Dar es Salaam. Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imepata mabadiliko makubwa katika mfumo wake wa biashara changa bunifu (startup), ikishuhudia ongezeko la ufadhili na kuibuka kwa wajasiriamali wabunifu.
Kwa mujibu wa ripoti ya Africa: The Big Deal, startups za Tanzania zimekusanya karibu dola milioni 300 (Sh750 bilioni) tangu mwaka 2019, na kuifanya nchi kuwa miongoni mwa maeneo 10 bora barani Afrika kwa uwekezaji wa startup, hata hivyo mabadiliko haya hayakutokea kwa usiku mmoja.
Wataalamu na wajasiriamali wanasema kuwa ukuaji huu umetokana na maboresho ya udhibiti, kuongezeka kwa imani ya wawekezaji na kizazi kipya cha wajasiriamali wa teknolojia wanaobadilisha sekta mbalimbali.
Hata hivyo, Kenya bado inaongoza katika ufadhili wa startup Afrika Mashariki, ikivutia dola bilioni 3.3 tangu 2019 zaidi ya asilimia 80 ya jumla ya ufadhili wa eneo hili. Tanzania, ingawa ipo nyuma ya jirani yake, imekuwa ikikusanya kasi kimya kimya.
Startup za huduma za kifedha, nishati na biashara mtandaoni zimekuwa mstari wa mbele, huku kampuni kama Nala na Zola Electric zikivutia uwekezaji mkubwa.
Akizungumza na gazeti dada la The Citizen, Victor Joseph, kutoka Tembo Plus, alikumbuka kipindi ambacho ilikuwa vigumu kupata ufadhili kwa startup nchini Tanzania.
“Siku za nyuma, wawekezaji walikuwa wakipuuza Tanzania kwa sababu soko lilionekana kuwa halijachangamka na lenye hatari kubwa. Lakini sasa tumeonyesha kuwa kuna fursa halisi hapa,” alisema.
Kwa miaka mitano iliyopita, mfumo wa startup Tanzania umebaki kwenye kivuli cha Silicon Savannah ya Kenya na miji mikubwa ya teknolojia kama Lagos, Nigeria.
“Wawekezaji walikuwa wakitaja changamoto kama urasimu, kutokuwapo kanuni zilizo wazi na upatikanaji mdogo wa mitaji ya ndani kama sababu za kusitasita kwao. Lakini sasa, nchi imechukua hatua kubwa kuboresha mazingira ya startup,” alisema Joseph.
Mojawapo ya mambo makuu yaliyosababisha mabadiliko haya ni Serikali kuongeza kuzijali startups.
“Mustakabali wa startup nchini ni mzuri kwani Serikali imechukua hatua ya kuanzisha kanuni zilizo wazi zaidi kwa startups, ikiwa ni pamoja na kuandaa Sera ya Taifa ya Startup. Hatua hii, pamoja na juhudi za kufanya usajili wa biashara kidijitali na kurahisisha taratibu za kodi, zimeifanya Tanzania kuwa kivutio kwa wawekezaji,” alieleza Joseph.
Kwa upande wake, Catherinerose Barretto, mwanzilishi mwenza wa Binary Labs, anaamini kuwa startups za ndani sasa zimekuwa na ushindani zaidi.
“Sasa tunaona mifumo bora ya biashara, timu zenye nguvu na bunifu zenye kuleta suluhu zaidi na wawekezaji wameanza kutambua hili,” alisema.
Sambamba na hayo, startups za Tanzania zimeanza kupata fursa zaidi za ufadhili. Mbali na mitaji ya kimataifa, mipango ya ndani kama Tanzania Venture Capital Fund, inayotarajiwa kuzinduliwa mwaka huu, inatarajiwa kutoa mtaji kwa biashara zenye matumaini.
Kama ilivyo kwa maeneo mengine ya Afrika, teknolojia ya huduma za fedha imekuwa injini kuu ya ukuaji wa startup Tanzania. Mathalani kampuni kama Nala, (jukwaa la malipo ya kidijitali), imekusanya mamilioni ya dola kwa kutoa huduma rahisi za uhamishaji wa fedha kwa Watanzania waishio nje ya nchi.
Vilevile, startup za nishati mbadala zimevutia uwekezaji mkubwa. Zola Electric imepata fedha kwa ajili ya kupanua huduma zake za nishati ya jua.
Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Horizon Digital Tanzania, Furaha Mohamed, amesema wawekezaji wanavutiwa zaidi na startups zinazotatua matatizo halisi.
“Tasnia ya teknolojia ya huduma za kifedha imepata Tanzania mafanikio makubwa kwa sababu ya mahitaji makubwa ya ujumuishaji wa kifedha. Wawekezaji wanatambua fursa hii na wanasaidia kampuni zenye uwezo wa kukua,” alisema Mohamed.
Kuongezeka kwa matumizi ya pesa kupitia simu na mifumo ya malipo ya kidijitali pia kumechochea ukuaji wa startup nchini.
“Kuenea kwa simu za mkononi Tanzania kumeongezeka kwa kiasi kikubwa, hivyo kufanya miamala ya kidijitali kupatikana kwa urahisi zaidi na kufungua milango kwa startups za teknolojia ya fedha.”
Naye mwanzilishi wa Kiasi App, Emansi Kiula, alibainisha kuwa wajasiriamali wa Tanzania sasa wanajua vyema jinsi ya kupata uwekezaji.
“Mazingira yamebadilika. Sasa tuna fursa bora zaidi kupitia programu za kukuza biashara (accelerators), mashindano ya uwekezaji (pitch competitions) na hata hivi karibuni tutakuwa na mifuko ya uwekezaji inayoungwa mkono na Serikali,” alisema Kiula.
“Huu ni mwanzo tu. Tukidumisha kasi hii, Tanzania inaweza kuwa mojawapo ya vituo vikubwa vya startup barani Afrika ndani ya muongo mmoja ujao.”
Hata hivyo pamoja na maendeleo haya, mfumo wa startup Tanzania bado inakabiliwa na changamoto kadhaa. Moja ya changamoto kubwa ni mazingira ya udhibiti. Ingawa juhudi zinafanyika kutengeneza sera rafiki kwa startup, baadhi ya wajasiriamali bado wanahisi kuwa kuna urasimu mwingi.
Kwa upande mwingine, mtafiti kutoka Shikana Group, Isai Mathias, alisisitiza kuwa kudumisha imani ya wawekezaji kutahitaji zaidi ya mabadiliko ya sera pekee.
“Sekta inahitaji mitandao ya mitaji ya ndani imara zaidi (venture capital), programu za ushauri kwa wajasiriamali, na ujumuishaji bora na masoko ya kikanda,” alieleza Mathias.
Changamoto nyingine kubwa ni upungufu wa vipaji. Ingawa Tanzania ina idadi kubwa ya vijana wanaojua teknolojia, bado kuna uhaba wa wajasiriamali waliowahi kuanzisha na kukuza startup kwa mafanikio.
“Hili huwafanya wawekezaji kusitasita kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha,” alihitimisha Mathias.