Na mwandishi wetu.
Benki ya Absa Tanzania imesema itaendelea kuunga mkono juhudi mbalimbali zenye lengo la kuhakikisha wanawake wa Tanzania wanapiga hatua za kimaendeleo mahali pa kazi.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Obedi Laiser, jijini Dar es Salaam hivi karibuni, wakati wa maadhimisho ya miaka 10 na mahafali ya 10 ya programu ya Mwanamke Kiongozi, inayoratibiwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE).
“Sisi Absa tuna kitu tunaita ahadi yetu ya chapa inayosema ‘Stori yako ina thamani’, kwa kuendana na ahadi yetu hii tunaamini kwamba story za wanawake wa Tanzania zina thamani na ndio maana tuliamua kuungana na ATE kusapoti jambo ili kama wadhamini , lakini pia tumekua wadau wa karibu sana na ATE kwa miaka 10 tumeweza kuweka wahitimu wengi, leo hii tukiwa na wahitimu kama wanne.
“Sababu kubwa inayotufanya tuendelee kusapoti juhudi hizi ni kwamba kwenye miaka hivi karibuni tumekuwa na mafanikio makubwa sana katika utendaji, wale ambao mnafuatilia nadhani mtakuwa mashahidi na sababu kubwa ya kwanini tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa ni kwa sababu tumekuwa na viongozi wanawake kwenye timu ya uongozi.
“Sisi Absa, tuna idara mbalimbali, tuna idara nne za biashara, kati ya hizo, tatu zinaongozwa na wakurugenzi wanawake, wamepata promosheni hivi karibuni kuingia katika ngazi ya ukurugenzi, hawa ndio wakurugenzi wa biashara, hivyo basi mafanikio ya benki yetu hayawezi kabisa kutenganishwa na uwepo wa viongozi wanawake”, alisema Bw. Laiser.
Mmoja wa wahitimu wa programu hiyo, kutoka Benki ya Absa, Ikunda Kishimbo, ambayo tokea ianzishwe jumla ya washiriki 462 kutoka sekta binafsi na umma wamehitimu alisema, programu hiyo imewajengea washiriki kujiamini na kuwapa uwezo wa kiutendaji katika maeneo yao ya kazi.


