Dar es Salaam. Benki kuu ya Tanzania (BoT) imesema haijawahi kufanya mazungumzo wala kutoa leseni ya kuruhusu kampuni ya Leo Beneath London (LBL) kufanya shughuli zake nchini kama taarifa za mitandaoni zinavyosema.
BoT imetoa taarifa hiyo wakati tayari watu 38 wamekamatwa na Jeshi la Polisi kutoka maeneo tofauti nchini kwa kujihusisha na kampuni hiyo katika mikoa ya Morogoro, Mbeya, Geita na Dar es Salaam.
Taarifa ya Jeshi la Polisi inasema watu hao walikamatwa kati ya kuanzia Februari 18 hadi 22, mwaka huu akiwemo Mkurugenzi wao, Najim Houmud.
Taarifa kwa umma iliyosainiwa na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba Februari 24, 2025 imeeleza kuwa kwa sasa, hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya maofisa wa kampuni ya LBL.
“Hatua hizi zinachukuliwa kwa maofisa hao kuhusika katika shughuli za udanganyifu, zikiwemo ukusanyaji wa amana na miamala ya kifedha bila kuwa na leseni halali kutoka BoT,” imeeleza taarifa hiyo
BoT ilitumia nafasi hiyo kuwataka Watanzania kuepuka taasisi, kampuni au watu binafsi wanaotoa huduma za kifedha bila leseni kutoka BoT au mamlaka nyingine za udhibiti wa huduma za kifedha.
“Watu binafsi au kampuni zinazotumia jina la BoT kinyume cha sheria kwa manufaa yao binafsi wanapaswa kuacha mara moja, la sivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
“Benki Kuu ya Tanzania inawahimiza wananchi kupata huduma za kifedha kutoka kwa taasisi zilizopewa leseni rasmi, ambazo orodha yake inapatikana kwenye tovuti ya BoT,” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hii inakuja katika kipindi ambacho Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam lietangaza kuwakamata jumla ya watuhumiwa 26 kwa tuhuma za kujihusisha na biashara haramu ya upatu mtandaoni, bila vibali vya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Taarifa ilitolewa na Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Februari 24, 2025, imewataja waliokamatwa kuwa ni Hatibu Kudura (25) mkazi wa Kinondoni, Fatum Hamisi (26) mkazi Kigamboni na Athumani Sadik (29) Mkazi wa Mabibo.
Maeneo waliyokamatiwa kwa mujibu wa jeshi hilo ni Mbagala, Gongolamboto, Tabata, Mbezi Magufuli, Ubungo Riverside na Mabibo.
Hatua ya kukamatwa kwao, ni matokeo ya uchunguzi wa jeshi hilo na BoT, uliobaini kampuni ya LBL haina uongozi maalumu.
“Vilevile ufanyaji kazi wake unahusisha kuwatoza wananchi kuanzia Sh50,000 na kuendelea ili uwe mwanachama, pia huchangisha fedha kwa kuwadanganya wananchi kuwa watapata faida kubwa kwa muda mfupi bila ya wanachama kuhusishwa kwa namna yoyote katika shughuli za uendeshaji wa kampuni hiyo,” imeeleza taarifa hiyo.
Jeshi la polisi, limesema baada ya upelelezi kukamilika watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
“Jeshi la Polisi kanda Maalumu Dar es Salaam linatoa wito kwa wananchi wote kuacha kujihusisha na biashara za upatu mitandaoni bila kujiridhisha kwanza kwa kuwa baadhi ya biashara hizo hazina leseni wala vibali kutoka mamlaka za kisheria zinazohusika hivyo kuhatarisha usalama pesa zao,” imeeleza.