Kahama. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, amezitaka taasisi za fedha nchini, hususan benki, kuwekeza kwa wananchi na wafanyabiashara wadogo wanaohitaji huduma za kibenki ili waweze kukua kiuchumi, badala ya kujikita kwa wafanyabiashara ambao wamefanikiwa.
Biteko, amesema hayo leo, Februari 25, 2025, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, wakati wa uzinduzi wa Benki ya Exim, tawi la Kahama, na kueleza kuwa hali hiyo itawafanya wananchi wote kujivunia uwepo wa huduma za kifedha, hususan benki.
“Wito wangu kwa Benki ya Exim, jaribuni kuwasaidia wananchi wa Kahama ambao wao wenyewe wanahitaji huduma za benki ili waweze kukua kiuchumi. Ni kawaida sana mabenki mengi kujishughulisha na matajiri na kuwaacha maskini.
“Mimi naamini tofauti. Naamini kuwa benki ikimuibua mtu maskini, ikamuwezesha kutoka kwenye umaskini wake na ikamkuza yenyewe, benki hiyo itakuwa imefanya kazi kubwa zaidi, badala ya kusubiri tajiri aliyejitengeneza mwenyewe ili iweze kufanya biashara naye,” amesema.
Amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuhakikisha kuwa Watanzania wanaendelea kupata huduma bora, kuboresha maisha yao na kupunguza umaskini miongoni mwao.
Naye Kamishna wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Dk Charles Mwamwaja, amesema kwa upande wa benki, huduma hizo zimeendelea kuongezeka hapa nchini.
Amesema kuwa mpaka sasa, Tanzania ina jumla ya benki 44, matawi ya benki zaidi ya 1,000, na mawakala wa huduma za kibenki zaidi ya laki moja, na kwamba ubora wa huduma za kibenki umeendelea kuongezeka, hali iliyosaidia kupunguza kiwango cha mikopo chechefu.
Amesema Wizara ya Fedha inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kupambana na changamoto zilizopo, ikiwa ni pamoja na kuendeleza kampeni yake ya kutoa elimu ya fedha mijini na vijijini ili kujenga uelewa kwa watu waweze kuona fursa zilizopo na kuzitumia kwa usahihi.
“Ubora wa huduma za kibenki umeendelea kuongezeka, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa kiwango cha mikopo chechefu. Wizara ya Fedha, kwa kushirikiana na wadau wengine, ina kampeni mahsusi ya kutoa elimu ya fedha katika maeneo yote nchini, ya mijini na vijijini, ili kujenga uelewa na kuwawezesha watu kuona fursa zilizopo na kuzitumia kwa usahihi,” amesema Mwamwaja.