Simba, Azam FC hakuna mbabe Kwa Mkapa

MASHABIKI wa Simba walikuwa wakihesabu dakika ili kuanza kushangilia ushindi wa 17 katika Ligi Kuu Bara, baada ya chama lao kuongoza kwa mabao 2-1 hadi dakika ya 87, lakini mambo yalitibuka sekunde chache tu baada ya mtokea benchi, Zidane Sereri kuchomoa bao katika Dabi ya Mzizima.

Zidane aliyeingia uwanjani kumpokea Idd Seleman ‘Nado’ alifunga bao dakika mbili kabla ya filimbi ya mwisho ya refa, Ahmed Arajiga aliwaduwaza wanasimba kwa kufunga bao tamu mbele ya kipa Moussa Camara na beki Chamou Karaboue waliyemkabili kinda huyo aliyekuwa kicheza dabi ya kwanza.

Pambano hilo lililokuwa limejaa ufundi na ushindani kwa dakika zote 90, lilipigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na timu hizo kugawana pointi na kuzidi kuipa nafuu Yanga iliyopo kileleni ambao huenda kwa sasa wanaendelea kushangilia matokeo hayo.

Matokeo hayo yameifanya Simba kufikisha pointi 51 kupitia mechi 20, wakati Azam ikifikisha 44 kwa mechi 21 na kuipa nafuu Yanga iliyopo kileleni yenye pointi 55 kupitia michezo 21.

Katika pambano hilo la 34 la Mzizima tangu mwaka 2008, lilikuwa na ushindani kutokana na makocah wa timu zote kuwajaza viungo kama Mwanaspoti lilivyowajulisha mapema utamu utakuwa eneo la kati na viungo wa timu hiyo walifanya mambo yaliyowapa burudani mashabiki walijazana Kwa Mkapa.

Hii ni sare ya tatu kwa Simba na ya tano kwa Azam, huku ikishuhudiwa kipa Moussa Camara akitibuliwa rekodi yake ya kutoruhusu bao  na kumuacha kusaliwa na clean sheet 15.

Azam ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya kwanza tu mfungaji akiwa winga Djibril Sillah aliyepokea krosi safi ya mwenzake Idd Seleman ‘Nado’, kisha mfungaji kupiga shuti kisha kipaCamara kuokoa na kumkuta tena na kumalizia kirahisi, wageni wakifanya shambulizi la kushtukiza.

Bao hilo liliiamsha Simba ambayo ilianza kutembeza boli, huku Ellie Mpanzu alionekana kuwa msumbufu kwa mabeki wa Azam waliongoza na Yoro Diaby na Yeison Fuentes aliyerejea uwanjani baada ya kukosekana kwa mechi kadhaa kama ilivyokuwa kwa nahodha Lusajo Mwaikenda.

Dakika 24 baadaye Simba ikarudisha bao hilo kupitia Ellie Mpanzu aliyemalizia kiufundi na mguu wa kulia akipokea pasi safi ya winga Kibu Denis aliyewakimbiza wachezaji wa Azam kwa umbali mrefu wakilipa bao la shambulizi la kushtukiza matokeo yaliyomaliza kipindi cha kwanza.

Wawili hao walionekana kucheza kwa ushirikiano mkubwa na kuisumbua ngome ya Azam, japo mara kadhaa Kibu ambaye asisti hiyo ilikuwa ya kwanza, alikuwa akijiangusha mara nyingi hata kiguswa kidogo na mabeki wa Azam na kuwa faida kwa Simba.

Kipindi cha pili dakika ya 76 Simba ikapata bao la pili mfungaji akiwa beki Abdulrazack Hamza kwa kichwa akimalizia mpira wa adhabu ndogo ya Jean Charles Ahoua.

Hiyo ilikuwa ni asisti ya sita kwa Ahoua anayemiliki mabao 10 na kumfanya awe mchezaji aliyehusika mabao mengi akiwa na 16 kwa sasa.

Kuingia kwa bao hilo Azam ikafanya mabadiliko ilimtoa Sillah nafasi yake ikichukuliwa na Zidane Sereri aliyekuja kuwa mwokozi kwa timu yake akifunga bao la pili dakika ya 88 akimalizia krosi ndefu ya Feisal Salum ‘Fei toto.

Matokeo hayo yanaifanya timu hizo kufikisha sare Saba wakati Simba ikishinda mechi sita wakati Azam ikishinda mechi Moja ndani g mechi 14 walizokutana.

Vikosi vilivyoanza: SIMBA: Camara, Kapombe, Tshabalala, Hamza. Che Malone, Kagoma, Kibu, Ngoma, Ateba, Ahoua na Mpanzu

AZAM: Mustafa, Lusajo, Msindo, Yoro, Fuentes, Zayd, Idd Nado, Akaminko, Saadun, Fei Toto na Sillah

Related Posts