Simba V Azam FC… utamu upo kati

SIMBA imetamba leo itaendeleza Ubaya Ubwela pale ilipoishia wakati itakapokuwa wenyeji wa Dabi ya Mzizima dhidi ya Azam FC, huku Wanalambalamba wakijibu mapigo kwamba safari hii hawakubali unyonge mbele ya Mnyama.

Mechi hii namba 167 ilipangwa kupigwa Uwanja wa KMC Complex, kuanzia saa 10:00 jioni, lakini juzi Bodi ya Ligi (TPLB) ilitoa taarifa ya kuuhamisha hadi Kwa Mkapa na muda wa kuanza nao umebadilishwa na  sasa kuwa saa 1:00 usiku, ili wanaume hao waonyeshane kazi.

Hili ni pambano la 34 kwa timu hizo katika Ligi Kuu Bara tangu Azam ilipopanda daraja msimu wa 2008-2009, huku Simba ikibebwa na rekodi ya matokeo mazuri dhidi ya wapinzani wao hao wenye machungu ya kupoteza mechi ya kwanza ikiwa nyumbani kwa mabao 2-0.

Mechi ya kwanza kama ilivyo hii ya leo, nayo ilibadilishwa muda na uwanja, ikitolewa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na kupelekwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ikipigwa pia kutoka saa 1:00 usiku hadi saa 2:30 usiku wa Septemba 26, mwaka jana.

Katika mechi hiyo ya Zenji, Leonel Ateba alifunga bao la kwanza dakika ya 15 akimaliza pasi ya Jean Charles Ahoua kabla ya kiungo Fabrice Ngoma kufunga bao la pili dakika ya 47 na kuzima Azam.

Hata hivyo, katika pambano la leo ni wazi utamu utakuwa kwa eneo la kati kunakozalisha mabao mengi kwa timu hizo.

Fadlu David na Rachid Taoussi ni makocha wanaopenda kujaza viungo zaidi ambao wamekuwa wakizibeba katika kupata matokeo mazuri uwanjani na hata namba za wachezaji wa maeneo hayo zinasomeka vizuri zaidi kuliko hata kwa mafowadi.

Jean Ahoua anayehusika katika mabao 15 ya Simba akifunga 10 na kuasisti matano, hapishani sana na Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyehusika na mabao 14, akifunga manne na kuasisti 10, huku wakipigwa tafu na viungo wengine kama Ellie Mpanzu, Ladack Chasambi, Fabrice Ngoma na Yusuf Kagoma kwa Simba na Gibril Sillah, Idd Seleman ‘Nado’, James Akaminko na Yahya Zayd, kwa Azam ambayo itamkosa Adolph Mtasigwa aliye majeruhi kama straika Jhonier Blanco.

Mbali na viungo ambao ndio watengeneza mashambulizi ya timu hizo wakishirikiana na mabeki wa pembeni, Simba ikiwa na Shomary Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ wakati Azam ikiwa na Pascal Msindo, Nathaniel Chilambo kama sio Lusajo Mwaikenda, timu hizo zina mastraika wa mabao.

Simba ikitambia Leonel Ateba mwenye mabao manane na asisti tatu na Steven Mukwala aliyefunga matano, wakati Azam ina Nassor Saadun mwenye manne na Alassane Diao aliyerejea kutoka majeruhi anayemiliki bao moja kwa sasa.

Timu hizo leo zinakutana huku, Simba ikiwa nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi inayoongozwa na Yanga, ikimiliki pointi 50 kutokana na mechi 19, wakati Azam ipo nyuma yake na alama 43 zilizotokana na michezo 20, huku kila moja ikipambana kuwania ubingwa wa msimu huu.

Mara ya mwisho, Simba kutwaa ubingwa wa Bara ilikuwa 2020-2021 ilipotetea taji kwa msimu wa nne mfululizo, wakati Azam ilibeba taji hilo 2013-2014 na tangu hapo haijawahi kulibeba tena.

Timu zote zinatambia wachezaji wenye viwango vya hali ya juu kwa msimu huu, Simba ikiwa na mastaa kama Jean Ahoua mwenye mabao 10 na asisti tano, Leonel Ateba anayemiliki mabao manane na asisti tatu, mbali na wengine walioiwezesha timu hiyo kufukuzana na Yanga.

Kwa aina ya vikosi na timu hizo zinavyocheza, namba zinaonyesha Simba ni bora kulinganisha na wapinzani wao, kuanzia eneo la ulinzi hadi safu ya ushambuliaji, ingawa Dabi ya Mzizima huwa haitabiriki kirahisi.

Ukuta wa Simba ndio ulioruhusu idadi ndogo ya mabao hadi sasa, ikifungwa sita tu katika mechi 19, huku safu ya ushambuliaji ilifunga 41, wakati Azam imefungwa tisa kama ilivyo kwa Yanga, lakini imefunga 29 katika mechi 20 ilizocheza hadi sasa.

Hii ina maana Azam itakuwa na kazi ya kujilinda, lakini kutafuta mbinu za kuipenya ngome ya Simba iliyo chini ya kipa, Moussa Camara mwenye clean sheet 15 na mabeki wasiopitika kirahisi, huku Wekundu wakiwa na kazi moja ya kutaka kuendeleza ubaya ubwela ili ishinde na kuzidi kuibana Yanga kileleni.

Kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema mchezo huo utakuwa tofauti na ule wa Septemba 26, 2024 uliochezwa Zanzibar, kwani kocha wa Azam, Rachid Taoussi kipindi hicho hakupata muda mrefu wa kukaa na kujenga kikosi hicho tangu alipowasili kikosini.

“Nafikiri ilikuwa ni mechi ya pili au ya tatu kwake tangu ateuliwe, hivyo utaona bado alikuwa ni mgeni wa kuingiza falsafa zake vizuri, huu ni mchezo mwingine ambao sisi kama benchi la ufundi tunaenda kwa tahadhari kwa lengo la kupata pointi tatu,” alisema Fadlu aliyeiongoza Simba kushinda mechi 16, ikitoka sare mbili na kupoteza moja tu mbele ya Yanga katika Dabi ya Kariakoo ya Okt 19,2024.

Nahodha wa kikosi hicho, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, alisema mechi hiyo itakuwa tofauti na ile ya Zanzibar, ikitokana na mabadiliko makubwa ya kiuchezaji wa kikosi hicho kwa michezo ya hivi karibuni.

Kocha Taoussi alisema anatarajia mchezo mgumu na wenye ushindani, huku akiwapongeza Simba kwa kiwango bora wanachoendelea kukionyesha hasa michuano ya kimataifa wakiwa hatua ya robo fainali.

“Tunaenda kucheza na timu yenye wachezaji wazuri na wenye shauku kubwa ya kupata matokeo chanya, lakini kama ninavyosema kila siku, tupo tayari kwa changamoto mpya na tumeandaa mikakati mizuri ya kuhakikisha tunashinda mchezo huo muhimu.”

Aidha, Taoussi alisema katika mchezo huo atamkosa kiungo nyota wa kikosi hicho, Adolf Mtasingwa aliye majeruhi, japo anajivunia wengine waliopo katika eneo hilo akiwamo Yahya Zayd aliyefiti kwa sasa.

Nahodha na beki wa timu hiyo, Lusajo Mwaikenda alisema maandalizi kiujumla yamekamilika na wanaenda katika mchezo huo kwa ajili ya kulipa kisasi kwa kile kilichotokea mechi ya mwisho, licha ya kukiri ugumu na ubora wa washambuliaji wa Simba hadi sasa.

Related Posts