Polisi yataja sababu kumshikilia kiongozi wa walimu wasio na ajira

Geita. Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limekiri kumshikilia mwalimu Joseph Paul (31) ambaye ni mwenyekiti wa umoja wa walimu wasiokua na ajira Tanzania (Neto), likieleza kuwa  uchunguzi umebaini umoja huo hauna usajili kutoka mamlaka za kisheria.

Katika taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita,  Safia Jongo imeeleza mwalimu huyo alikamatwa Februari 24,2025 kwa mahojiano na  tayari ameachiwa kwa dhamana.

Kamanda Safia amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi na taarifa kamili itatolewa mara baada ya uchunguzi kukamilishwa na hatua za kisheria zitakazochukuliwa.

Safia amewataka wananchi kuzingatia sheria na kujiepusha na makundi ya kihalifu kwa kuwa jeshi hilo halitamvumilia yeyote atakayebainika kuhusika katika vitendo vya kihalifu au kuhamasisha uvunjifu wa amani.

Barnabas Daud ambaye ni kaka wa mwalimu huyo amesema mdogo wake alimueleza kuwa anafuatiliwa na alipomuuliza anafuatiliwa na nani hakusema, lakini alimuacha dukani akiuza na aliporudi hakumkuta.

Amedai akiwa dukani baada ya muda mfupi gari dogo ilifika nje ya duka na kumuita mkewe na baada ya muda alirudi dukani na yeye aliitwa na kuwataka wamfuate dukani, lakini walizidi kumuita na alipowafuata alimuona ndugu yake kwenye gari akiwa amefungwa pingu na alipouliza kosa lake hakuelezwa bali aliambiwa wanampeleka kwa RCO

“Walimkamata kwenye saa nane inaenda kwenye saa tisa nilifika polisi sikumuona na namba niliyopewa ikawa haipatikani nikaenda vituo vyote vya polisi sikumuona ile namba niliyopewa nikaitumia ujumbe kuomba anipigie ndio akanipigia nikamwambia nimefika kituoni simuoni ndugu yangu akaniambia anahojiwa kwa RCO”

Amesema saa mbili usiku alipata taarifa yupo kituo cha polisi na aliruhusiwa kupewa chakula lakini kama familia hawakuweza kuzungumza naye kwa kuwa alikua chini ya uangalizi wa askari.

Alipoulizwa kuhusu mwonekano wake amesema yuko kwenye hali ya kawaida na hana jeraha lolote linaloonekana.

Mwandishi alipotaka kujua hali ya ndugu yake ameeleza alipomuona hakuwa na jeraha lolote na hawezi kusema kama amepigwa ama la.

Related Posts