Boma la zahanati lageuka pango la wabakaji

Shinyanga. Wakazi wa kata ya Kizumbi mkoani Shinyanga wamelalamikia kutokamilika kwa jengo la zahanati iliyoanzishwa na wananchi wa eneo hilo, hali iliyosababisha liwe pango la wahalifu.

Jengo hilo ambalo ujenzi wake umesimama kwa takribani miaka 10 limegeuka eneo la kufanyia vitendo vya uhalifu ikiwamo ubakaji na kuhatarisha maisha ya wanawake na wasichana.

Hayo yamebainishwa leo Februari 25, 2025 wakati wa mkutano wa hadhara kwenye kata ya Kizumbi katika ziara ya Mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini, Patrobasi Katambi.

Akizungumza katika mkutano huo  Yunis Ezekiel ameeleza hofu yao kufuatia vitendo vinavyofanyika kwenye jengo hilo.

“Humu ndani kuliwahi kukutwa gauni, viatu na mtandio siku nyingine alikimbia mama mmoja kutoka humo akiwa mtupu, hili limeshakuwa dampo la wabakaji ninaomba mlishughulikie” amesema Yunis.

Mbunge wa jimbo la Shinyanga mijini Patrobas Katambi akisikiliza kero za wananchi wa kata ya Kizumbi iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.

Naye mwenyekiti wa jeshi la jadi, maarufu sungusungu, John Kombe ameeleza hatua walizochukua kudhibiti vitendo hivyo.

 “Tulijaribu kufanya doria  ili kuweka ulinzi eneo hili limeshakuwa kama sehemu ya kufanyia mambo ya kingono ambapo tumebaini matukio kama hayo mawili” amesema Kombe.

Akijibu kero hiyo Mganga Mkuu wa Manispaa ya Shinyanga, Dk Elisha Ndaki ameeleza hali ya ukamilishaji wa maboma ya vituo na zahanati yalivyoanzishwa kwa nguvu ya wananchi ndani ya manispaa hiyo.

 “Tulikuwa na maboma 16 katika manispaa yetu na kati ya hayo sita yamekamilika na tunaendelea na ukamilishaji wa mengine boma la zahanati ya Bugambelele ni miongoni mwa yaliyotengewa fedha katika bajeti ya mwaka huu,” amesema Ndaki.

Akizungumzia hilo Katambi ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu ameahidi kulishughulikia jambo hilo na kuhimiza kuongezwa ulinzi na kuwabaini wanaofanya uhalifu huo.

 “Nimesikia huyu mama akilalamikia matendo ya ubakaji yanayoendelea katika zahanati hii na mimi kama mbunge lazima tufanye kazi katika hili na ninaahidi nitasimamia hadi kukamilika kwake, ili kurudisha heshima ya wananchi,” amesema Katambi.

Related Posts