Kyiv. Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesema kuwa yuko tayari kujiuzulu wadhifa huo, ikiwa uamuzi huo utarejesha amani nchini mwake.
Shirika la Associated Press limeripoti kuwa, Zelensky pia amesema kuwa yuko tayari kung’atuka endapo tu Ukraine itakubaliwa kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi (Nato).
Alipoulizwa kwenye mkutano wa waandishi wa habari kama yuko tayari kuachia madaraka ikiwa hilo litahakikisha amani kwa Ukraine, Zelensky amesema: “Kama itahakikisha amani kwa Ukraine, kama mnahitaji kweli nijiuzulu, niko tayari. Naweza kubadilishana hilo pia kwa uanachama wa Nato.”
Awali, Zelensky alisema jeshi la nchi yake litahitaji kuongezeka maradufu endapo Nato itakataa kuiingiza Ukraine kwenye umoja huo.
Mapema mwezi huu, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth alisema kwamba Ukraine kujiunga na Nato si jambo linalowezekana kwa sasa.
Kauli ya Zelensky imekuja baada ya mvutano kuongezeka kati yake na Donald Trump, baada ya Rais huyo wa Marekani kumtuhumu kuwa aliichokoza Russia na kuanzisha vita ambavyo alijua kuwa kamwe hawezi kushinda.
Baadaye Trump alimlaumu mtangulizi wake, Joe Biden na Zelensky kwa kushindwa kukomesha mapigano mapema kabla madhara hayajawa makubwa.
Kutokana na kauli hiyo, Zelensky alimjibu Trump akimshutumu kuwa anafanya maamuzi yake kwa kuzingatia taarifa za upotoshaji anazopatiwa na hasimu wake, Rais Vladimir Putin wa Russia.
Hivi karibuni maofisa wa Marekani na Russia walikutana Saudi Arabia na kufanya mazungumzo ya awali kuhusu mkakati wa kumaliza vita hiyo, huku Ukraine ikitengwa kushiriki mkutano huo jambo lililozua hofu miongoni mwa washirika wa Ulaya.
Jumapili, Zelensky alisema mbinu yake kwa utawala wa Trump ni ya kivitendo. “Hakuna nafasi ya hisia hapa,” alisema Zelensky.
Akijibu kauli za Trump kuhusu yeye, kiongozi huyo wa Ukraine alisema: “Ni wazi, siwezi kusema kwamba maneno ya Rais Trump kuhusu mimi ni pongezi na hilo nalisema hadharani kabisa.”
Shambulio kubwa la ndege zisizo na rubani la Russia
Usiku wa kuamkia Jumapili, Russia ilipeleka mashambulizi nchini Ukraine kwa kutumia ndege zisizo ya rubani (droni) zaidi ya 267 na kusababisha kifo cha mtu mmoja huku kadhaa wakijeruhiwa.
Rais Zelensky alisema: “Kila siku, watu wetu wanapambana na ugaidi wa anga,” huku akiongeza kuwa shambulio hilo lilikuwa kubwa zaidi tangu droni za Russia zilipoanza kushambulia miji na vijiji vya Ukraine.
“Tunapaswa kufanya kila liwezekanalo kuleta amani ya kudumu na ya haki kwa Ukraine. Hili linawezekana kupitia mshikamano wa washirika wote tunahitaji nguvu za Ulaya, Amerika, na nguvu za kila mtu anayetaka amani ya kudumu,” Zelensky alichapisha kwenye akaunti yake ya Mtandao wa X.
Mkuu wa Idara ya Ujasusi ya Ukraine (SBU) Kyrylo Budanov, aliita shambulio hilo la usiku kuwa ni njia ya vitisho na matendo ya kigaidi dhidi ya nchi yake.
Tangu Russia itangaze kuanzisha operesheni yake ya kijeshi nchini Ukraine imeyatwaa maeneo ya mkoa wa Donetsk, Luhansk, Kherson, Pokrovisk, Zaporizhia na Crimea iliyotwaliwa tangu mwaka 2022.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.