Dodoma. Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imetenga Sh3 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya amali kwenye shule 20 nchini, lengo likiwa ni kuwezesha utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023 na mtaala mipya.
Mwaka jana Serikali ilianza utekelezaji wa mtaala huo kwa awamu ambapo wameaanza na elimu ya awali, darasa la kwanza, la tatu, kidato cha kwanza na mwaka wa kwanza wa ualimu.
Jumla ya shule 98 za sekondari teule, 28 zikiwa za Serikali na 68 zisizo za Serikali zilipangwa kuanza utekelezaji kwa kutoa mafunzo ya amali ikiwa ni sehemu ya utekelezaji mitaala mipya ya elimu iliyoboreshwa.
Hata hivyo, Februari 11, 2025, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, ilisema kuwa uhaba wa walimu wa amali wenye sifa na weledi na ukosefu wa vyuo maalumu kwa mafunzo ya ualimu wa amali, ambapo mahitaji ni walimu 620, waliopo 62 na upungufu 558.
Mwenyekiti wa kamati huyo, Husna Saiboko amesema uhaba wa vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia ukosefu wa miundombinu sahihi kama vile maabara na warsha za vitendo.
Saiboko alisema hali hiyo inakwamisha na kuzorotesha elimu ya amali nchini pamoja na utekelezaji wa mtaala wa mafunzo ya amali katika shule za Serikali.
Pamoja na mambo mengine ilitaka Serikali kuongeza bajeti ya kutosha ya kuajiri walimu wenye sifa na weledi wa masomo ya amali kulingana na mahitaji na kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya kisasa kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia katika shule za amali.
Pia kamati hiyo ilitaka Serikali iboreshe vifaa na miundombinu muhimu katika shule za Serikali ambazo zimeanza utekelezaji wa mtaala katika mkondo wa amali.
Akizungumza kuhusu mafanikio ya miaka mine ya Serikali ya awamu ya sita, leo Jumanne Februari 25, 2025 Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dk Erasmus Kipesha amesema katika kuhakikisha kuwa mtaala mpya wa elimu unatekelezwa mamlaka imetenga Sh3 bilioni.
“Kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa mafunzo ya amali katika shule zilizochaguliwa kuanza kufundisha mafunzo hayo. Na katika kiasi hiki cha fedha shule 20 zitakwenda kunufaika,”amesema.
Amesema kiasi hicho cha fedha kitahusisha ujenzi wa miundombinu lakini ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia,”amesema
Aidha, Dk Kipesha amesema TEA imejipanga kutekeleza miradi 113 yenye thamani ya Sh11.3 bilioni kwa mwaka 2024/25.
Amesema katika utekelezaji wa miradi hiyo 113 wanafunzi 19,482 na walimu 12 watanufaika na miradi hiyo.
Pia amefafanua kuwa TEA inasimamia mifuko miwili ambao ni mfuko wa kuendeleza ujuzi na mfuko wa elimu ambapo katika kipindi cha miaka minne imepokea Sh49.05 bilioni kwa ajili ya mfuko wa elimu.
Amesema Sh2.8 bilioni zilipelekwa kwenye mfuko wa kuendeleza ujuzi na Sh4.11 bilioni zilitoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo kwa ajili ya kusaidia kuendeleza mamlaka hiyo.
Kuhusu idadi ya watu walionufaika na mfuko wa kuendeleza ujuzi Kaimu Mkurugenzi Utafutaji na Usimamizi wa Miradi ya Elimu wa TEA, amesema Masozi Nyirenda takribani watanzania 49,000 wamenufaika huku wanawake wakiwa ni zaidi ya 2,000, Makundi maalum 474, kaya maskini 4000 na 600 kutoka Zanzibar.
Akifafanua kuhusu nini kitakachokwenda kufanyika katika mitaala mipya, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za taasisi wa TEA, Mwanahamis Chambega amesema watakwenda kuboresha miundombinu pamoja na ununuzi wa vifaa vya kujifunzia kulingana na mafunzo yanayotolewa kwenye shule husika.
“Kwa mfano kama shule inatoa elimu kwa mkondo amali wa michezo basi tutaboresha viwanja vya michezo, kama ni muziki basi tunanunua vifaa vya kujifunzia na ICT basi nako tutawaboreshea na iwapo ni kilimo tutaangalia pia mashamba,”amesema.
Amesema kwa mwaka huu wameanza na kiasi hicho cha fedha na kwamba wataendelea kutenga bajeti kwa ajili ya eneo hilo.