Majeraha yamtibulia Yacouba Songne | Mwanaspoti

MSHAMBULIAJI nyota wa Tabora United, Yacouba Sogne huenda akakosa mechi zilizosalia za Ligi Kuu Bara kutokana na kusumbuliwa na majeraha yaliyomuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu, kwani hivi sasa yupo Morocco kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.

Yacouba aliyetua Tabora msimu huu akitokea AS Arta Solar ya Djibouti, ni wazi kuwa hajaanza kazi vizuri msimu huu.

Nyota huyo wa zamani wa Yanga, mara ya mwisho kuonekana uwanjani akikipiga ilikuwa ni katika pambano la Ligi Kuu dhidi ya KMC, Novemba 29, mwaka jana, kwenye Uwanja wa KMC Complex, ambapo walitoka na ushindi wa mabao 2-0, huku akiitanguliza kwa bao la kipindi cha kwanza.

Baada ya hapo alikaa benchi kutokana na tatizo la majeraha, jambo lililomfanya kukosa mechi nane hadi sasa.

Hii sio mara ya kwanza kwake kumaliza msimu akiwa nje, jambo lililowahi kutokea alipokuwa Yanga baada ya kupata majeraha ya goti na kukosa msimu mzima. Ndani ya mechi 14 alizocheza Yacouba akiwa Tabora amefunga mabao manne, huku kikosi hicho kikiweka rekodi ya kushika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu na kucheza michezo 21.

Baada ya kupata majeraha, Yacouba alirudi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu yaliyochukua takriban miezi mitatu. Wakati alishaanza kupona na kuanza mazoezi kwa bahati mbaya akatonesha tena jeraha la goti na vipimo vikaonyesha ili awe fiti ni vyema akafanyiwa upasuaji wa ‘ligament’.

Ndipo alipoanza safari ya kwenda Morocco wikiendi iliyopita kwa ajili ya matibabu ya upasuaji huo utakaofanywa na daktari bingwa wa matatizo hayo.

Akizungumza na Mwanaspoti baada ya kufika Morocco, Yacouba alisema yupo tayari kwa matibabu kwani vipimo vimeshafanyika.

“Nimeshafika Morocco nimefanya vipimo nasubiri kupewa tarehe ya upasuaji ambayo nadhani itatoka wakati wowote kuanzia kesho,” alisema.

Tabora United imebakiza mechi tisa kumaliza msimu, hivyo huenda Yacouba akamaliza akiwa nje, kwani awali alishakaa miezi mitatu. Rekodi ya majeraha kumuweka nje ilimng’oa Yanga kutokana kushindwa kuitumikia akijiuguza na kisha kusajiliwa katika dirisha dogo na Ihefu (sasa Singida Black Stars) misimu miwili iliyopita alikoifungia mabao matatu kabla ya kuondoka kwenda Djibouti na kuifungia mabao saba zikiwamo hat trick mbili msimu wa 2023-2024 ambapo timu hiyo ilibeba ubingwa wa nchi hiyo.

Related Posts