Ugonjwa wa ajabu waibuka DRC, WHO yadai unaua ndani ya saa 48

Ugonjwa wa ajabu usiojulikana umeua zaidi ya watu 50 ndani ya saa chache baada ya kuanza kwa dalili zao huko Kaskazini Magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Tovuti ya Daily Mail imeripoti leo Jumanne Februari 25,2025, kuwa takriban watu 419 wameripotiwa kuugua ugonjwa huo, huku kukiwa na vifo 53, tangu mlipuko wa ugonjwa huo ulipoanza nchini DRC mnamo Januari 21.

“Hilo ndilo linalotia wasiwasi zaidi,” amesema Serge Ngalebato, ambaye ni Mkurugenzi wa Matibabu wa Hospitali ya Bikoro ambacho ni Kituo cha Ufuatiliaji cha kikanda.

Kwa mujibu wa WHO Afrika, mlipuko wa kwanza ulianza Mji wa Boloko baada ya watoto watatu kula popo na kufariki ndani ya saa 48 na kuonyesha dalili za homa ya kutokwa damu.

Kumekuwa na hofu ya muda mrefu kuhusu magonjwa yanayolipuka kutoka kwa wanyama hadi kwa binadamu.

Idadi ya milipuko kama hiyo barani Afrika imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 60 katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, WHO ilisema mwaka 2022.

WHO pia imesema baada ya mlipuko wa pili wa ugonjwa huo wa ajabu kuanza katika Mji wa Bomate Februari 9, sampuli kutoka kesi 13 zimetumwa katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Baiolojia ya DRC (INRB) iliyoko Kinshasa kwa uchunguzi.

Sampuli zote zimeonekana kuwa hasi kwenye ugonjwa wa Ebola, na magonjwa mengine ya kawaida ya homa ya kutokwa damu kama Marburg.

Baadhi ya sampuli zilionyesha uwepo wa malaria.

Mwaka jana, ugonjwa mwingine wa ajabu wenye dalili kama homa ambao uliua watu kadhaa katika sehemu nyingine ya Congo ulithibitishwa kuwa huenda ulikuwa malaria.

Mapema mwezi huu, WHO ilionya kuwa ongezeko la hivi karibuni la ghasia mashariki mwa Congo limesababisha uharibifu wa miundombinu muhimu ya afya.

WHO imeendelea kuwepo eneo hilo tangu wakati huo ikitoa vifaa vya matibabu, kusaidia wahudumu wa afya na kuratibu shughuli za dharura.

Mbali na hilo, DRC kwa sasa ni miongoni mwa nchi zilizoathirika zaidi na mlipuko wa magonjwa mbalimbali ikiwamo Mpox.

Nchi hiyo imerekodi matukio 79,519 yanayoshukiwa kuwa ya Mpox na vifo 1,507 katika majimbo 26 kati ya wiki ya kwanza ya 2024 na wiki ya sita ya 2025 kwa mujibu wa takwimu rasmi za WHO.

Wiki hii, Wizara ya Afya ya Umma, Usafi na Ustawi wa Jamii imezindua kampeni ya chanjo ya Mpox inayolenga kuwafikia zaidi ya watu 660,000.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts