Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, Amani Golugwa leo amefika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kipolisi Kinondoni kufuatia wito wa Polisi uliotolewa kwake na Jeshi hilo jana.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Februari 25, 2025 baada ya kupata taarifa kuwa kiongozi huyo aliitwa Polisi, Golugwa amesema wito umetokana na video fupi iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha akihamasisha kuhusiana na tukio la kichama linalokusudiwa kufanyika Februari 27, mwaka huu.
Golugwa amesema alipokea barua ya wito iliyomtaka kufika kituoni hapo leo saa tano asubuhi bila kukosa.
“Nilipopatiwa barua hiyo na kuangalia muda, nilimpigia Kamanda wa upelelezi wa Mkoa wa Kinondoni, Davis Msangi kumuomba nifike saa saba mchana kwa sababu, muda alionihitaji nisingeweza kufika, kwa sababu nilikuwa na kikao na Balozi wa Norway,” amesema kiongozi huyo.

Amesema baada ya kumaliza kikao na viongozi wengine wa Chadema, waliitikia wito na kufika kituoni Saa Saba mchana na kuonana na Msangi ambaye alihitaji ufafanuzi wa kile walichopanga kukifanya siku hiyo.
Kwa mujibu wa Golugwa, Kamanda Msangi alisikiliza maelezo yao na akaridhika nayo kwa kuwa hamasa hiyo haina nia mbaya bali ni kutoa hamasa kwa wanachama wao kushiriki kampeni za kidijitali ambazo Chadema anakwenda kuzitekeleza.
“Kwa kuwa hatukuwa na jambo baya, tulikaa nusu saa na ilitusaidia pia kufahamiana na kuongea masuala mengine ya kawaida licha ya viongozi wengine walionyesha masikitiko yao kwa kudai kuwa jambo hilo halikuhitaji usumbufu wa kufika kituoni,” amesema Golugwa.
Amesema kimsingi jambo hilo halikupaswa kuchukuliwa kwa ukubwa wa kuandikiana barua na kuitana kituo na badala yake, Jeshi la Polisi lingepiga simu na wangeweza kupata taarifa na maelezo ambayo yangewatosheleza.
Akizungumzia tukio hilo la Februari 27, Golugwa amesma Chadena kitazindua tukio kubwa la kuwaunganisha Wanachama wa Chadema na Watanzania ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu harakati za mabadiliko nchini.
Kituoni hapo Golugwa alisindikizwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa cham hicho, John Heche, Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema na Wakili wa kujitegemea, Hekima Mwasipu.
Mwananchi lilimtafuta kwa simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Mtatiro Kitinkwi ili kupata ufafanuzi zaidi wa tukio hilo, alisema si msemaji bali atafutwe msemaji wa Kanda Maalumu.
Hata hivyo, alipotafutwa Kaimu Kamanda Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Faustine Mafwele amesema hajapata taarifa kuhusiana na wito huo wa kiongozi wa Chadema, hivyo anafuatilia kutoka Kinondoni.