Rais Samia aahidi ujenzi shule za sayansi za wavulana

Kilindi. Baada ya kukamilisha ujenzi wa shule za sekondari za sayansi za wasichana, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameahidi kuanza ujenzi wa shule hizo kwa upande wa wavulana.

Kauli hiyo ya Rais Samia inakuja, ikiwa tayari katika mikoa yote 26 shule hizo za wasichana zimejengwa kwa gharama ya Sh116 bilioni.

Rais Samia ameeleza hayo leo Jumanne, Februari 25, 2025 katika mkutano wa hadhara muda mfupi baada ya kufungua shule maalumu ya sayansi ya wasichana ya Tanga, iliyopo wilayani Kilindi katika mwendelezo ya ziara yake iliyoingia siku ya tatu mkoani hapa.

“Tutakapomaliza mzigo huu tutaelekea kwa wavulana, ingawa wavulana wanafaidika sana kwenye Veta (Vyuo vya Ufundi Stadi nchini) na shule za amali na wasichana wanakuwepo, lakini kwenye masomo ya sayansi wavulana wanawatangulia.

“Ndiyo maana tumeweka shule hizi maalumu kwa wasichana ili wajisikie kwamba wana haki ya kusoma masomo ya sayansi,” amesema kiongozi huyo mkuu wa nchi.

Katika ukaguzi wake wa shule hiyo, Rais Samia ameelezea kufurahishwa na uwepo wa darasa la Tehama (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano) akisema ndiko ulimwengu unajielekeza hivyo ni vyema wanafunzi hao wakaipata elimu hiyo mapema.

Akumbuka Beatrice Shellukindo

Katika hotuba yake, Rais Samia alipendekeza shule hiyo kuitwa Beatrice Shellukindo ambaye ni mbunge wa zamani wa Kilindi aliyefariki dunia mwaka 2016 jijini Arusha akisumbuliwa na maradhi ya mgongo na miguu.

“Ndugu zangu nina ombi kwenu, naomba mkubali shule hii iitwe Beatrice Shellukindo, nilikuwa nanong’ona na Mkuu wa Mkoa (Dk Baltrida Burian) hapa, nikamuuliza mmeipa jina gani? Akasema inaitwa tu shule ya wasichana sekondari bado haina jina.

“Lakini Kilindi hapa tulikuwa na mpambanaji mzuri sana aliyekuwa mbunge wenu na alikuwa mpambanaji wa masuala ya wanawake, na alifariki akiwa bado mbunge akiendelea kupambania maendeleo ya jimbo hili,  najua leo angekuwepo angesikia furaha sana, nikuombe mkuu wa mkoa ikikupendeza mnaweza mkaipa shule hii jina lake,” amesema Rais Samia.

Shellukindo alikuwa ni mmoja wabunge hodari wa kupambania haki za wanawake, lakini pia aliwahi kuwa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala). Pia Shellukindo aliwahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kupitia wilaya ya Kilindi.

Majibu ya changamoto za shule

Rais Samia amesema katika risala ya wanafunzi wa shule hiyo, ameelezwa uwepo wa changamoto ya usafiri hasa kwa wanafunzi kwenda na kurudi mjini pale inapohitajika, sambamba na maombi ya jenereta ili kupata umeme wa uhakika.

“Mambo haya mawili niachieni mimi, ofisi yangu itashughulika na hayo ya usafiri na jenereta. Masuala ya maji shule waziri ameninong’oneza tayari ameunganisha, lakini kuna mradi mwingine unaolekezwa huku utakaounganishwa ili kuwa na uhakika wa maji,” amesema.

Amtaka Ndejembi kupeleka kliniki Kilindi

Mwishoni wa hotuba yake Rais Samia amesema anafahamu kwamba Kilindi kuna migogoro ya ardhi, ikiwemo viongozi hivyo amemuagiza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi kuishughulikia.

“Namtaka ashughulikie na migogoro iondoke kabisa ndugu zangu tuishi bila migogoro kama wote tutasaidiana. Migogoro mingine inachangiwa na viongozi katika maeneo husika,” amesema Samia huku akishangiliwa na wananchi.

“Kwa kushangiliwa huku ina maana Kilindi na kwenyewe kuna mchango wa viongozi kwenye migogoro katika maeneo husika. Nimuagize waziri wa ardhi, zile kliniki zako sogea Kilindi pigeni kambi hapa, sikilizeni pande zote ili tupate mwafaka na watu waishi kwa amani,” amesema Rais Samia.

Awali, Mbunge wa Kilindi, Omary Kigua amezungumzia barabara ya kutoka Handeni- Kilindi hadi Kiteto akisema ni muhimu inayounganisha mikoa minne kwa uchumi hasa kwa kutumia bandari ya Tanga ambayo Serikali imewekeza fedha nyingi, ili wananchi mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro kupitisha mizigo.

“Mizigo inayokwenda Uganda, DRC (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) na Burundi kwa bandari ya Tanga ni muhimu sana. Upo umuhimu wa barabara hii kujengwa.”

“Nimezungumza na comrade Waziri wa Ujenzi (Abdallah Ulega) ameniambia jana imeingia Sh2.7 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo, hivyo tunamuomba mkandarasi aingie kazini ili iweze kupitika kwa urahisi,” amesema Kigua.

Azindua jengo la halmashauri ya Handeni

Katika hatua nyingine, Rais Samia amezindua jengo la Halmashauri ya Mji wa Handeni huku akiwataka watumishi kutoa huduma kwa wananchi, badala ya kupandisha mabega.

Amesema jengo hilo ni kati ya majengo 122 yaliyojengwa katika halmashauri mbalimbali ndani ya miaka minne.

Ameeleza dhamira ya ujenzi wa majengo hayo, ni kumpunguzia mwananchi adha ya kuzunguka kutafuta huduma.

“Kwa wanangu watakaofanya kazi kwenye jengo hili, yale makoti na briefcase mtakazobeba yasiwapandishe mabega, mnatakiwa kuwahudumia wananchi,” amesema na kuibua shangwe kutoka kwa wananchi.

Kwa upande wa changamoto ya upungufu wa umeme, amesema Serikali imeanza kufanyia kazi kwa kujenga kituo cha kupozea umeme.

Amesema kitakapokamilika, kitaongeza kiwango cha umeme unaoingia katika eneo hilo.

Rais Samia amesema utekelezaji wa miradi yote ni matokeo ya kodi zinazokusanywa katika halmashauri na mapato mengine.

Amesema Serikali imekataa watu kulimbikiziwa kodi na isingependa kuona wananchi wanakwepa kulipa pia.

“Ninazo taarifa kwamba wapo baadhi ya wananchi hawaielewi falsafa hiyo, hawalipi kodi na wanaipuuza,” amesema.

Amesema katika halmashauri hiyo pamoja na kufanya vizuri katika makusanyo, lakini zingekusanywa nyingi zaidi iwapo kila upande ungetekeleza wajibu wake kwa hiari.

Related Posts