FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Wafanyakazi nchini wametakiwa kuanza maandalizi ya kustaafu mara tu wanaposaini mkataba wa ajira ili kujijengea mazingira bora ya maisha baada ya kumaliza utumishi wao.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Utafiti na Mazingira (RAAWU) Tawi la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Faraja Kamendu, wakati wa semina ya wanachama wa chama hicho iliyofanyika katika Kampasi ya Edward Moringe, Morogoro.
Kamendu amesema RAAWU imeamua kuandaa semina hiyo baada ya kufanya tafiti mbalimbali na kubaini kuwa wafanyakazi wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu maandalizi ya kustaafu na uwekezaji wanapokuwa kazini. Hivyo, mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha wastaafu watarajiwa kuelewa mazingira yao baada ya kustaafu na kujipanga vyema ili kuepuka changamoto za kifedha.
Kwa upande wake, Katibu wa RAAWU Mkoa wa Morogoro, Bi. Agness Gwau, amesema uongozi wa chama hicho umeona umuhimu wa kutoa mafunzo hayo ili kuwajengea wafanyakazi misingi bora ya uwekezaji. Ameongeza kuwa chama kitaendelea kuandaa mafunzo kama haya mara kwa mara ili kuwajengea wanachama wao uwezo wa kiutendaji.
Aidha, wafanyakazi wapya na wale waliohama kada wametakiwa kujiunga na vyama vya wafanyakazi ili kuwa na sauti ya pamoja mahali pa kazi. Hii itawawezesha kuboresha mazingira ya kazi kwa kuzingatia haki na wajibu wao.
Mmoja wa washiriki wa semina hiyo, Haroun Kapingo, ambaye ni mtumishi wa SUA, amesema mafunzo hayo yamekuwa yenye manufaa makubwa. Ameeleza kuwa semina imewapa uelewa wa haki na wajibu wao kama wafanyakazi, pamoja na mbinu bora za kujiandaa kwa uwekezaji kabla ya kustaafu.
Semina hiyo ya siku mbili, iliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya RAAWU Makao Makuu na RAAWU Tawi la SUA, imewajengea washiriki uelewa kuhusu vyama vya wafanyakazi, mbinu za kukuza taaluma kazini, na maandalizi ya maisha baada ya kustaafu.