Bariadi. Wafanyabiashara wa mazao mchanganyiko katika Mkoa wa Simiyu wameeleza changamoto wanazokutana nazo kutumia Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani, huku Serikali ikisisitiza umuhimu wa mfumo huo.
Hayo yamebainika leo Februari 24, 2025 mjini Bariadi mkoani Simiyu katika mkutano wa wafanyabiashara hao na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kighahe.
Baadhi ya wafanyabiashara wa mkoa wa Simiyu, wakati wa kikao cha pamoja na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara,Exaud Kighahe(hayupo pichani)Picha na Samwel Mwanga
Miongoni mwa malalamiko yao ni kuwepo kwa vikwazo vingi, ikiwemo hitaji la mtaji mkubwa kama dhamana hali inayowafanya wakulima wengi kushindwa kumudu mfumo huo na hivyo kuuza mazao yao holela.
Pia, umbali wa maghala yaliyosajiliwa na TMX unaleta ugumu kwa wakulima kufikisha mazao yao kwa urahisi.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara mkoani humo, John Sabu amesema kuwa mfumo hauna mazingira rafiki ya ufanyaji wa biashara kutokana na kuwekwa kwa vikazo vingi, hivyo walio wengi wanashindwa kuumudu.
“Awali, tulipokaa na mkuu wetu wa mkoa, viongozi wetu wakishirikiana na wataalamu walitueleza kuwa mfumo huo utapunguza vikwazo vya kifedha kwa kuweka masharti nafuu ya dhamana na mtaji ili kuwawezesha wakulima na wafanyabiashara wadogo kushiriki kikamilifu katika mfumo wa stakabadhi ghalani.
“Lakini sasa tumeingia sisi wafanyabiashara kwenye ununuzi wa mazao hayo, hali ni tofauti kabisa na maelezo tuliyopatiwa, jambo linalotukatisha tamaa na tumefikia hatua kushindwa kuielewa hii Serikali yetu maana tumekuwa kama sisi si Watanzania,” amesema.

Mfanyabiashara,Issa Mohamed wa mji Bariadi akizungumza wakati wa kikao cha wafanya biashara wa mkoa wa Simiyu waliokutana na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara,Exaud Kighahe(hayupo pichani)Picha na Samwel Mwanga
Naye Mohamed Issa ambaye ni mfanyabiashara wa mjini Bariadi, amesema katika kuboresha miundombinu ya maghala walielezwa ya kuwa yatakuwa karibu na wakulima ili kupunguza umbali, lakini suala hilo halijatekelezwa na baadhi ya maghala yamekuwa umbali wa kilomita 40 kutoka kwa wakulima.
“Serikali ilisisitiza umuhimu wa kuwekeza kwenye maghala ya kisasa ili kuhakikisha uhifadhi bora wa mazao na kurahisisha upatikanaji wa masoko sambamba na kujengwa karibu na wakulima, lakini mengi yapo umbali mrefu, hivyo kumchosha mkulima kubeba mazao yake na kuyapeleka,” amesema.
John Matagulwa ni mfanyabiashara kutoka Wilaya ya Maswa, amesema kuwa Serikali ilipaswa kwanza kutoa elimu na uhamasishaji juu ya mfumo huo na kuhakikisha wadau wote wanauelewa kuliko hali ilivyo sasa ambapo umekumbwa na changamoto nyingi.
“Elimu na uhamasishaji ingetolewa kwa wakulima na wafanyabiashara kuhusu faida na matumizi sahihi ya mfumo wa stakabadhi ghalani na TMX ili kuongeza uelewa,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga amesema kuwa Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa mfumo wa stakabadhi ghalani katika kuboresha sekta ya kilimo na biashara ya mazao.
“Mfumo huu umetusaidia kudhibiti biashara holela ya mazao na kuhakikisha wakulima wanapata bei nzuri na halmashauri zinaongeza mapato,” amesema.
Akizungumzia malalamiko hayo, Waziri Kighahe amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (Copra), imeanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani na minada ya kidijitali kupitia TMX kwa lengo la kulinda masilahi ya wakulima na wafanyabiashara.
Amesema mfumo huo unalenga kuongeza uwazi katika biashara ya mazao, kuhakikisha wakulima wanapata bei nzuri na kutoa takwimu sahihi za masoko na uzalishaji.
“Hata hivyo, kutokana na changamoto mlizozitaja hapa wafanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu zinaonyesha kuwa mfumo huu bado unahitaji maboresho zaidi katika utekelezaji wake, hivyo niuombe uongozi wa mkoa ukae chini tena na hawa wafanyabiashara na kuona njia sahihi za kutekeleza mfumo huu,” amesema.
Amesema kwa kushughulikia masuala haya, mfumo wa stakabadhi ghalani utakuwa chachu ya maendeleo katika sekta ya kilimo kwa kuhakikisha wakulima na wafanyabiashara wanapata faida stahiki na kuinua uchumi wa mkoa huo.