UJUMBE WA TANZANIA NCHINI MALAWI WASISITIZWA KUTUMIA JUKWAA LA JPCC KUIBUA MAENEO YENYE TIJA YA USHIRIKIANO.

Ujumbe wa Tanzania utakaoshiriki Mkutano wa Sita wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Malawi wamesisitizwa kutumia Mkutano huo kuibua na kuendeleza maeneo muhimu ya Ushirikiano yenye manufaa kwa mataifa hayo.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, alipowasili jijini Lilongwe, Malawi na kuzungumza na ujumbe wa Tanzania katika kikao kilichofanyika katika makazi ya balozi wa Tanzania nchini humo.

Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Mussa alisisitiza kuwa Mkutano huo ni fursa muhimu ya kuboresha uhusiano wa pande zote mbili kwa faida ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii.

Aliwasihi wajumbe wa Tanzania kuwa mstari wa mbele kuwasilisha hoja zenye manufaa kwa Tanzania.

“Ni muhimu kwa kila mmoja wetu kutambua malengo ya safari hii na kuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya nchi kwa kuzingatia maeneo muhimu hususan biashara, miundombinu, amani na usalama, kilimo, viwanda, nishati na gesi hivyo ni kuhakikisha hoja hizi zinazingatiwa,” alisema Balozi Mussa.

Aidha, amefafanua kuwa mkutano huo pia utatoa fursa kwa pande zote mbili kupitia makubaliano yaliyofikiwa katika mikutano iliyopita na kutathmini utekelezaji wake, pamoja na kuweka mikakati mipya ya ushirikiano kwa kuzingatia kipaumbele maalum kwenye maeneo mbalimbali hususan diplomasia, Siasa, uchumi, miundombinu na mawasiliano, masuala ya kijamii na kibinadamu, ulinzi na usalama pamoja na utatuzi wa changamoto za kikanda.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb), anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi nchini Malawi kuanzia tarehe 25 ambapo atashiriki mkutano ngazi ya Mawaziri wa Sita wa Tume ya kudumu ya pamoja ya ushrikiano kati ya Tanzania na Malawi utakaofanyika tarehe 26 Februari 2025. Mkutano huo utatanguliwa na vikao vya Maafisa Waandamizi vitakavyofanyika tarehe 24 na 25 Februari 2025.

 

Related Posts