TIMU YA WASHAURI KUTOKA AfDB YAVUTIWA NA UKUAJI WA UCHUMI

Washauri Waandamizi wa Wakurugenzi Watendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) wameanza ziara ya siku tano nchini kwa ajili ya kuelewa vipaumbele vya maendeleo ya Tanzania na namna AfDB inavyoweza kuchangia shughuli zenye matokeo chanya na kubadilisha maisha ya watanzania.

Akizungumza kuhusu ziara hiyo, baada ya kukutana na ujuembe huo jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, alisema kuwa ziara ya Washauri hao ni sehemu ya ajenda ya kila mwaka ya Bodi ya Wakurugenzi Watendaji wa AfDB katika nchi wanachama wa Kanda.

Alisema pamoja na kuelewa vipaumbele hivyo, washauri hao watapata fursa ya kuelezewa mwenendo wa uchumi wa nchi, kujadili miradi inayotekelezwa nchini kwa kushirikiana na Benki hiyo ikiwa ni pamoja na kuangalia changamoto zilizopo na namna ya kuzitatua.

“Uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa imara ambapo kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2024 uchumi umekua kwa asilimia 5.4 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.8 kwa mwaka 2023, ambapo ukuaji huo umechochewa na uwekezaji kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na miradi ya nishati, maendeleo ya jamii na miundombinu ya usafirishaji”, alisema Bi. Shaaban.

Aidha, alieleza kuwa mfumuko wa bei umeendelea kuwa imara kwa wastani wa asilimia 3.1 kwa mwaka 2024 ikilinganishwa na asilimia 3.8 kwa mwaka 2023.

Vilevile alisema kuwa Tanzania inatekeleza zaidi ya miradi 29 Tanzania Bara na Zanzibar ikiwa na thamani ya takribani dola za Marekani bilioni 3.91 ikiwemo ya maji, miundombinu, nishati, kilimo, sekta binafsi na uendelezaji wa ujuzi, iliyosainiwa kati ya mwaka 2015 na 2025.

Kwa upande wake Kiongozi wa Timu ya Wataalam ya Washauri wa Wakurugenzi Watendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Bi. Betty Ngoma, alisema kuwa, wamekuja Wizara ya Fedha ili kujua maendeleo ya uchumi lakini pia mikakati mbalimbali inayotumika katika kukuza uchumi wa nchi.

Bi. Ngoma, ameipongeza Tanzania kwa namna inavyoimarisha uchumi wake na namna ilvyoweza kusimamia vema utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inatekelzwa kupitia ufadhili wa Benki hiyo.

Alisema wapo nchini ili waweze kujionea miradi inayotekelezwa kwa ufadhili wa Benki hiyo Tanzania Bara na Zanzibar na kujionea juhudi zinazofanywa na Serikali katika kukuza uchumi wake.

Related Posts