Dar es Salaam. Wajasiriamali wadogo nchini wametakiwa kusimamia vyanzo yao vya mapato na kujihusisha na mikopo endelevu kutoka kwenye taasisi za kifedha zinazoaminika ili kulinda biashara zao.
Hayo yameelezwa wakati wa hitimisho la mafunzo maalumu ya wajasiriamali vijana katika kampeni maalumu ya Going Beyond iliyoandaliwa na taasisi ya Her initiative ambapo, mtalaamu wa masuala ya fedha, James Manyama amesema watu wengi mitaji yao inakufa kutokana na kutojua namna ya kupata, kulinda na kuendeleza mitaji yao.
Katika mahafali hayo yaliyofanyika leo Februari 24, 2025 jijini hapa, wataalamu mbalimbali wa kifedha waliwaeleza wahitimu hao umuhimu wa kusimamia biashara zao kikamilifu katika ngazi zote za wali ili kuhakikisha ukuaji thabiti.
“Kutokana na shughuli zao za ujasiriamali ni vyema wasijiingize kwenye mikopo umiza kwani wataenda kuua biashara zao, muhimu zaidi watumie sekta ya fedha rasmi ili kupata huduma za nzuri za kifedha,” amesema Manyama.
Ameongeza kuwa ni muhimu wajasiriamali wadogo wawe na utaratibu wa kujiwekea akiba kwani kufanya hivyo itakuwa rahisi kwao kujipatia mikopo kutoka taasisi za kifedha zinazoaminika.
Akitoa maoni yake kuhusu mafunzo hayo, mmoja wa washiriki, Scola Wales amesema kuwa amenufaika vyema na matumizi ya mitandao ya kijamii katika kukuza na kuendeleza biashara yake.
“Ninafanya biashara ya nguo maeneo ya Mwenge nimeona mwanga wa kutumia mitandao ya kijamii kuboresha huduma hasa kwenye upande wa delivery (kufikisha mzigo) kiukweli nimehamasika sana, sasa nitahudumia walio maeneo ya karibu na mbali bila shida, yoyote,” amesema Scola.
Mustapha Ramadhani, ameshukuru kwa mafunzo aliyoyapata kwani anaamini yatakwenda kubadilisha mwenendo wa biashara yake mara baada ya kupata elimu ya ujasiriamali mtandaoni.
Kwa upande wa Mkufunzi wa mradi huo Zafarani Juma, amesema mafunzo hayo yaliwafikia vijana 1, 575 yalifanyika kwa miezi sita ikihusisha mikoa mitatu ambayo ni Dar es Salaam, Arusha na Morogoro.