Kiongozi wa upinzani katika utawala wa Israel amemshutumu waziri mkuu wa utawala huo Benjamin Netanyahu kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza na kubadilishana mateka na Hamas baada ya kuchelewesha zoezi la kuwaachia huru Wapalestina wanaoshikiliwa kwenye jela za utawala huo.
Yair Golan, kiongozi wa Chama cha Kidemokrasia cha Israel, ameeleza kwenye mtandao wa X. “Netanyahu ameamuru kucheleweshwa kuachiliwa wafungwa, na hivyo kukiuka waziwazi makubaliano na kuhujumu awamu ya kwanza, kama tulivyoonya”.
Golan ameendelea kubainisha: “Hakuna mazungumzo ya kweli kwa awamu ya pili, ni udanganyifu tu na kutelekezwa maisha ya mateka”.
Golan, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa serikali ya Netanyahu, ameapa kwamba upinzani Israel hautamruhusu waziri mkuu huyo abaki madarakani kama alivyosema kwa gharama ya kaka na dada zetu.
Kiongozi huyo wa upinzani amemwambia Netanyahu: “Nakuambia Bibi, ikiwa utauhujumu mpango huo, milango yote ya moto itakuwa wazi”.
Utawala wa Israel ulitakiwa siku ya Jumamosi uwaachilie Wapalestina 620 unaowashikilia kwenye magereza yake kwa kuachiwa mateka sita wa Israeli waliokuwa wakishikiliwa na Hamas na makundi mengine ya Hamas wa Palestina katika Ukanda wa Gaza, lakini umekaidi kufanya hivyo kwa kisingizio kwamba utaratibu unaotumiwa na Hamas kuwakabidhi mateka wa Israel ni wa kudhalilisha.