Shinyanga. Wakulima wa zao la matikiti katika Kijiji cha Kishapu kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, wanalazimika kujenga mahema mashambani ili kukabiliana na uharibifu wa zao hilo unaofanywa na fisi.
Hayo yamebainishwa leo Februari 24, 2025 na Katibu wa kikundi cha Jipagile kilichopo katika kijiji hicho, Samwel Lusona amesema fisi hao hula matikiti hayo usiku, jambo linalosababisha uharibifu wa zao hilo.
Amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo, wamelazimika kuweka mahema karibu na mashamba yao ili kupata urahisi wa kuamka usiku kulinda mazao yao.
“Hapa tuna changamoto ya fisi kushambulia mazao yetu ya bustani, kwa mfano kama kipindi hiki matunda yamekomaa, fisi wakipita wanakula na mengine wanayauma na kuyaacha, inakuwa hasara kwetu na ndiyo maana tunalinda,” amesema Lusona.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha akiwa amebeba tikiti maji baada ya kutembelea shamba la kikundi cha Jipagile.
Mkulima mwingine, Ally Mfaume ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Kishapu, amesema mbali na fisi kusumbua, kilio chao kikubwa ni kupata kisima cha maji kutokana na kuwa na changamoto ya maji ya kumwagilia hasa wanapolima wakati wa kiangazi.
“Ombi letu kubwa ni kupata soko la uhakika maana tunazalisha matikiti maji mengi ambayo kwa sasa tunatafuta masoko maeneo mbalimbali na kwa mwaka tunalima mara tatu na changamoto nyingine ni maji, tungepata kisima kirefu ingetusaidia,” amesema Mfaume.
Amesema awamu ya kwanza mwaka 2023 walivuna matikiti 11,000 kutoka ekari tisa walizokuwa wamelima na kupata Sh22 milioni baada ya kuuza kwa Sh2,000.
Amesema mwaka 2024 walilima ekari 16 na kupata matikiti 25,100 ambapo waliuza kwa Sh3,000 na kupata Sh75.3 milioni ambazo zimewawezesha kuendelea kufanya kazi nyingine za maendeleo.
Ofisa Kilimo na Mratibu wa Mazao ya Bustani Wilaya ya Kishapu, Deus Gomba amekiri kuitambua changamoto ya fisi kushambulia zao hilo, ambapo wakulima wamekuwa wakikabiliana nalo kwa kujenga mahema mashambani.
Hivi karibuni, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha aliwatembelea wakulima hao na kuwahakikishia kuwa Serikali itawawekea miundombinu mizuri ya maji kwa kuchimba kisima kirefu.