TMA yatoa angalizo jipya uwepo wa upepo mkali kwa siku tano, Dar imo

Dar es Salaam. Kwa mara nyingine Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa angalizo la uwepo wa upepo mkali na mawimbi makubwa katika pwani ya kaskazini mwa Bahari ya Hindi.

Kwa takribani wiki moja sasa TMA imekuwa ikitoa angalizo kuhusu hali hiyo ikieleza kiwango cha athari zinazoweza kutokea ni wastani.  

Kwa mujibu wa taarifa ya hali mbaya ya hewa kwa siku tano, TMA imetoa angalizo la upepo mkali kuanzia leo Februari 25, 2025 hadi Alhamisi Februari 27.

“Angalizo la upepo mkali unaofikia kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofikia mita mbili, limetolewa kwa baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani ya Kaskazini mwa Bahari ya Hindi,” imesema taarifa hiyo.

Mikoa inayotajwa kwa siku ya leo Februari 25 ni Lindi, Mtwara, Tanga, Dar es Salaam na Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, Unguja na Pemba.

Kwa Februari 26 na 27, TMA imetoa angalizo hilo kwa maeneo ya ukanda wa pwani kaskazini mwa Bahari ya Hindi mikoa ya Tanga, Dar es Salaam na Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, Unguja na Pemba.

“Athari zinazoweza kujitokeza, kuathirika kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi, uvuvi na usafirishaji baharini,” imeeleza mamlaka hiyo.

Kwa Februari 28 na Machi Mosi, 2025 hakuna tahadhari iliyotolewa na TMA.

Taarifa ya Februari 20 ya TMA ilitoa angalizo kuhusu hali mbaya ya hewa ikihusisha upepo mkali na mawimbi makubwa kuanzia Ijumaa Februari 21 katika ukanda huo.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, mtalii mmoja aliyekuwa kwenye boti katika alipotea na baadaye kupatikana akiwa hai kutokana na upepo mkali na mawimbi.

Mtalii huyo alipotea katika Bahari ya Hindi, Kisiwa cha Songosongo alipokuwa akifanya utalii na alipatikana akiwa hai katika eneo la Kilwa Kivinje, wilayani Kilwa mkoani Lindi.

Raia wa kigeni kutoka nchini Ufaransa, Nakar Fszman (51), kwa mujibu wa taarifa ya Polisi Mkoa wa Lindi alipotea Februari 23, 2025, wakati akifanya utalii kwa kutumia boti aina ya Kayati maarufu Kidau. Aliwasili nchini Februari 16, 2025 akiwa na mkewe na watoto wawili.

Alipatikana Februari 24, 2025, saa tatu asubuhi katika pwani ya Kilwa Kivinje, umbali wa maili nane za baharini (takribani kilomita 12.9) kutoka alikopotea.

Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuchukua tahadhari wanapoona hali mbaya ya hewa kwa kuepuka safari za baharini hadi upepo utakapopungua.

Related Posts