Tuko Tayari Usitishaji Mapigano – Global Publishers



Muungano wa waasi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Alliance Fleuve Congo (AFC), unaojumuisha waasi wa M23, umetangaza kuwa tayari kushiriki mazungumzo na serikali ili kusitisha mara moja mapigano mashariki mwa nchi, msemaji wa kundi hilo amesema.
Lawrence Kanyuka amechapisha ujumbe kwenye ukurasa wake wa mtandao waa X, akitangaza kuwa AFC imejitolea kwa suluhisho la mazungumzo ya mgogoro.

Amesema hatua hiyo inalenga kuwezesha utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa hivi karibuni katika mkutano wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), pamoja na mkutano wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika.

Kanyuka amesema:”Maazimio haya yanatoa wito wa kusitisha mapigano kati ya pande husika na mazungumzo ya kisiasa kati ya Serikali ya Kongo na AFC/M23. Tunatumaini kuwa serikali, wakati huu, itaheshimu na kutekeleza kikamilifu maazimio haya.”

Katika taarifa tofauti, muungano wa waasi uliishutumu serikali ya DRC na wanamgambo washirika wao kwa kuendelea kufanya mashambulizi ya ardhini na angani dhidi ya raia katika maeneo kadhaa, hasa Uvira na Minembwe katika jimbo la South Kivu.

Hayo yanajiri wakati ambao Tanzania jana Jumatatu, ilikuwa ni mwenyeji wa mkutano wa kikanda, kufuatilia matukio ya nyanjani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kuchukua hatua zinazohitajika za kukabiliana na mgogoro huo.

Mkutano huo unahudhuriwa na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Katika mapigano ya hivi karibuni, waasi wa M23 wameteka miji miwili mikubwa ya DRC ambayo ni Goma na Bukavu katika eneo lenye utajiri wa madini la mashariki mwa nchi hiyo.


Related Posts