DIRA ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni kuhakikisha inatengeneza mifumo ya kuvutia zaidi ya wanasoka wa kike milioni moja kucheza katika ligi za ngazi mbalimbali hapa nchini.
Ni lengo zuri hasa ukizingatia hatua za maendeleo zilizofikiwa na timu za soka za taifa za wanawake na klabu katika kufuzu na kushiriki michuano mbalimbali ya ngazi ya kimataifa na kitaifa.
Soka la wanawake linakua kwa kasi duniani, huku Shirikisho la Kimataifa la Vyama Vya Soka (Fifa), likiripoti idadi ya wanasoka wa kike kwenye ngazi mbalimbali za mashindano ikiongezeka maradufu katika miongo ya karibuni, ikielezwa hadi kufikia mwaka 2014 kulikuwa na kadirio la wanasoka wa kike milioni 30 kwenye mchezo huo.
Katika msimu wa 2014-2025, zaidi ya wanasoka wa kike 300 wanashiriki kwenye Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (WPL), ikionyesha ni mchezo mwingine unaoibuka kwa kasi kubwa ukiweka kando soka la wanaume.
Sambamba na hilo, hata mvuto wa mashabiki kwenye soka la wanawake umeongezeka kulingana na idadi ya watu wanaojitokeza katika mechi zinazofanyika viwanjani.
Kasi ya kukua kwa soka la wanawake pamoja na ongezeko la mashabiki limevutia kufanya utafiti unaohusu afya za wanasoka wa kike hasa wanaocheza kwenye timu za soka za wanawake za Ligi Kuu Tanzania (WPL).

Tofauti ya kijinsia inapaswa kuzingatiwa zaidi linapokuja suala la usimamizi wa wanasoka wa kike kwa sababu wenyewe wapo kwenye hatari kubwa ya kupata majeraha ukilinganisha na wale wa kiume. Na hilo lipo kibaolojia.
Majeraha mengi yanayosumbua wanasoka wa kike ni yale ya kujiumiza wenyewe na machache yanayohusisha kugongana au kukwatuana uwanjani kwenye mechi au mazoezini. Na maumivu mengi yasiyokuwa ya kugusana yanayosumbua wanasoka wengi wa kike ni ya maumivu ya misuli ya goti, kitaalamu Anterior Cruciate Ligament (ACL). ACL ni tatizo kubwa kwa wanasoka wa kike hapa nchini.
Maumivu ya magoti (ACL) kwa wanasoka wa kike hapa nchini hasa wa timu za WPL yamesababisha timu nyingi kukosa wachezaji wao muhimu kwenye mechi kutokana na kuwa nje ya uwanja muda mrefu, kuingia gharama za kuwatibu huku wengine maumivu hayo yakiwaathiri pakubwa kiasi cha kukaribia kuachana na soka kabisa.
Mchezaji Hadija Petro, ni miongoni mwa wachezaji ambao walilazimika kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti.
Baada ya kudhaniwa kwamba maumivu hayo yamesababisha aachane na soka, Hadija kwa sasa amerejea mazoezini, lakini mwenyewe akifichua bado hajapata matibabu yanayostahili na kwamba anahitajika kufanyiwa upasuaji.
Kwanini magoti ni tatizo kwa wanasoka wa kike?
Magoti ni janga kwa wanasoka wa kike hapa nchini, likiwaathiri wao zaidi kulinganisha na wanaume. Kwenye vikosi vya timu za soka zinazoshiriki WPL kuna idadi kubwa ya wachezaji wenye maumivu ya magoti.
Tofauti iliyopo wapo ambao ACL imeanza kujionyesha bayana na kuwafanya kushindwa kucheza na pia wapo wale ambao wamekuwa wakicheza wakiwa na maumivu ya misuli ya goti na kuathiri ubora wa ndani ya uwanja.

Kuanzia kwenye viatu vya kuchezea, miundombinu ya kufanyia mazoezi, maumbile na lishe vimesukuma kufanya utafiti huu kujua visababishi vikubwa nyuma ya janga hilo kwa wanasoka wengi nchini kusumbuliwa na maumivu ya magoti ili kupunguza au kutokomeza tatizo hilo.
Kumekuwapo na madai kwamba maumbile ya wanawake yanawaweka kwenye nafasi kubwa ya kupata maumivu ya magoti, kwamba nyonga zao pana haziwaweki sawa kimaumbile kuweza kujihusisha na mchezo wa soka vizuri.
Hata hivyo, kwenye utafiti wa kimataifa, mbobezi wa afya ya wanawake upande wa michezo, Dk Emma Ross anasema hakuna ushahidi wa kutosha kwamba maumbile ya wanawake yanaweza kuwa kisababishi kikuu cha kuwafanya kupata majeraha ya magoti kwenye mchezo wa soka, akiondoa fikra kwamba mwili wa mwanamke haukuumbwa kwa ajili ya kucheza mpira wa miguu.
Lakini, kwanini wanasoka wa kike Tanzania wanasumbuliwa zaidi na maumivu ya magoti? Baadhi ya wadau wa mchezo huo wa kada mbalimbali wakiwamo makocha, wachezaji, mafiziotherapia wa klabu, madaktari bingwa wa fiziolojia ya homoni na mazoezi wamezungumza na gazeti hili katika mahojiano mbalimbali.
Dk Samwel Shita anasema: “Kwa kifupi vichochezi vya kike vinawafanya wanawake kuwa na ligament na tendoni zilizo laini na rahisi kunyumbulika. Kiasili ipo hivyo kwa sababu ya uwepo wa homoni zao. Ikumbukwe kuwa maungio yote ya mwili yanaundwa na ligament, tendoni na mifupa. Ligement inaunganisha mfupa na mfupa. Na tendoni ni miishilio au ni mkia wa msuli unaounga msuli na mifupa.
“Sasa ligament na tendoni za kike hazina uimara kama zile za kiume, hii ikiwamo na misuli. Misuli ya kiume ligament na tendoni zipo imara kutokana na homoni za kiume, hiyo ndiyo sababu ya wanaume kuwa na viungo imara tofauti na wanawake. Wanaume wana ustahimilivu mkubwa kuliko wanawake.”
Naye Fredrick Mashili wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) amesema: “Sifahamu sana juu ya utafiti huo, lakini sishangai kuona kuna tofauti kati ya wanaume na wanawake na jambo kubwa ni homoni. Homoni za performance ya nguvu zipo kwa wanaume kuliko wanawake. Wanawake wana misuli dhaifu na ndio maana hata uponaji wao unachukua muda mrefu.
“Kwa wanawake kuna hedhi pia ina mambo yake. Miili yao pia ina viwango vikubwa vya mafuta, kwenye matiti na makalio yote ni mafuta hivyo vyote hivyo vinavyowafanya kuwa na uzito. Kwenye hedhi wanapoteza damu na madini chuma, hivyo ni rahisi kupata majeraha na kuchukua muda mrefu kupona.”

Kocha wa Mashujaa Queens, Morice Abraham aliongeza juu ya hilo: “Magoti na enka ni tatizo kubwa. Wanawake miili yao ina mafuta mengi na hawazingatii sana masuala ya vyakula na matokeo yake wanakuwa na uzito mkubwa unaowafanya kujiweka kwenye urahisi wa kupata majeruhi ya magoti na enka.
“Ukakavu wao upo chini sana, hivyo ni misuli yao ni rahisi kupata matatizo ya maumivu.”
Daktari wa zamani wa Simba Queens, mwanamama Dk Lunina Hasadi anasema: “Magoti na enka ni aina ya majeraha yanayosumbua wachezaji wote wa kike na kiume. Lakini, kwa wanawake tatizo linaonekana kuwa kubwa kwa sababu ya kimaumbile. Kuna kitu tunakiita Q-Angle kitaalamu. Unajua muundo wa nyonga ya mwanamke na homoni zake zinamweka kwenye urahisi mkubwa wa kupata majeraha. Ukiwalinganisha na wanaume hata ukakamavu wao wa misuli ni tofauti. Mchezaji wa kiume anaweza kwenda gym siku chache tu, lakini misuli yake ikakaza, wakati mchezaji wa kike anaweza kwenda gym miezi mitatu, bado mwili wake ukaonekana kuwa vilevile. Kuna wachezaji wengine wa kike hawataki kufanya mazoezi magumu wakihofia kuharibu shepu zao. Hivyo, tatizo kubwa lipo kwenye fitness na Q-Angle.”
Viwanja, viatu ni tatizo?
Mwanasoka anahitaji miundombinu mizuri kwa maana ya viwanja vya kuchezea pamoja na vifaa sahihi kwa maana ya viatu ili kuonyesha kiwango bora uwanjani kwenye mechi atakazopewa nafasi ya kucheza. Kwa wanasoka wa kike, uwanja mzuri na viatu vizuri ni nyenzo muhimu katika kuwafanya kuwa na ubora mkubwa ndani ya uwanja na kuepuka majeraha ya mara kwa mara.
“Kuna kipindi tulikuwa tunafanya mazoezi kwenye uwanja mbovu (mgumu) tulikuwa na matatizo mengi ya magoti na vifundo vya mguu (enka) yaliyowaweka nje ya uwanja kwa muda mrefu wachezaji wetu. Tulisumbuka sana hadi tulipobadilisha uwanja wa mazoezi,” amesema kocha Morice.
Dk Mashili anasema: “Viatu na viwanja ni tatizo kubwa sana, ni mjadala ambao unapaswa kuwa na topic yake ya kujadiliwa kutwa nzima. Kuna kitu kinaitwa kujikinga na majeraha kwenye michezo, hilo linahusu nguo anazovaa mchezaji, viatu anavyovaa, uwanja anaochezea na chakula anachokula. Ni vitu muhimu.
“Unaweza kushangaa kwanini mtu ananunua viatu vya shilingi milioni moja badala ya kununua viatu vya Sh70,000 (Elfu Sabini). Hivyo vitu ni muhimu sana katika kumlinda mchezaji kupata majeraha kama ya magoti na enka ya mara kwa mara.
Fiziotherapia wa timu ya soka ya wanawake ya Alliance Girls ya Mwanza, Mary Gwatenda amesema: “Viwanja wakati mwingine ni sababu pia, unakuta pengine uwanja una vishimoshimo kwa hiyo mchezaji akikanyaga vibaya anapata maumivu kama sio goti basi ni enka. Kingine ni viatu, inaweza kuwa chumu zake zimekwisha au vipo ndefu sana, ukilinganisha na hali ya uwanja, mchezaji anaweza kuanguka, au wakati wa kuruka juu na kutua chini vibaya, anaumia.
Gwatenda anaongeza: “Kama mchezaji kuna aina ya vyakula pia unapaswa kula, kuna ishu ya kulala mapema pia ili mwili upate muda wa kupumzika.”
Fiziotherapia wa Fountain Gate Princess amesema: “Unajua viwanja vyetu havimwagiwi maji, vigumu sana. Halafu unakuta mchezaji amenunua buti zenye njumu ndefu, hapo anaweza akapata maumivu ya enka na magoti. Tunaondoka hapa (Dodoma) tunaenda kule Manyara, nadhani uwanja hautakuwa sababu.”
Kwenye soka la wanawake hapa nchini, shida ya maumivu ya magoti inaonekana kuwa kubwa na kuathiri viwango vya wachezaji na timu kwenye mashindano mbalimbali hasa kwenye michuano ya WPL. Kwa utafiti uliofanya, timu ya Alliance Girls iliripotiwa kuwa na zaidi ya wachezaji watano wenye tatizo la magoti, huku Bunda Queens ikiripoti kuwa na tatizo hilo kwa ukubwa kwenye kikosi chao, sambamba na Mashujaa Queens waliolazimika hadi kubadili uwanja wa mazoezi kuona kama kutakuwa na unafuu wa wachezaji kupata maumivu ya magoti.
Hali kadharika kwenye kikosi cha Fountain Gate Princess hali si nzuri, Mlandizi Queens, Simba Queens, Yanga Princess na hata JKT Queens ambako kumeripotiwa kuwapo na wachezaji kulalamika kusumbuliwa na maumivu ya magoti. Kwenye timu hizo, kuna ambao maumivu yaliyawafanya kulazimika kufanyiwa upasuaji ili kurudi uwanjani, huku wengine wakivaa vifaa tiba maalumu kwa ajili ya kupoza maumivu kwa kurudisha misuli hiyo ya magoti kwenye utimamu.

Kocha wa Mlandizi Queens, Jamila Kasimu anasema: “Matatizo hayo kwenye timu yangu yapo na kuna mchezaji wangu alilazimika kukaa nje kwa muda mrefu kwa maumivu ya goti. Huyu aligongana na mwenzake uwanjani.”
Fizio wa Alliance Girls amesema: “Hawa wadada nipo nao muda wote. Na matatizo yao makubwa kuhusu majeraha yanayowasumbua ni magoti na enka. Kwa timu ya wanawake hapa, kuna wachezaji watano wanasumbuliwa na tatizo la magoti. Kuna mwingine tumemfanyia upasuaji baada ya maumivu kuwa makali sana na kushindwa kucheza huku mwingine tumemvisha kifaa tiba kuona kama atakuwa sawa. Maumivu ya enka pia ni tatizo jingine kubwa.
“Unajua shida ni kwamba majeraha mengi ni ya muda mrefu. Unakuta mchezaji anacheza na maumivu kwa muda mrefu, sasa siku akiitonesha tu ndiyo inaibuka. Ikitokea amekanyaga vibaya au amefanya mazoezi ya viungo vibaya au hata uchovu, basi tatizo linaweza kuibuka.”
Fizio wa Fountain Gate anasema: “Hapa injury siriazi sana ya goti ipo kwa mchezaji mmoja. Wengine ni enka. Lakini, tumegundua pia kuna matatizo ya maumivu ya mgongo. Tumefanya vipimo vya mkojo kujua tatizo hilo la maumivu ya mgongo linaanzia wapi.
“Mimi sina rekodi kubwa sana ya historia ya majeraha ya wachezaji hawa, kwa sababu sina muda mrefu. Sasa nipo hapa kutafuta namna ya kutambua majeraha yanatokea wapi na shida ni nini. Chakula inachangia sana. Unajua hapa Tanzania, mchezaji anakunywa chai ya rangi, haina virutubisho vyovyote.
“Hali ilivyo hapa, mchezaji hawezi kucheza mechi tano mfululizo, tayari ameshaumia na hapo anakaa nje ya uwanja kwa muda mrefu sana. Kingine wakati wa usajili, wachezaji wanachukuliwa tu mtaani hawafanyiwi vipimo. Kwa hivyo, wanakuja wakiwa tayari na majeraha yao baada ya muda mfupi tu, yanaibuka.”
Kocha wa zamani wa Alliance Girls, Ezekiel Chobanka anasema: “Tangu niwepo kwenye timu hii, tatizo la magoti limekuwa kubwa sana kwa hawa mabinti. Kuna binti nilikuwa naye hapa, alisumbuliwa sana na tatizo la goti, anaitwa Aisha Masaka. Badaaye aliondoka hapa kwenda nje kufanyiwa upasuaji. Na hivi karibuni kabla hajaondoka kwenda Brighton, aliniambia licha amefanyiwa upasuaji, lakini bado kuna shida japo anacheza. Shida nadhani migongano imekuwa mingi sana kwa watoto wa kike. Mtoto wa kike akienda anaenda jumla jumla tu, japo tunajaribu kuwafanyisha mazoezi tofauti tofauti angalau kupunguza hilo tatizo.
Kocha Chobanka, ambaye kwa sasa anainoa Ceasiaa Queens ya Iringa anaongeza: “Kuna aina nyingi za majeraha, lakini magoti tu ndiyo naona ni shida, hilo nadhani labda wataalamu watatufanyia utafiti ili tujue ni nini maana sio kwangu tu, hata ukifuatilia kwenye timu nyingine za watoto wa kike tatizo hilo la magoti linawasumbua sana, likifanyika hilo pengine wataalamu watakuja na ufunguzi wa aina ya mazoezi tunayowapatia hawa mabinti zetu.”
Kocha Abraham amesema: “Tuna wachezaji 27 kwa ajili ya msimu huu wa WPL. Lakini, magoti na enka limekuwa tatizo kubwa linalosababisha kuwakosa wachezaji wetu kwa muda mrefu. Kuna kipindi hali ilikuwa mbaya hadi tulipobadilisha uwanjani, walau kidogo imekuwa tofauti. Lakini, suala la kumkosa mchezaji kwa wiki kadhaa kutokana na tatizo la magoti hiyo ni kawaida.”
Kocha wa Yanga Princess, Edna Lema amefichua: “Linaonekana kuwa ni tatizo kwasababu shida ipo kwenye uwekezaji na matibabu sahihi…hata kwa wachezaji wa kiume, tatizo la majeraha ya magoti lipo, lakini huku kwa wanawake linaonekana kuwa kubwa kwa sababu ya matibabu tu.
“Namna anavyotibiwa mchezaji wa kiume ni tofauti kabisa na wa kike. Unakuta mchezaji wa kiume akiumia, hadi klabu inatoa taarifa, lakini huku kwa wanawake, mchezaji ataishia tu kufungwa barafu na kesho unamwona anaendelea na mazoezi.”
Staa huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Twiga Stars anaongeza: “Tatizo linaweza kuanza dogo tu, lakini linaachwa, linachelewa kufanyiwa matibabu sahihi hadi linakuwa kubwa na kumfanya mchezaji kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu. Kutibu goti ni gharama kubwa, lakini hilo halifanyiki kwa wakati na hivyo kumfanya mchezaji kutumia muda mwingi nje ya uwanja.”
Kocha Edna Lema amebainisha kwamba kwenye kikosi chake kulikuwa na mchezaji aliyekuwa na tatizo kubwa la goti, ambaye amefanyiwa upasuaji na sasa amepona na kuendelea na majukumu yake katika kuitumikia miamba hiyo kwenye mchakamchaka wa kusaka ubingwa wa WPL msimu huu.
Kutibu maumivu ya goti hasa kwenye mchezaji aliyepata tatizo la ACL ni gharama kubwa. Kutokana na uchumi wa timu za soka za wanawake ulivyo, kuna baadhi yao zinashindwa kugharimia gharama za kutibu mastaa wake wenye matatizo ya aina hiyo au kuwaweka kwenye mazingira ya kuwaepusha kupata madhara zaidi kwa maana ya kuwatafutia vifaa bora vya michezo na kufanya mazoezi kwenye miundombinu mizuri.
Kutokana na hilo, kuna baadhi ya timu zimewaachia mzigo wa kujitibu wachezaji wenyewe jambo linalokuwa changamoto kubwa kwao kwenye kuhimili gharama za matibabu na hivyo kuwafanya wachezaji hao kushindwa kucheza soka kwa muda mrefu wakisubiri kupata tiba ya kumaliza matatizo yao.
“Kuna kitu kinaitwa kujikinga na majeraha, hii kitu ni gharama kwa sababu itahusisha kiatu gani unavaa, uwanja gani unacheza na chakula gani unakula. Unahitaji kuwa na vifaa vizuri vya kufanyia mazoezi na mechi na uwanja mzuri pia, ili kuepuka kupata majeraha,” anasema Dk Mashili.
Dk Lunina, ambaye pia aliwahi kuwa kwenye idara ya utatibu ya klabu ya Kagera Sugar inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara anaongeza: “Kuna wakati kulikuwa na mchezaji wa timu fulani tofauti na ile niliyokuwa mimi, alipata matatizo ya goti, lakini pesa ya matibabu ilionekana kuwa shida, hadi kwenye kufanya vipimo tu vya MRI ilikuwa tatizo, hana pesa hadi hapo alipokuja kupata msaada kutoka shirikisho la mpira (TFF). Mchezaji alikaa nje kwa muda mrefu sana, sababu ya matibabu tu, gharama zilikuwa kubwa na mchezaji alionekana kuachiwa mwenyewe mzigo wa kujitibu. Kwenye hizi timu za wanawake kuna changamoto kubwa ya kiuchumi.”

Kocha wa Yanga Princess, Edna Lema anaongeza: “Unakuta mchezaji ameumia na matibabu anayopaswa kupatiwa ni upasuaji. Hapatiwi anaachwa tu. Ukweli uwekezaji kwenye hizi timu ni duni sana. Unajua dawa za maumivu ni nyingi, lakini unampatia mchezaji wako dawa gani ya kumtibu akapona? Wachezaji wa kiume na wanawake wote matatizo ya majeraha yanayowakabili ni yaleyale, lakini huko kwa wengine tiba zinafanyika haraka, huku kwa wengine wanaaachwa tu, wanafungwa mabarafu na kesho wanatakiwa kuendelea na mazoezi.”
Daktari wa upasuaji afichua
Baada ya kuwapo na madai ya gharama za matibabu kuwa moja ya vikwazo kwa wanasoka wa kike kupata tiba sahihi kwenye majeraha yanayowasumbua hususani ya magoti, daktari bingwa wa upasuaji (MOI), Dk Kenedy Nchimbi anaweka wazi utaratibu ulivyo na matibabu yanavyokwenda kwa mchezaji anayefanyiwa upasuaji wa goti.
“Kadirio la chini ni miezi tisa hadi 12 kupona ACL,” anasema Dk Nchimbi, ambaye alifichua pia matibabu yake yanategemea na bima ili kugharimia vipandikizi vilivyotumika wakati wa kufanyiwa matibabu ya upasuaji wa eneo lenye maumivu.
Katika kutambua umuhimu mkubwa wa mafunzo yaliyopatikana kwenye utafiti huu, utawasaidia wadau mbalimbali wa soka la wanawake kuhakikisha wanaweka mazingira ambayo yatamkinga mchezo wa kike kupata majeraha ya magoti kirahisi kwa maana ya kuhakikisha anapata viatu vizuri vya soka, anacheza kwenye uwanja uliomwagiwa maji kupunguza ugumu, anapatiwa tiba sahihi, anapata lishe nzuri na kuandaliwa vyema kimwili na kisaikolojia, huku nguvu ikiwekezwa katika kuwawekea bajeti za kutosha za matibabu ikiwamo kuwakatia bima za afya kulingana na urahisi wao kibaolojia katika kupata majeraha kama hayo ya magoti.
Habari hii imeandikwa kwa udhamini wa Taasisi ya Gates Foundation.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp; 0765864917