Bei vifaa vya ujenzi juu licha ya viwanda kuongezeka

Dar es Salaam. Licha ya ongezeko la uzalishaji katika vifaa vya ujenzi nchini, watumiaji hawaoni faida kwa kuwa bei za bidhaa hizo bado iko juu, hivyo kusababisha wenye nyumba kuongeza gharama za upangishaji.

Kwa miaka 10 iliyopita, takwimu rasmi kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara zinaonyesha uzalishaji wa saruji umeongezeka zaidi ya mara mbili kutoka tani milioni 4.4 hadi tani milioni 9.1.

Hata hivyo, wadau wanataja ushuru na changamoto nyingine za kiutendaji zinawalemea wazalishaji jambo linalopunguza uwezekano wa kupungua bei, huku Serikali ikisema yapo mambo mengi yanayoathiri mabadiliko ya gharama.

Kwa mujibu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, jitihada zinaendelea kufanywa ili kuhakikisha ukuaji wa viwanda unaleta manufaa kwa walaji wa mwisho.

Kuhusu nondo, mahitaji ya ndani kila mwaka hadi kufikia Machi, 2024 yalikuwa tani 605,369.6.

Uzalishaji huu wa ndani unakidhi mahitaji na kuwapo ziada ya tani 294,630.4 inayosafirishwa kwenda nchi jirani kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi na Rwanda.

Pamoja na hayo, bei ya nondo imepanda, huku yenye upana wa milimita 12 ikiuzwa kati ya Sh22,000 na Sh25,000 kulingana na mkoa.

Utafiti uliofanywa na Gazeti la The Citizen, umebaini bei ya saruji imepanda katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kutoka Sh12,000 kwa mfuko hadi kati ya Sh14,500 na Sh17,000. Kwa baadhi ya mikoa imeshuhudiwa bei inayozidi Sh20,000.

Bei ya nondo nayo imeongezeka, gharama kwa tani ikipanda kutoka Sh1.8 milioni hadi takribani Sh2.4 milioni.

Wateja wanakiri kushuka kidogo kwa bei ya saruji, hata hivyo wanaeleza kupungua huko hakuakisi ongezeko la idadi ya viwanda nchini.

Akizungumza na Mwananchi, jana Jumatatu Februari 24, 2025, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Neepeace Wambuya amesema hali hiyo ya bei imechangiwa na mambo mbalimbali ya nje na ndani, ikiwa ni pamoja na kukosekana ufanisi katika usambazaji, athari za kijiografia, mwelekeo wa uchumi wa dunia na viwango vya ubadilishaji fedha za kigeni.

“Mahitaji ya vifaa vya ujenzi bado ni makubwa kutokana na ukuaji wa kasi katika sekta hiyo, jambo linaloleta vikwazo vya usambazaji. Hata hivyo, mahitaji haya pia yanachochea ongezeko la uwekezaji katika sekta hii, ambao unapaswa baada ya muda, kuboresha ufanisi na usambazaji,” amesema.

Amesema Serikali inajitahidi kuboresha ugavi, kuongeza uwazi wa bei na kuhakikisha njia bora za usambazaji kusaidia kuleta utulivu wa bei.

Wambuya amesema juhudi zinaendelea kupunguza utegemezi wa malighafi zinazoagizwa kutoka nje, wakati ambao Serikali inakamilisha makubaliano na wawekezaji wa miradi ya chuma ya Liganga na makaa ya mawe ya Mchuchuma, ambayo yatarahisisha uzalishaji wa chuma wa ndani na kupunguza gharama kwa muda mrefu.

Ili kuboresha hali ya biashara, amesema mamlaka zinaendelea kutekeleza mpango wa kuboresha biashara unaolenga kupunguza vikwazo vya kufanya biashara.

Wambuya amesema uhakiki wa sera ya viwanda unakaribia kukamilika ili kuendana na mwelekeo wa kimataifa na maendeleo ya teknolojia.

Katika hilo, wataalamu wa sekta wanaeleza kodi na teknolojia iliyopitwa na wakati huchangia kuongeza gharama.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Vijay Contractors, Joseph Magida anaamini msamaha wa kodi kwenye vifaa vya ujenzi unaweza kupunguza ukali wa bei.

“Serikali inahitaji kuzingatia afua, vinginevyo watu wengi hawataweza kumudu nyumba. Ukiwa na Sh20 milioni unaweza tu kujenga nyumba ndogo kwa bei ya sasa,” amesema.

Amesema utegemezi wa malighafi zinazoagizwa kutoka nje ya nchi na kushuka kwa viwango vya ubadilishaji fedha za kigeni unaendelea kuongeza gharama.

Mkurugenzi Mkuu wa Joint Consult Limited, Alex Silayo amesema gharama kubwa za uendeshaji zinafanya iwe vigumu kwa viwanda kupunguza bei licha ya kuongezeka kwa uzalishaji.

Kwa upande wake, mkazi wa Goba, Adeline Tarimo amesema kupanda kwa gharama za vifaa vya ujenzi kunawakatisha tamaa vijana kujenga nyumba za makazi.

“Nilianza kujenga nyumba ya vyumba vitatu mwaka 2020, lakini imekuwa ngumu. Bei ya chuma imepanda kwa kiasi kikubwa, hasa kutokana na kupanda kwa kiwango cha ubadilishaji wa fedha,” amesema.

Amesema kupanda kwa gharama za ujenzi kunaongeza bei ya kupangisha kwa wenye nyumba kutafuta mapato ya haraka kwenye uwekezaji.

“Tuna viwanda vingi, lakini bei bado iko juu. Mengi zaidi yanahitajika kufanywa ili kuipunguza,” amesema.

Related Posts