Utafiti: Zanzibar kuna popo 32,000

Unguja. Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Kimataifa ya Uhifadhi wa popo (Bat Conservation International) ya mwaka 2020 umeonesha jumla ya popo 32,000 wanapatikana kisiwani hapa kati yao 7,560 wanapatikana bandari ya Wete.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Shamata Shaame Khamis leo Jumanne  25,2025 katika Baraza la Wawakilishi wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohammed Ali Suleiman.

Dk Mohammed alihoji juu ya wasiwasi wa kupungua kwa popo hao (flying fox) ambao kwa wingi wanapatikana eneo la bandarini Wete.

Mwakilishi huyo alitaka kufahamu tafiti zinazoonesha kuhusu wingi na uzalishaji wa popo hao katika eneo hilo, juhudi za Serikali za kuwalinda kwani wapo katika orodha ya wanyama walio katika hatari ya kupotea na Serikali inawatumia vipi ili waweze kuleta tija kwa wananchi.

Akijibu hoja hizo, Waziri Shamata amesema miongoni mwa juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuwalinda popo hao wa Pemba ni pamoja na kulindwa kisheria kwa kuwekwa katika kundi la kwanza (Appendix I) katika Sheria namba 10 ya mwaka 1996 ya misitu.

Amesema, kundi hilo limejumuisha  wanyamapori wanaohitaji kuwekewa ulinzi wa hali ya juu ikiwa pamoja na kupiga marufuku uwindaji wao.

“Pia, kuanzisha vilabu vya uhifadhi wa popo katika Kisiwa cha Pemba ikiwemo Kidike, Makoongwe na Mjini-wingwi na kuanzisha programu maalumu mashuleni kwa ajili ya kutoa uelewa wa elimu wa uhifadhi wa popo,” amesema Shamata

Shamata amesema, shughuli za uhifadhi wa popo pamoja na popo zimekuwa kivutio maalumu cha utalii, hivyo kuwaingizia kipato wananchi, pia mifumo ya ikolojia ya popo hao wamekuwa wakitumika katika tafiti mbalimbali.

Waziri huyo, amesema utafiti uliofanywa mwaka 2010 umeonesha uwepo wa popo 22,100 katika kisiwa cha Pemba kati yao 6,729 wanapatikana katika eneo la bandari ya Wete.

“Utafiti uliofanywa 2010 ulionyesha idadi ya popo 22,100 katika kisiwa cha Pemba kati ya hao 6,729 wanapatikana katika eneo la bandari ya Wete, na utafiti uliofanywa mwaka 2020 umeonyesha popo 32,000 wanapatikana kisiwani Pemba kati yao popo 7,560 wanapatikana bandari ya Wete, Hiyo inaonyesha ongezeko la asilimia 12.35 la katika eneo hilo,” amesema Shamata

Hivyo kulingana tafiti hizo, Shamata amesema ni wazi kuwa popo wengi wanaonekana kuwepo katika bandari hiyo hivyo wizara inatoa elimu kwa wananchi wa maeneo hayo kuendelea kuwalinda.

Amesema, kawaida ya popo wanakaa katika sehemu ambayo wanapata utulivu ili kufanya shughuli zao kwa maana hiyo hawapaswi kubughudhiwa.

Related Posts