Dar es Salaam. Wengi wanaoitaja Tanzania kuwa ina utajiri wa rasilimali, huorodhesha vitu kama vile, ardhi, vito vya thamani, uoto wa asili na vinginevyo.
Wanachosahau ni kuwa nchi hiyo kubwa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki, ina rasilimali watu wanaokuna vichwa vyao barabara.
Katika orodha hiyo, yumo kijana Noel Sebastian (24) mkazi wa Gongolamboto, Dar es Salaam, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa shahada ya awali katika udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Kilimanjaro Christian Medical Center (KCMC).
Noel amefanikiwa kutengeneza mfumo unaotumia teknolojia ya akili mnemba (AI) anaouita ‘NOBE AI’ unaosaidia watu kupata taarifa mbalimbali.
Mfumo wake anasema una uwezo wa kufanya mjadala juu ya mada mbalimbali ili kumuongezea zaidi uelewa zaidi mtumiaji wake.
Kama haitoshi, kijana huyo anasema mfumo wake unaweza kumsaidia mtu mwenye changamoto ya uoni hafifu au ulemavu wa macho, ukimtahadharisha dhidi ya mazingira hatarishi katika eneo analotembea.
Teknolojia ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence – AI), ni teknolojia mpya ya kompyuta yenye mifumo inayoweza kufanya kazi zinazohitaji akili ya binadamu. Teknolojia hii imeleta mapinduzi makubwa katika sekta mbalimbali duniani.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, Noel amesema amebuni mfumo huo, kutokana na hamu yake ya kutaka kutumia maarifa aliyonayo kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii hasa katika upande wa upatikanaji wa taarifa mbalimbali.
Amesema mwaka 2019 alianza kusoma kwa mazingatio aina mbalimbali za utafiti wa kisayansi, ambazo ziliwahi kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
“Baada ya kuzisoma kadhaa nilibadilisha mawazo na kuhamia katika upande wa teknolojia. Niliwaza kuja na mfumo utakaowasaidia watu kupata taarifa mbalimbali wanazozihitaji ndani ya muda mchache, ”anaeleza.
Ameongeza kuwa alitaka mfumo huo uweze kutumika na watu wote ikiwemo wale wenye ulemavu wa macho au changamoto ya uoni hafifu.
Amesema wakati anawaza hilo, alijaribu kuchunguza mifumo mbalimbali ya Akili Mnemba (AI) ambayo sasa inatumiwa na watu wengi duniani na namna inavyofanya kazi.
“Kuwepo kwa mifumo ya aina hiyo, kulinipa matumaini kuwa ninaweza kufikia ndoto yangu ya kubuni mfumo wa akili mnemba, lakini hofu ilikuwa juu ya gharama ya kulifikia hilo, iilitaka kunikatisha tamaa, ”anaeleza.

Noel akizungumza na mwandishi wa makala haya katika ofisi za Mwananchi zilizopo Tabata jijini Dar es Salaam.
Anaongeza: “Hata hivyo, baada ya kufanya utafiti mwingi na uchunguzi, niligundua teknolojia mbalimbali za gharama nafuu ambazo zinaweza kunisaidia katika kutengeneza teknolojia hiyo.”
Amesema pamoja na kutumia teknolojia hizo zenye gharama nafuu, bado zilimhitaji kulipa gharama nyingine kwa ajili ya kuboresha zaidi mfumo huo aliokuwa akiubuni.
“Baadhi nilikuwa nalipia kati ya Sh10, 000 hadi Sh15,000 kwa saa mbili na majaribio yalitakiwa kufanyika ndani ya miezi miwili, hivyo ilikuwa ngumu kwangu kwa kuwa mimi bado ni mwanafunzi, ”anasema.
Hata hivyo, anasema baba yake alikuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha anamsaidia kulipa gharama hizo ili aweze kufikia ndoto zake.
“Baba hakunikatia tamaa japo safari ilikuwa ngumu, bado hakuniacha alinisaidia kwa kila nilichokihitaji na kunipa moyo kuwa ndoto yangu itakamilika siku moja, ”amesema.
Ilipofika mwaka 2022 anasema mfumo ulianza kufanya kazi kwa kujibu maswali yaliyohitaji taarifa chache pekee bila kutoa ufafanuzi zaidi.
Anasema hilo lilimpa moyo hata alipowaonyesha wazazi wake, walifurahi na kuona kuwa ndoto yake inawezekana kufikiwa.
Hata hivyo, anasema haikuwa hivyo kwa baadhi ya watu wake wa karibu wakiwemo marafiki na wanafunzi wengine, ambao wapo waliodiriki kusema hawezi kufika kokote.
“Baadhi ya watu wangu wa karibu hawakuamini katika uwezo wangu; walinikatisha tamaa na kunicheka na kuona siwezi kufikia ndoto zangu, iliniumiza”
Walisema wenzio wametumia pesa nyingi sana wewe mwenzetu utaweza? Awali ilinikatisha tamaa lakini niliamua kutumia kebehi zao kujipa nguvu zaidi za kuifikia ndoto zangu, ”anasema.
Anasema sasa mfumo huo umekamilika na unafanya kazi rasmi kama ilivyo mifumo mingine inayotumia Akili Mnemba (AI)
Anaeleza kuwa kwa sasa mtu yeyote anaweza kuingia na kuuliza chochote na ndani ya sekunde mbili atakuwa amepata maelezo na ufafanuzi zaidi ya kile alichotaka kukifahamu.
Tofauti yake na mifumo mingine
Amesema teknolojia hiyo aliyoibuni inaweza kumpatia mtu jibu na ufafanuzi wa chochote alichouliza chini ya sekunde mbili.
Anasema kama mtu hajaelewa ufafanuzi uliotolewa, anaweza kuletewa ufafanuzi zaidi kwa njia ya video kuhusiana na kile alichokiuliza.
“Pia unaweza kufanya mdahalo juu ya mada husika ambayo mtu ameuliza ili kumsaidia kupata ufafanuzi zaidi juu ya kile alichokiuliza pamoja na kufanya utambuzi wa hatari katika mazingira yanayotuzunguka, ”anasema.
Anasema japokuwa mfumo huo haujawa rasmi katika majukwaa ya kiteknolojia ya Playstore na Appstore, bado amekuwa akitafutwa na watu mbalimbali kwa ajili ya kuufahamu zaidi mfumo huo na wengine kutaka kufanya kazi naye.
Noel anaomba mamlaka husika kumsaidia kupata hakimiliki ya ubunifu wake ili rasmi uweze kutumika sehemu mbalimbali duniani.
Baba mzazi wa kijana huyo, anasema tangu akiwa kidato cha kwanza alikuwa ni mdadisi wa mambo mbalimbali.
Amesema alikuwa anapenda kuuliza sana maswali kuhusu asili ya vitu mbalimbali na wakati mwingine kuomba simu ili aweze kupata ufafanuzi wa maswali yake katika intaneti.
“Kama mzazi nilijitahidi kuendeleza kile kipawa nilichokiona ndani ya mtoto wangu, nilimlipia kozi mbalimbali za mtandaoni nilijitahidi kumpatia kile anachokihitaji ili kufikia ndoto zake”amesema.
Amesema wakati mwingine alitaka kumkatisha tamaa kwa kuona anatoa fedha nyingi asizoona matunda yake, lakini alijipa matumaini kuwa iko siku mtoto wake atazifikia ndoto zake.
Alipotafutwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na teknolojia (Costech), Dk Amos Nungu, amesema japo tume yake haijapokea ubunifu huo, kijana huyo anakaribishwa kwan kuna dawati maalum ambalo kazi yake kubwa ni kuwasaidia, kuwashauri na kuwaongoza wabunifu wanaochipukia kulingana na mahitaji yao.
“Mahitaji ya wabunifu hawa yanatofautiana kulingana na hatua aliyofika katika ubunifu wake pamoja na malengo aliyojiwekea, “amesema na kutaka mwandishi amtumie mawasiliano ya kijana huyo.