Mashabiki wataja kete ya ubingwa Bara

WAKATI mashabiki wa Yanga wakichekelea matokeo ya sare waliyoipata watani zao, Simba dhidi ya Azam, mashabiki wa Wekundu wamesema suala la ubingwa bado wakitaja michezo ya kuamua hatima ya taji msimu huu.

Jana Simba ikiwa wenyeji wa Azam waliambulia sare ya mabao 2-2 na kufanya Yanga kuendelea kubaki kileleni kwa pointi 55 licha ya kutangulia mechi moja mbele kwenye msimamo.

Hata hivyo, licha ya Simba kuwa na mechi moja mkononi, iwapo itashinda itabaki nafasi ya pili ikizidiwa alama moja dhidi ya Yanga na kuendelea kuwa na matumaini huko mbeleni.

Shaban Musa, shabiki wa Simba jijini Mbeya, amesema pamoja na matokeo ya sare ya jana, lakini Yanga wasijiamini sana wala kutamba kubeba ubingwa kwani bado wana mlima mrefu.

“Naweza kusema ubingwa bado, hawajakutana na sisi Machi 8, wana mzigo dhidi ya Azam na Tabora United. Kama watatoboa hapo basi ubingwa utaenda tena Jangwani,” amesema Mussa.

Naye mchambuzi na mchezaji wa zamani wa Tukuyu Stars na Coastal Union, Charles Makwaza amesema ni mapema sana kutabiri ubingwa kwani kuna mechi zitakazoamua baina ya Simba na Yanga.

“Yanga ana mechi na Azam, Simba na Tabora United, Simba ana safari ya Coastal Union na Yanga, sasa hizi mechi ndizo zinaweza kuamua hatma ya miamba hawa msimu huu,” amesema beki huyo wa zamani.

Shabiki wa Yanga, Benson John amesema timu zilizopata ushindi kwa bingwa huyo mtetezi kwa sasa zisitarajie mteremko kwani sare ya Simba mbele ya Azam imewarahisishia kazi.

“Simba alisakwa sana sasa amepatikana, tutamfunga tena Machi 8 na ndiye atatuonesha rasmi njia ya ubingwa wa mara nne mfululizo, wale Tabora, Azam na Pamba ni mteremko kwetu,” amesema shabiki huyo.

Yanga imepoteza mechi mbili dhidi ya Azam 0-1 na Tabora United 1-3 na sare dhidi ya JKT, huku Simba ikipoteza mbele ya Yanga 0-1 na sare tatu mbele ya Coastal Union 2-2, Fountain Gate 1-1 na Azam 2-2.

Related Posts