika.
Hata hivyo, matokeo hayo yameibua hofu nchini humo hususan katika vyama vikubwa baada ya chama kinachopingana na sera ya uhamiaji cha AfD kupata matokeo bora zaidi katika historia yake.
Kampeni hiyo iligubikwa na wasiwasi kuhusu kudorora kwa uchumi wa Ulaya kwa miaka kadhaa na shinikizo la kudhibiti uhamiaji, jambo ambalo liliibua mvutano baada ya Merz kusisitiza msimamo mkali katika wiki za hivi karibuni.
Uchaguzi huo pia ulifanyika katika hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu mustakabali ushiriki wa Marekani na Ulaya katika vita ya Ukraine dhidi Russia.

Kansela ajaye aliyeshinda uchaguzi wa Ujerumani, Friedrich Merz
Matokeo yaliyotolewa na mamlaka ya uchaguzi yalionyesha kuwa chama cha Kikristo cha Merz na Kisoshalisti cha mrengo wa kushoto vilipata idadi kubwa ya viti katika bunge la kitaifa, baada ya vyama vidogo kushindwa kufikia kiwango cha chini cha uwakilishi kwenye sanduku la kura.
Akizungumza usiku wa kuamkia leo kabla matokeo yote kutangazwa, Merz alisema kuwa ataunda serikali mpya kabla ya Pasaka.
Ameweka wazi kuwa hatoshirikiana na chama cha mrengo mkali wa kulia, AfD, ambacho sasa ni chama cha pili kwa ukubwa nchini Ujerumani.
Kwa sasa, Kansela anayeondoka Olaf Scholz, ambaye chama chake cha Social Democratic Party (SPD) kilipata pigo kubwa, ataendelea kuisimamia serikali ya mpito hadi Merz atakapoingia madarakani.
Chama cha Conservatives cha Merz kilipata viti 208 kati ya 630 katika bunge la nchi hiyo (Bundestag), huku AfD wakipata 152.
Vyama vitatu vya muungano wa zamani wa serikali vilipoteza viti, ambapo SPD kilipata viti 120 na chama cha Kijani (the Greens) kikapata 85.
Chama cha Demokrasia Huria (FDP), ambacho kilikwamisha uchaguzi wa awali kwa kujiondoa kwenye muungano, hakikufanikiwa kupata asilimia tano ya kura zinazohitajika kushinda viti katika bunge hilo.
Hata hivyo, chama cha mrengo wa kushoto cha Die Linke kimepata viti 64, huku muungano wa mrengo wa kushoto wa Sahra Wagenknecht Alliance ukikosa kufikia kiwango cha chini cha kura cha asilimia tano.
AfD walisherehekea Jumapili usiku, huku viongozi wake wakiahidi kuwa chama kikuu katika uchaguzi ujao kadri mvuto wao unavyozidi kuongezeka.
Chama hicho cha mrengo mkali wa kulia kinachopinga uhamiaji kimejijengea umaarufu mkubwa tangu kilipoanzishwa miaka 12 iliyopita, ingawa bado hakijawa sehemu ya serikali yoyote ya kitaifa ama ya jimbo.
Vyama vingine vimesema havitashirikiana na AfD, ambacho kinachunguzwa na Idara ya Ujasusi ya Ujerumani kwa tuhuma za kuwa na msimamo mkali, madai ambayo AfD inayakanusha vikali.
Matawi ya chama hicho katika majimbo matatu ya mashariki yametajwa kama makundi tishio jambo linaloibua hisia kali na kuwarejesha watu katika historia ya za chama cha Nazi.
Uchaguzi huo umefanyika miezi saba kabla ya ratiba iliyokuwa imepangwa baada ya muungano wa vyama vinavyomuunga Scholz kuvunjika Novemba, 2024, ikiwa ni miaka mitatu ya muhula wake wa kwanza, ambao ulikumbwa na migogoro ya ndani.
Katika uchaguzi huo, kulikuwa na mwamko mdogo wa wananchi kupiga kura na hamasa ndogo kutoka kwa wagombea wote.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.