Kigoma. Mahakama ya Wilaya Kigoma imetengua ushindi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Mtaa wa Gezaulole, Kata ya Gungu, Manispaa ya Kigoma Ujiji, baada ya kujiridhisha haukuwa huru na wa haki, pia kutokana na kuwepo kura bandia.
Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi, Katoki Mwakitalu jana Februari 24, 2025, katika hukumu ya shauri la uchaguzi lililofunguliwa na mwanachama wa (ACT- Wazalendo), Lovi Lovi.
Lovi aliyekuwa mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa mtaa huo wakati wa uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika Novemba 27, 2024 alifungua shauri kupinga mwenendo na matokeo ya uchaguzi huo.
Alifungua shauri hilo dhidi ya aliyetangazwa mshindi wa nafasi hiyo kupitia CCM, Hassan Mashoto kama mjibu maombi wa kwanza, msimamizi msaidizi wa uchaguzi Mtaa wa Gezaulole (ambaye ni mtendaji wa Kata ya Gungu) na msimamizi wa uchaguzi, Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji (ambaye ni mkurugenzi wa manispaa hiyo).
Lovi aliwakilishwa na jopo la mawakili lililoongozwa na Emmanuel Msasa. Wengine ni Eliutha Kivyiro na Prosper Maghaibuni. Upande wa utetezi ulikuwa na mawakili zaidi ya 20.
Katika shauri hilo, Lovi alipinga mwenendo na matokeo akidai mchakato na uchaguzi wenyewe ulikiuka kanuni, sheria na taratibu za uchaguzi akidai uligubikwa na ulaghai kutokana na kuwepo kura bandia, hivyo kuufanya kutokuwa huru na wa haki.
Alidai ukiukwaji huo wa sheria, kanuni na taratibu ulisababisha madhara kwake na kwa wananchi, kwani walinyimwa haki ya kumchagua kiongozi wanayemtaka.
Aliiomba Mahakama itamke kuwa uchaguzi huo ni batili, imuamuru msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa mtaa huo atangaze uchaguzi ndani ya siku saba na ndani ya siku 60 uchaguzi mwingine wa nafasi hiyo uendeshwe.
Walalamikiwa katika majibu yao walipinga na kukanusha madai yote, wa kwanza na wa pili wakimkana Lovi kwamba, hakuwa mgombea na wakieleza uchaguzi ulikuwa huru na wa haki, hakukuwa na kasoro yoyote.
Katika kuthibitisha madai yake aliwaita mashahidi watano, akiwamo yeye na aliyekuwa mgombea wa nafasi hiyo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Walalamikiwa waliwaita mashahidi wanne waliotoa ushahidi kinzani dhidi ya madai na ushahidi wa mlalamikaji.
Katika kuamua shauri hilo kama ulivyo utaratibu, Mahakama kwa pamoja na mawakili wa pande zote iliandaa hoja tano zilizobishaniwa, zilizojumuisha madai yote ya mlalamikaji yaliyohitaji kutolewa ushahidi kuyathibitisha.
Mahakama katika hukumu imejibu hoja hizo kwa kuelezea mada na kuchambua jinsi ilivyothibitishwa.
Hoja iwapo mchakato na uchaguzi ulikiuka sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi, Lovi amedai haukuwa huru na wa haki kwa kukiuka taratibu za uchaguzi, kwa mawakala kutokupewa daftati la wapigakura ili kuwahakiki.
Amedai katika kituo C cha kupigia kura kuna watu walipiga zaidi ya kura moja na kituo E, mtu aitwaye Ucheke alikamatwa na kura bandia zikiwa zimepigwa kwa CCM.
Amedai hali hiyo ilisababisha vurugu, yeye na wakala wake walitolewa nje na kituo kikafungwa kwa muda, hivyo baadhi ya wananchi kuondoka bila kupiga kura.
“Wajibu maombi walipinga hoja hizo zote. Nimechambua ushahidi wa pande zote mbili, mwombaji ameweza kuthibitisha madai yake bila kuacha shaka kwa mujibu wa kesi za uchaguzi,” alisema hakimu Mwakitalu.
Amesema ni msimamo wa kisheria kwamba, kila shahidi anastahili kuaminiwa na ushahidi wake kukubaliwa labda kama kuna sababu za msingi kufanya asiaminiwe.
Hakimu amesema hana sababu za kutoamini madai ya mwombaji kwamba kulikuwa na ulaghai, kwani ushahidi wake uliungwa mkono vilivyo na aliyekuwa wakala wake aliyemkamata Ucheke akiingiza kura bandia.
Amesema wakala wa mlalamikaji alimuona mmoja wa wasimamizi wa kituo akichukua kura mfukoni na kuzichanganya na zile walizokuwa wakizihesabu, hivyo kusababisha vurugu zilizofanya uchaguzi kusimama.
Hakimu amesema ushahidi huo uliungwa mkono na shahidi wa tano, mpigakura aliyeeleza upigaji kura ulisimama kutokana na vurugu baada ya mtu kukamatwa na kura bandia na yeye hakuweza kupiga kura.
Mwakitalu amesema shahidi wa tatu, aliyekuwa wakala wa Chadema katika kituo C alisikia vurugu kituo B ambako wakala wa Chadema alitolewa nje.
Amesema ushahidi huo uliungwa mkono na shahidi wa nne, aliyekuwa mgombea wa Chadema aliyethibitisha kuwa wakala wake katika kituo B, Irene Polito alitolewa nje.
“Sijaona sababu za kutilia shaka ushahidi wao na wala sijaona kupishana ambako kungeifanya Mahakama kuutilia shaka. Hivyo, utetezi wa wajibu maombi hautoshi kuibua mashaka dhidi ya ushahidi wa mwombaji,” amesema.
Hakimu Mwakitalu amesema: “Kwa hiyo, nakubali hoja ya pili kwamba mchakato wa uchaguzi na uchaguzi Mtaa wa Gezaulole ulikiuka kanuni za uchaguzi. Na kwa wasimamizi kuongeza kura katika masanduku ya kura unathibitisha kuwepo ulaghai ambao umelalamikiwa na mwombaji.”
Hakimu amesema huo ni uvunjifu wa kanuni nyingi na maadili ya uchaguzi ambazo zinaufanya uchaguzi huo usiwe wa haki.
Amebainisha kuwa wamevunja Kanuni ya 48(1), (b), (i ), (j ) na (l) ya Kanuni ya Uchaguzi huo, Tangazo la Serikali GN 574 zinazobainisha makosa yasiyoruhusiwa, likiwamo mtu kupiga kura zaidi ya moja kwa mgombea mmoja.
Hakimu amebainisha wasimamizi wa vituo C na B walikiuka kanuni ya 4 ya Kanuni za Maadili ya Uchaguzi inayowataka wasimamizi na wasaidizi wa uchaguzi kuendesha uchaguzi kwa misingi ya uhuru na haki kwa kuzingatia Katiba na sheria.
Mwakitalu amesisitiza wasimamizi hao wana wajibu wa kukemea vitendo vinavyoweza kuharibu uchaguzi na kwamba, wamevunja kanuni ya 4.2 ya Kanuni za Maadili kuhusu mambo wasiyotakiwa kama vile kukipendelea chama au mgombea yeyote.
Hivyo amesema mjibu maombi wa kwanza na wasimamizi wa vituo wamekiuka kanuni za uchaguzi na kuufanya kutokuwa huru na wa haki.
Kuhusu hoja kama kulikuwa na tofauti ya kura na kama iliathiri matokeo ya uchaguzi huo, hakimu amesema baada ya kufanya uchambuzi wa ushahidi wa pande zote amekubaliana nazo.
“Ukiukwaji huo umechafua matokeo ya mwisho yaliyotangazwa na kubandikwa. Hivyo naona ukweli katika madai na ushahidi wa mwombaji kuwa baada ya kuhesabu kura matokeo yalionyesha amepata kura 303 lakini baada ya majumuisho yaliyobandikwa yakaonekana ana kura 221 tu vituo vyote vine,” amesema.
Hakimu amesema hali hiyo inaonyesha matokeo yaliyotangazwa na kubandikwa hayakuwa halali yaliyotokana na kuhesabu kura kutoka katika vituo.
Amesema hakuna ushahidi wa nyaraka kuthibitisha mlalamikaji alipata kura hizo baada ya fomu ya matokeo ya kituo B kuonyesha mlalamikaji alipata kura 303 kukataliwa kwa sababu za kiufundi, isipokuwa ushahidi wa mdomo pekee.
Amesema ni msimamo wa kisheria akirejea moja ya kesi zilozowahi kuamuliwa na Mahakama ya Rufani, kuwa ushahidi wa mdomo hauwezi kuonekana dhaifu kwa sababu tu ushahidi wa nyaraka uliotakiwa kuambatanishwa haukutolewa.
Hakimu akizungumzia hoja kuhusu nafuu ambazo wadaawa wanastahili, amesema kutokana na ukiukwaji wa kanuni ni wazi wananchi wa Gezaulole walinyimwa haki ya kumchagua kiongozi wanayemtaka kutokana na udanganyifu wa wasimamizi.
“Mahakama hii inatamka kuwa mchakato na uchaguzi wa mwenyekiti Mtaa wa Gezaulole uliofanyika tarehe 27, mwezi wa 11, wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vitongoji na Vijiji ni batili.
“Ushindi wa mjibu maombi wa pili (Mashoto wa CCM), unabatilishwa na wajibu maombi wanaamuriwa kumlipa gharama mwombaji,” amesema.