Unguja. Licha ya msisitizo kwa wawekezaji kuhakikisha wanawaajiri wazawa katika miradi ya uwekezaji, bado wananchi kisiwani hapa wanahisi kutonufaika na fursa zinazotajwa huku Serikali ikisema tatizo ni viwango.
Akizungumza katika Baraza la Wawakilishi leo Jumanne Februari 25, 2025, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mudrick Ramadhani Soraga amesema wazawa hawajanufaika na fursa za utalii kutokana na kutokuwa na sifa na kukidhi viwango vya kuajiriwa katika sekta za utalii.
“Nikiri kuwa vijana wetu bado hawajanufaika na fursa za utalii Zanzibar licha ya Serikali kutoa maelekezo kwa wawekezaji kuajiri wazawa, kwani wanaonekana hawana uwezo wa kuajirika,” amesema Soraga.
Waziri Soraga amesema, Serikali ina kazi ya kuwajengea uwezo vijana wazawa ili kuwa na sifa zitakazowafanya kuajirika katika miradi ya maendeleo inayowekezwa kisiwani hapa, huku akisisitiza kuwa wizara anayoiongoza inaendelea kufanya mapitio Sera ya Utalii ambayo kwa sasa inaratibiwa kwa ajili ya kuwasilishwa katika kikao cha makatibu wakuu.
Soraga amesema, katika rasimu hiyo kuna maeneo ya utekelezaji yatakayowashirikisha na kuwanufaisha wazawa wa visiwa vya Unguja na Pemba kupitia programu maalumu za utalii kwa wote na utalii endelevu.
Kauli ya Soraga, ilitokana na hoja ya Mwakilishi wa Mwanakwerekwe, Ameir Abdalla Ameir aliyetaka kufahamu malengo ya sera mpya ya utalii katika dhana ya kuwanufaisha wazawa.
Wakati huohuo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Shariff Ali Shariff amesema Serikali inatumia mbinu mbalimbali kurejesha imani ya wananchi ambao wanaamini hawanufaiki na uwekezaji unaofanyika karibu na maeneo yao.
Sharrif alikuwa akijibu hoja ya Mwakilishi wa Kiembesamaki, Suleiman Haroun Suleiman aliyehoji baadhi ya maeneo ya uwekezaji Zanzibar, kutonufaisha wananchi kinyume na ahadi ya Serikali kuwa wanapokuwepo wawekezaji wananchi wa eneo husika hupata manufaa.
Mwakilishi huyo alitaka kufahamu, Serikali inatumia mbinu gani kurejesha imani ya wananchi ambao wanaamini hawanufaiki na baadhi ya wawekezaji waliopo karibu na maeneo yao.
Akijibu hoja hiyo, Waziri Shariff amesema Serikali imekuwa ikijitahidi kuwa wazi kuhusu manufaa ya miradi ya uwekezaji kwa jamii, hiyo ni pamoja na kutoa taarifa kuhusu miradi inayofanyika, namna inavyonufaisha wananchi, na jinsi Serikali inavyohakikisha uwekezaji unachangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Pia, amesema Serikali imeweka sheria na kanuni zinazohakikisha wawekezaji wanazingatia masilahi ya jamii ikiwemo wawekezaji kutoa sehemu ya faida kwa ajili ya miradi ya kijamii kama vile elimu, afya na miundombinu ili kuhakikisha wananchi wanapata manufaa ya moja kwa moja.