Upelelezi kesi ya kumiliki kobe 116,  bado ‘kiza’

Dar es Salaam. Serikali imeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi katika kesi ya kuongoza genge la uhalifu na kumiliki kobe 116 inayowakabili watu wanane wakiwemo maofisa wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere( JNIA) pamoja na raia wa Ukraine, haujakamilika.

Wakili wa Serikali, Gloria Kilawi ameieleza Mahakama leo Jumatatu Februari 24, 2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga, ilipoitwa kwa kutajwa.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni mfanyabiashara, Josephat Moyo (52) mkazi wa Tabata, Deogratius Lugeng’a (40) mfanyabiashara na mkazi wa Kipunguni pamoja na ofisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania( JWTZ) mwenye namba MT 88046 Sajent  Cosmas Ndomba(39) mkazi wa Kivule.

Wengine ni ofisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) mwenye namba MT 118102, Kassim Abdallah (35) ambaye pia ni  Ofisa Usalama wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere( JNIA) na mkazi wa Tabata Segerea.

Washtakiwa wengine ni Nkanamuli Mgaza (52) ambaye ni Ofisa Usalama Uwanja wa Ndege wa JNIA,  Stephano Chedego (51) mkulima na mkazi wa Dodoma,  Mwaluko Mgomole (41) mkulima na mkazi wa Dodoma pamoja na raia wa Ukraine, Olga Kryshtopa (35) mwenye makazi yake Kiev – Ukraine.

Kilawi amedai kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado unaendelea, kwa hiyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Ruboroga  baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 10, 2025 kwa ajili ya kutajwa.

Mshtakiwa wa kwanza hadi wa sita wapo nje kwa dhamana, isipokuwa Mgomole ambaye  yupo rumande baada ya kufutiwa dhamana na Mahakama kutokana na kutoroka akiwa nje kwa dhamana.

Pia mshtakiwa Kryshtop yeye dhamana yake ilizuiliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) baada ya kuwasilisha maombi maalumu mahakamani hapo.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matatu likiwemo la kuongoza genge la uhalifu na kumiliki nyara za Serikali katika kesi ya uhujumu uchumi namba 1/2023.

Katika shitaka la kwanza, ambalo ni kuongoza genge la uhalifu, washtakiwa wanaodaiwa kutenda kosa hilo katika tarehe tofauti, kati ya Januari 2022 hadi Julai 2022, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere( JNIA) uliopo wilaya ya Ilala.

Inadaiwa katika kipindi hicho, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kukusanya, kununua na kusafirisha nyara za Serikali ambazo ni kobe, kinyume cha sheria.

Shitaka la pili ni kuteka nyara za Serikali, tukio wanalodaiwa kulitenda katika tarehe hizo JNIA, ambapo walinunua, kukusanya na kuuza kobe 116  wenye thamani ya Sh18.93 milioni bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Shitaka la tatu ni kumiliki nyara za Serikali kinyume cha sheria, tukio wanalodaiwa kulitenda Julai 3, 2022 uwanjani hapo.

Inadaiwa siku hiyo ya tukio washtakiwa kwa makusudi walikutwa wakimiliki kobe 116, bila kuwa na kibali cha Serikali.

Related Posts