Dar es Salaam. Joto la Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 limeendelea kupanda jijini Arusha ambapo Paul Makonda na Mrisho Gambo wanatajwa kuwa katika mvutano wa kuwania ubunge.
Makonda ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Gambo, mbunge wa Arusha Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) wamekuwa kwenye mvutano wa hapa na pale katika siku za karibuni na sasa ‘vita’ hivyo vinatajwa kuelekea kwenye uwakilishi wa wananchi.
Licha ya Makonda kutoweka wazi kama anautaka ubunge, lakini kitendo cha madiwani wa Arusha kumwomba kuwa wakati ukifika awania ubunge, kimemwibua Gambo akitaka aachwe atekeleze wajibu wake na “yeyote anayetaka kuwania asubiri tu muda utafika, utaratibu utatangazwa halafu aje uwanjani aone kama ngoma ya kitoto inakesha.”
Wawili hao si mara ya kwanza kuonekana kama wanavimbiana kwani Januari 6, 2025 waliibua mzozo baada ya Gambo kuwasilisha kwa Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega aliyekuwa ziarani mkoani Arusha ombi la kujengwa barabara ya kona ya Kiseria – Mushono ili kupunguza foleni kuelekea kwenye mashindano ya Afcon 2027.
Kwa mujibu wa Gambo, katika barabara hiyo Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) umejenga kilomita moja na mwaka huu wa fedha haikutengewa bajeti, licha ya kupelekwa maombi maalumu na kuahidiwa kwamba itatekelezwa.
“Ombi langu jingine ni barabara ya Arusha – Kibaya hadi Kongwa, ambayo Jiji la Arusha tungepata kilomita 27, lakini tangu mwaka 2022 hatujamuona mkandarasi. Ningependa utumie fursa hii utueleze zile kilomita 27 kwa ajili ya Afcon, Serikali ina mpango gani wa kuziweka vizuri,” alisema Gambo.
Makonda ambaye naye alikuwa jirani, alipopokea kipaza sauti na kusema maombi yanayotolewa na mbunge huyo ni kwa sababu hahudhurii vikao, kwani yalishajadiliwa vikaoni, akisisitiza anachokifanya ni utovu wa nidhamu.
“Nimsaidie Waziri (Ulega). Hoja alizozisema Gambo, kwenye vikao haji. Ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu kumsubiri kiongozi kwenye hadhara ili umvizie upachike mambo,” alisema Makonda.
Jana Jumatatu, Februari 24, 2025 katika mkutano wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Arusha baadhi ya madiwani walimuomba Makonda muda ukifika achukue fomu ya kutwaa ubunge wa Arusha Mjini.
Aliyeanzisha suala hilo ni Naibu Meya wa jiji hilo, Ibrahim Mollel ambaye alimtaka Makonda aliyeingia muda mfupi ukumbini hapo, achukue fomu ya ubunge muda ukifika.
“Muda ukifika chukua fomu tupo nyuma yako, sisi ni miongoni mwa watu waliopangiwa watu lakini siogopi. Nishakuwa mwenezi wa wilaya, Mungu kaniweka nimekuwa diwani, Mungu kaniweka chukua maneno haya nenda nayo kayafanyie kazi,” amesema Mollel.
Japokuwa Makonda hakutoa msimamo kufuatia kauli ya madiwani hao, aliwataka kuchukua hatua kwa watendaji ambao hawaendani na kasi yao.
“Msibaki mnanung’unika eti kuna wakubwa, hakuna wakubwa kwenye mkoa huu, mimi kwenye mkoa huu sitalinda mtu mvivu, mvivu halindwi mlarushwa halindiwi, nataka Rais akija aone maendeleo kwenye mkoa huu,” alisema Makonda.
Leo Jumanne, Februari 25, 2025, Gambo aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ameibuka kujibu kile kilichoelezwa na madiwani hao, akisema yeye ndiye mbunge wa jimbo hilo, anayetaka ubunge asubiri muda ufike waingie ulingoni.
Gambo kupitia kipande cha video, ameonekana akitoa maelezo hayo akisema alihudhuria kwenye kikao cha Baraza la Madiwani na baada ya shughuli zote muhimu kukamilika, aliondoka kuendelea na majukumu mengine yaliyomsubiri.
“Badaye nilipata taarifa kuwa Makonda alihudhuria mkutano huo na kulikuwa dalili zote za kuwepo kwa ‘watu wake aliowatengeneza’ kuzungumza yale masuala waliyozungumza,” amesema.
Gambo amedai kiini cha kutokea hujuma hizo, kulikuwa ni eneo la ujenzi wa shule ya msingi kata ya Muriet, ambalo njama zilifanyika kununuliwa Sh552 milioni kwa ekari tano, lakini aliingilia kati akiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na eneo likapatikana kwa Sh300 milioni ekari sita.
Kutibua dili hilo ndiko anakoeleza ni kinyongo cha baadhi ya watu, ambao walipanga kuiba fedha hizo.
Amesema hakuna anayeweza kumfanya lolote, ndio maana njama hizo dhidi yake zimesukwa.
“Nafasi pekee waliyotumia ni kumuita Makonda na kukaa naye kuelezea kiu yao, watu hao wanafahamika hawazidi wanne ambao walifanya jambo hilo. Nitoe rai kwa chama changu na Serikali, mimi ndiye mbunge niliyepo madarakani, natumika kutekeleza wajibu wangu kama mbunge.
Kama kuna kiongozi yeyote anayetamani nafasi ya ubunge hakuna mtu anayekatazwa, cha msingi asubiri tu muda, utaratibu utatangazwa aje uwanjani aone kama ngoma ya kitoto inakesha,” amesema.
Gambo amesema: “Sisi wengine kwa sababu tuna uzoefu na masuala ya kisasa wala sina wasiwasi wowote, ukishaona mtu anatafuta madiwani awatengeneze wamuombe agombee, madiwani wana nafasi yao kumchagua mwenyekiti wa halmashauri au meya, ila mbunge anachaguliwa na wajumbe na wananchi.”
Kufuatia mvutano huo, Mchambuzi wa Masuala ya kisiasa Buberwa Kaiza amesema si mara ya kwanza kwa Makonda kufanya hivyo kwani aliwahi kujaribu kwa Hayati Faustine Ndugulile aliyekuwa mbunge wa Kigamboni akashindwa kupitia kura za maoni.
“Historia ya Makonda ipo na amewahi kushindwa hata kwa jitihada za kuitaka Kigamboni, mashindano haya yanaonyesha wazi watu wanatafuta ajira na sio kuwatumikia wananchi,” amesema.
Anachokisema Kaiza ni kile kilichotokea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ambapo Makonda alikuwa miongoni mwa wana CCM waliojitosa kugombea ubunge wa Kigamboni.
Hata hivyo, Dk Ndugulile aliyekuwa akitetea nafasi hiyo, aliibuka mshindi kwa kura 190 kati ya 369 zilizopigwa na Paul Makonda ameshika nafasi ya pili baada ya kupata kura 122.
Kwa sasa jimbo la Kigamboni liko wazi kufuatia Dk Ndugulile kufariki dunia Novemba 27, 2024 nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu.
Januari 2019, Gambo akiwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha aliingia kwenye ugomvi dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqarro. Kipande cha picha jongefu kiliwaonyesha wakitupiana maneno kuhusu suala la mabati katika Kituo cha Afya Murieti.
Mzizi wa ugomvi huo ulikuwa wasiwasi ulioonyeshwa kuhusu kiwango cha mabati yaliyotumika katika ujenzi wa kituo hicho cha afya, ambayo ni geji 30 badala ya 28 inayotakiwa na Serikali.
Ugomvi mwingine uliomhusu Gambo ulikuwa dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dk Maulid Madeni, akimtuhumu kwa kupeleka maneno kwa wakuu wake na hivyo kumharibia.
Katika kipande kingine cha picha jongefu, Novemba 2019, Gambo alionekana akimsema Dk Madeni: “Msemaji wa mkoa huu ni Mkuu wa Mkoa na halmashauri zote zipo chini ya Mkuu wa Mkoa. Hakuna anayeweza kuwa na kauli zaidi ya Mkuu wa Mkoa.”
Kwa upande wa Makonda, Septemba 25, 2019 akiwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, katika moja ya mkutano wake na wakuu wa wilaya, aliwahi kumfokea aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo akimtaka akae kimya, baada ya kujaribu kufafanua maswali yaliyoulizwa na Makonda.
“Wee… kaa kimya.. kaa kimya. Hakuna mtumishi ambaye yuko juu ya hili, hatufurahii ujinga hap,a hakuna mtumishi aliye juu ya Katibu Tawala wa Mkoa, mtumishi yeyote anayejua wajibu wake anajua nafasi ya RAS,” alisema Makonda.
Pia Mei, mwaka 2017 Makonda alitishia kuwachapa viboko watumishi wa umma, iwapo wangebeba mabango katika sherehe za Mei mosi, kushinikiza nyongeza ya mshahara.
“Ningewaona sijui jumangapi ile tarehe moja, Mei mosi mmebeba mabango eti, bila kuongeza mshahara ,hii kauli ya hapa kazi tu, ningewachapa viboko wala msingeamini,” alisema.