Kocha Azam: Simba bahati yao

SARE ya mabao 2-2 bado inaiumiza kichwa Simba ikiona kama inajipa wakati mgumu kuwania ubingwa wa Ligi Buu Bara, lakini kumbe Azam nao wanalia wakiamini Wekundu hao wana bahati na walitaka kuwamaliza kabisa katika mchezo uliopigwa jana, Jumatatu.

Simba ikiwa nyumbani ililazimishwa sare dhidi ya Azam iliyoipunguza kasi kwenye harakati za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha wa Azam, Rachid Taoussi alisema hana raha kutokana na matokeo hayo kwani kwa namna timu yake ilivyocheza mechi hiyo ilistahili kushinda.

Alisema walicheza mechi wakiwa na mpango maalumu wa kuimaliza Simba wakijua Wekundu hao hawana kasi kwenye kuzuia, lakini wachezaji wake wakashindwa kumalizia mashambulizi yao.

Mmorocco huyo ameongeza, kikosi chake kilikosa ubora wa kukamilisha mashambulizi ya haraka kwa kutoa pasi za kumalizia au hata kufunga hatua iliyowaweka kwenye wakati mgumu dhidi ya Simba walipojibu mashambulizi kwa kusawazisha na kufunga bao la pili.

“Unaona aina ya shambulizi tulilofunga bao la kwanza pale, tulifanikiwa. Lakini yapo mengine tuliyatengeneza tukijua Simba haina kasi ya kuja kuzua haraka, lakini shida ikabaki kwetu kwenye kumalizia sawasawa,” alisema.

“Ilikuwa ni mechi tuliyostahili kushinda, lakini sisi wenyewe tukafanya makosa ya kushindwa kumaliza mchezo mapema. Kuna wakati pasi zetu za mwisho hazikufika, pia kuna tulizoshindwa kuweka mpira wavuni.”

Matokeo hayo yameifanya Azam kufikisha pointi 44 na kusalia nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi baada ya michezo 21.

Related Posts