Mchome atoa saa 48 Chadema, amtaja Lissu na Mnyika

Arusha. Sakata la barua ya malalamiko kuhusu uteuzi wa viongozi ulioufanywa na Tundu Lissu wa watendaji wa juu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wajumbe wa kamati kuu limeendelea kuibua mjadala, baada ya muhusika kuibuka akitaka malalamiko yake yajibiwe na si vinginevyo.

Barua hiyo ni ya kada wake, Lembrus Mchome, aliyoiandika kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chadema na nakala kuituma Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa akipinga uteuzi wa viongozi hao uliofanywa na Lissu, Januari 22, 2025, akidai umekiuka katiba ya chama hicho.

Mchome, ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro, katika barua hiyo amesema uteuzi wa vigogo hao uliidhinishwa bila akidi ya kikao cha baraza kuu kutimia.

Kwa mujibu wa Mchome, viongozi waliopatikana katika utaratibu huo ni pamoja na Katibu Mkuu, John Mnyika, Aman Golugwa (Naibu Katibu Mkuu – Bara) na Ally Ibrahim Juma (Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar).

Katika barua hiyo, Mchome amesema wajumbe wa kamati kuu walioteuliwa na kuidhinishwa na kikao hicho ni Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh na Dk Rugemeleza Nshala, akidai uteuzi wao ni batili.

Tangu Februari 18, 2025, Mchome alipowasilisha barua hiyo yeye mwenyewe makao makuu ya Chadema, Mikocheni jijini Dar es Salaam na kuituma ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, kumekuwa na mijadala mikali ndani na nje ya chama hicho.

Mchome amedai ili akidi ya kikao hicho chini ya uenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kilichowaidhinisha vigogo hao ikamilike, kilipaswa kuwa na wajumbe 309, badala ya 85 waliokuwepo ambao ni sawa asilimia 20.6.

Jumapili ya Februari 21, 2025, Lissu alizungumzia hilo akisema Mchome hana hoja yoyote ya msingi kwani akidi ya Baraza Kuu ilitimia na atajibiwa barua yake na Katibu Mkuu, John Mnyika.

Hata hivyo, Mnyika alitumia ukurasa wake wa kijamii wa X kutoa ufafanuzi wa barua ya Mchome ambaye naye alisisitiza hakuna ukiukwaji wowote wa katiba.

Februari 20, 2025, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Aman Golugwa alipoulizwa na Mwananchi kipi kinaendelea juu ya barua hiyo alisema:-

“Ni barua ambayo haina mambo magumu. Ni barua itakayojibiwa kwa page (kurasa) moja tu, itakuwa imejitosheleza. Itakavyofanyiwa kazi, atajibiwa muhusika aliyeandika. Utaratibu wa kiutawala, barua itakwenda kwa muhusika.”

Leo Jumanne, Februari 25, 2025, Mchome ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu amekutana na waandishi wa habari jijini Arusha kuzungumzia suala hilo la barua yake akishikilia msimamo wake wa kutaka majibu ya kupinga uteuzi wa viongozi hao.

Mchome amesema katika barua hiyo yenye kumbukumbu namba KM/CDM/AD/2025 ilitaka ufafanuzi wa uhalali wa viongozi hao kupitishwa na akidi ndogo ya wajumbe.

Kwa mujibu wa Mchome, akidi ya wajumbe ni wanachama 412 ambayo akidi inayotakiwa angalau iwe na wajumbe 309 sawa na asilimia 75 lakini viongozi hao walipitishwa na akidi ya wanachama 85 tu sawa na asilimia 20.6.

“Kutokana na idadi hiyo ndogo ya wajumbe, baraza hilo halikupaswa kufanyika lakini tunashangaa imefanyika kinyume na taratibu, sheria na kanuni za chama, hii inamaanisha watu hao sio sahihi kuhudumu kisheria,” amesema.

Katika kusisitiza hilo, Mchome amesema, “sasa basi baada ya kuandika barua kwa mujibu wa katiba yetu na makubaliano makubwa na mwenyekiti wetu kuwa mwanachama yoyote mwenye hoja asikimbilie kwenye mitandao awasilishe kwenye chama.

“Nashangaa mimi barua yangu sijajibiwa badala yake John Mnyika ameenda kutoa ufafanuzi kwenye mitandao ya kijamii, huku Makamu Mwenyekiti naye akifanya hivyohivyo akifuatiwa na Mwenyekiti wetu Tundu Lissu anayeongelea kwenye vyombo vya habari.”

Mchome amesema hatua hizo zilizofanywa na viongozi hao ni ukiukwaji mkubwa wa taratibu na sheria za chama na bado hajachukua majibu hayo kama rasmi, hivyo kutoa siku mbili barua yake ijibiwe.

“Tangu nimeandika barua imepita wiki nzima sijajibiwa kimaandishi kwa mujibu wa taratibu za chama, zaidi naona mijadala tu kwenye mitandao ya kijamii, hivyo sasa nitoe siku mbili (sawa na saa 48) kwa Katibu Mkuu anijibu barua yangu ili kama sijaridhika nifuate hatua ya juu na kama pia asipojibu ndani ya hizi siku mbili nitajua hatua ya kufuata kwani hapo sio mwisho,” amesema.

Mchome amesema, siku hizo mbili ni kuanzia leo na kesho Jumatano, “ikifika kesho jioni sijapata majibu sasa nitajua uelekeo.”

Hata hivyo, Mwananchi limewatafuta Golungwa saa 12 jioni ambapo amesema: “Sijaona hicho alichokiongea na sijasikia kwa hilo alilozungumza.”

“Barua yake iko tayari na katibu mkuu alimjulisha kuwa iko ofisini anaweza kuipata. Kwa hiyo majibu mbalimbali mnayosikia ni waandishi kuuliza na sisi tunajibu. Barua ipo atajibiwa na kutoa saa 48 kimsingi hawezi kukitisha chama, alihitaji ufafanuzi,” amesema.

Baada ya majibu hayo ya Golungwa, Mwananchi likamtafuta tena Mchome kujua taarifa kuwa amepewa akachukua majibu yake ambapo amesema, “hakuna taarifa yoyote ambayo nimepewa.”

Zaidi mwanachama huyo ameonyesha nia ya kuchukua hatua za kisheria kwa baadhi ya watu waliojitokeza na kuvuruga mkutano wake na waandishi wa habari leo jijini Arusha.

Hali hiyo imejitokeza baada ya watu walioshindwa kutambulika kwa haraka kujitokeza ndani ya ukumbi wa mkutano na waandishi wa habari saa sita mchana na kuanza kufukuza watu katika eneo hilo kabla ya baadaye kuhamia eneo lingine.

Mmoja wa watu hao, Mchome amesema kuwa amemtambua kuwa ni mlinzi wa karibu wa kiongozi wa juu wa chama hicho.

“Siamini kama tumefikia hatua ya kuwindana hivi na nyie wenyewe waandishi mmeona jinsi tumevamiwa na vijana wale akiwemo mlinzi wa karibu wa (tumeficha jina kwa sababu tumeshindwa kuthibitisha), siwezi kusema wametumwa na nani lakini hili sitalifumbia macho bali nitachukua hatua za kisheria dhidi ya tukio hilo na vitisho ninavyovipata kwa ajili ya usalama wa maisha yangu,” amesema Mchome.

Februari 19, 2025 Mwananchi lilimtafuta Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza kujua kinachoendelea ambapo alisema kuwa barua ya Mchome imeshafika katika ofisi hiyo, wanasubiri kwanza ifanyiwe kazi ndani ya Chadema.

“Kwa sababu barua imeandikwa kwa katibu mkuu, tunasubiri ifanyiwe kazi kwanza ndani ya chama, lakini tumeiona ina malalamiko ya msingi sana. Kwa utaratibu uliopo wasiporidhika anakuja kwetu kwa kuwa sisi tunasimamia katiba na sheria za vyama.”

“Tunasubiri, lakini ukiyasoma unaona mantiki yake, ila huo ni upande mmoja, lazima tusikilize na upande wa pili,”alisema.

Kwa mujibu wa Nyahoza, kama mlalamikaji (Mchome) hataridhika na majibu atakayopewa atawasilisha malalamiko yake katika ofisi ya msajili kwa sababu mambo ya katiba hayaishii ndani ya chama.

Lissu amesema anajua anachokifanya kada huyo ni kuwapotezea muda au hajui vizuri Katiba ya chama hicho, kwani wana orodha yote ya wajumbe wa Baraza Kuu lililokutana Januari 22, 2025 katika ukumbi wa Mlimani City.

Lissu alishinda kwa kura 513, ambazo ni asilimia 51.5, huku Mbowe akipata kura 482, sawa na asilimia 48.3. Charles Odero alishindwa na kura moja.

Katika maelezo yake, Lissu amesema,  “Moja ya swali ambalo mnapaswa kumuuliza (Mchome) alikuwepo? Alikuwepo siku hiyo, yeye si ni mjumbe wa Baraza kuu je, alikuwa wapi? Kama hakuwepo sasa alijuaje kuwa akidi haikutimia?”

Lissu ambaye kitaaluma ni mwanasheria amesema Mchome anaruhusiwa kupeleka hoja yake kokote, lakini chama hicho kitaenda kumjibu kwani wanachojua ni kwamba anataka kuwapotezea muda.

 “Mchome kwanza hakuwepo kwenye kikao, nataka kumwambia akidi ilitimia, kama wajumbe ni 412 akidi ya kiwango hicho ni 206, lakini walioorodhesha majina yao walikuwa 234 unasemaje walikuwa 85 unawatoa wapi, kwa hiyo atajibiwa akienda kwa msajili tutamfuata huko huko tutaenda kumwambia unasikiliza maneno ya watu ambao wanaokoteza okoteza mambo,” amesema.

Related Posts