Aidha alisema kuwa lengo la Chama hicho kuendelea kushika dola sio kwenda kucheza rede bali ni kuendelea kutatua shida na changamoto za wananchi.
Mjumbe huyo wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (Nec) alitoa kauli hiyo jana wakati wa uzinduzi wa kambi ya Vijana wa ccm mkoa wa Kilimanjaro wapatao zaidi ya 700 inayofanyika wilayani Hai.
Alisema kuwa, hakuna Chama cha siasa kinachoweza kutatua matatizo ya Wananchi katika Taifa hili zaidi ya Chama cha Mapinduzi na kuwataka wananchi kutodanganyika na watu wenye nia hovu na Taifa.
“Vijana mnapaswa kutambua kuwa CCM sio Chama ambacho kinatafuta dola ili kwenda kucheza rede bali ni kuendelea kutatua matatizo ya wananchi na ndio maana mmeshuhudia fedha nyingi zimetolewa na serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo” Alisema Mwakitinya.
Aliwataka Vijana kusimamia maadili na kuchunga njia zao kama vijana wa CCM ili kuendelea kuwavutia vijana walio nje ya Chama kujiunga na Chama hicho.
Alisema kuwa, CCM kinamisingi ya Umoja na mshikamano na kuwataka kutokuruhusu kutengana kwani itaruhusu kuingiliwa na maadui na kuruhusu Chama kushindwa katika chaguzi mbalimbali.
“Ili Chama kiendelee kuwa imara ni lazima kushikamana hivyo vijana mnawajibu wa kutambua kuwa Chama kinawahitaji katika kuhakikisha wagombea wake wanashinda hivyo tuendelee kuilinda na kuitunza imani hiyo tuliyopewa na Chama chetu” Alisema Mwakitinya.
Akitoa taarifa ya kambi hiyo, Katibu wa UVCCM mkoa Kilimanjaro, Ahmady Kibamba alisema kuwa, vijana wameamua kujinoa, kujiivisha na kujiimarisha ili kuweza kuhakikisha CCM inapata ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu.
Kibamba alisema kuwa, kambi hiyo itaanza Februari 25 mwaka huu hadi Machi 2 ambapo vijana zaidi ya 700 kutoka wilaya saba za mkoa wa Kilimanjaro wameshiriki katika kambi hiyo.
Kwa upande wake, Mbunge wa viti maalum kupitia Vijana, Asia Halamga alisema kuwa, kijana aliyepo ndani ya Chama cha Mapinduzi anakuwa katika njia sahihi na kuwataka vijana kuendelea kujiunga na Chama hicho.