Dar es Salaam. Uwekezaji katika tafiti za kisayansi, umeelezwa utasaidia kuchangia usimamizi na utekelezaji wa sera katika kuboresha na kukuza sekta ya uchumi wa buluu.
Wakati huohuo kuunganisha watafiti, wajasiriamali na watunga sera katika ushirikiano wa sayansi na biashara kunatajwa kutoa suluhisho linaloweza kupanuliwa kwa changamoto zilizopo kwa sasa.
Hayo yameelezwa leo Jumatatu, Februari 24, 2025 na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti wakati wa uzinduzi wa wiki ya Bahari Endelevu na kongamano la ushirikiano linalolenga kuharakisha na kupanua suluhisho chanya kwa mazingira, tabianchi na jamii katika bara la Afrika.
Amesema Serikali inatambua umuhimu wa kushughulikia changamoto za uchumi wa buluu kupitia ushirikiano, uvumbuzi na uwekezaji katika sayansi na teknolojia.
“Lazima tuendeleze suluhisho za baharini zinazolinda mazingira na kuwezesha jamii za pwani. Hili ndilo serikali ya Tanzania Bara na Zanzibar wanahimiza. Tafiti zimekuwa zikifanywa na Serikali itaendelea kufanya tafiti zaidi.
“Kwa kuonesha dhamira hii, Serikali imeanzisha mpango wa Building Better Tomorrow (BBT), ambao ni wa miaka minane 2022-2030, unaolenga kuwanoa vijana na wanawake kupitia mafunzo ya vitendo,” amesema.
Mnyeti amesema kwa kutambua hilo, leo katika ziara yake mkoani Tanga, Rais Samia Suluhu Hassan atakabidhi boti 30 na mitumbwi 60 ya uvuvi, ikiwa ni awamu ya pili ya mpango wa BBT.
Kwa mujibu wa Mnyeti, kupitia mpango huo, Tanzania inalenga kuwawezesha vijana na wanawake kwa maarifa, ujuzi na fursa za kushiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa buluu endelevu.
Kipo kituo cha utafiti kinaendelea na zimekuwa zikifanyika na zinafanyiwa kazi, utafiti ni suala endelevu huwezi kulimaliza
Mkurugenzi mkaazi wa programu maalumu kutoka Bahari Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini IUCN ESARO, Elinasi Monga amesema watafiti, watunga sera na wafanyabiashara za uchumi wa buluu kwa miaka mingi wamekuwa wakifanya kazi bila ushirikiano.
Amesema mkutano huo unaangalia namna gani tafiti zinaweza zikachangia uangalizi na utekelezaji wa sera na pia jinsi gani zinaweza kuboresha biashara ya uchumi wa buluu.
“Masuala ya utafiti hayawezi kufanywa na mtu mmoja, kuna umuhimu wa makundi haya kuzungumza, watu wa sera waseme maeneo gani bado yana upungufu wa taarifa, tafiti zifanywe zitakazojibu maswali sababu kuna changamoto nyingi zinahitaji majibu.
“Tunalima mwani kwa mbegu kutoka Asia, lakini kwa sasa mbegu hiyo ina changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi na magonjwa, wanaweza kugundua mbegu bora za asili za mwani tunazoweza kuzitumia kuongeza uzalishaji, lakini pia mbegu bora za asili kutoka Tanzania zinazoweza kukabiliana na magonjwa,” amesema Monga.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (Tafiri), Dk Ismael Kimirei amesema mpango bunifu waliouzindua (The BAHARI Accelerator) unalenga kufanikisha biashara zinazotokana na tafiti za kisayansi katika uchumi wa buluu.
“Unalenga kuunganisha tafiti na suluhisho za kibiashara, na hivyo kusaidia ajira, ustahimilivu wa kiuchumi na maendeleo endelevu ya jamii za pwani,” amesema.
Pia amesema kupitia mpango huo bunifu Tafiri watachukua matokeo ya utafiti ambayo ni bunifu kuyawekea msingi, kuwasaidia wabunifu wanaotaka kukuza biashara zao kutoka kwenye wazo kwenda kutengeneza mradi kama biashara.
Katika ushirikiano wa kimataifa, Mkuu wa Ushirikiano katika Ubalozi wa Canada nchini Tanzania, Carol Mundle amesema kupitia mpango wa Canada wa Partnering for Climate, wamekuwa wakisaidia miradi bunifu ya bahari kama ReSea Project, inayosimamiwa na Mission Inclusion na Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN).
“Ushahidi unaonesha kuwa mbinu za urejeshaji wa mifumo ya bahari zinatoa fursa endelevu kwa jamii za pwani na viumbe wa baharini. Tunapowekeza katika suluhisho za kiasili na kuwawezesha viongozi wa jamii, hususan wanawake na vijana, tunasongesha lengo letu la pamoja,” amesema Mundle.