Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb), amesema kuwa Tanzania imeendelea kuweka kipaumbele katika uendelezaji na ulinzi wa Haki za Binadamu katika utekelezaji wa shughuli za Serikali.
Akizungumza wakati akiiwakilisha Tanzania katika Kikao cha 58 cha Haki za Binadamu kinachofanyika Geneva, Uswisi, Waziri Ndumbaro amesema kuwa kupitia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Tanzania imeendelea kusimamia utu wa kibinadamu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu.
Hii inaendana na mkakati uliopitishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, unaojikita katika “4Rs,” yaani Maridhiano, Uthabiti, Mageuzi, na Kujenga Upya.
Akiwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa Haki za Binadamu katika Hifadhi ya Ngorongoro, Waziri Ndumbaro amesema kuwa Serikali ya Tanzania imeendelea kuweka uwiano sawa kati ya Haki za Binadamu na maisha kwa kuzingatia uhifadhi.
Waziri Ndumbaro amefafanua kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kusimamia Haki za Binadamu Ngorongoro, alikutana na viongozi wa vijiji na kimila, kusikiliza kero zao, na kuanzisha timu mbili za ushauri: moja kuhusu masuala ya ardhi na nyingine kuhusu mpango unaoendelea wa kuwahamisha wakazi wa Ngorongoro kwenda Msomera.
Aidha, Waziri Ndumbaro ameongeza kuwa lengo la jitihada hizo ni kuhakikisha zoezi la hiari linafanyika kwa urahisi na kero za wananchi zinashughulikiwa.
Maeneo mengine ya usimamizi wa Haki za Binadamu yaliyowasilishwa katika mkutano huo ni pamoja na kufanya uchaguzi huru na haki kila baada ya miaka mitano, uhuru wa vyombo vya habari na kujieleza, kulinda haki za makundi hatarishi, ukiwemo ustawi wa watu wenye ualbino na usaidizi kwa watu wenye ulemavu.