Moshi/Shinyanga. Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) umewaonya vijana juu ya usaliti, fitna, mgawanyiko katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, ili kujihakikishia ushindi wa kishindo.
Pia umewasisitiza kuzingatia maadili, uadilifu na kudumisha umoja na mshikamano huku ukisema CCM lazima ishinde katika uchaguzi mkuu ujao kwa lengo la kuendelee kutatua shida na changamoto zinazowakabili Watanzania.

Naibu katibu mkuu wa UVCCM Bara, Mussa Mwakitinya, akizungumza wakati akifungua kambi ya vijana wa chama hicho, Mkoa wa Kilimanjaro
Hayo yamesemwa leo Jumanne, Februari 25,2025 na Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Bara, Mussa Mwakitinya wakati akifungua kambi ya siku sita ya vijana zaidi ya 708 wa UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro, inayofanyika Wilaya ya Hai mkoani humo.
Mwakitinya amesema chama hicho kinastahili kushinda kutokana na kazi kubwa zilizofanywa na serikali yake na ametoa rai kwa vijana kuogopa kushindwa kwa chama hicho kama wanavyoogopa kutenda dhambi.
“Katika katiba yetu ya CCM imezungumza malengo ya chama na lengo kuu la kwanza ni kushinda uchaguzi na kushika dola, hivyo ushindi ni lazima wala si ombi,” amesema Mwakitinya.
Amesema UVCCM haitatamani chama chao kikashinda uchaguzi ili wakacheze rede, “Hapana, tunatamani kushinda ili tuendelee kutatua changamoto za Watanzania kwa sababu hakuna chama kingine chochote kinachoweza kutatua shida na changamoto za Watanzania isipokuwa CCM. Ndiyo maana tunatamani kuendelea kushinda ili watanzania waendelee kupata maendeleo.”

Mwakitinya amesema; “Kama kitabu chako cha dini kinakuambia usitende dhambi, sisi Katiba ya CCM inayotulinda imesema ni lazima tushinde. Kutoshinda au kushindwa, umetenda dhambi kwa Chama cha Mapinduzi, hivyo kama unavyoogopa kutenda dhambi kama kuiba, kusema uongo, kuzini na dhambi nyingine ndivyo hivyo hivyo unapaswa kuogopa CCM kushindwa.”
Amesema moja ya mambo ambayo vijana wanapaswa kuzingatia kwa umakini ni maadili na mienendo yao, kuhakikisha kuwa havileti changamoto kwa ushindi wa CCM.
“Kuna mambo ambayo yanaweza kutuletea matatizo endapo hatutakuwa waangalifu. Kijana anapaswa kuchunguza mienendo yake, kutambua njia sahihi za kufuata, kutenda mema na kuepuka mabaya. Ni muhimu kusimamia maadili na kufikia hatua ya kuelewa kuwa mtu anachokifanya kinaendana na matakwa ya chama.”
Ameongeza kuwa, “Kijana akiwa na maadili mabaya, kuna watu wanaoweza kusita kujiunga na CCM wakidhani kuwa wote ni sawa. Hivyo, mienendo isiyo ya kimaadili inaweza kuathiri juhudi za kuongeza wanachama au kufanikisha ushindi wa chama chetu. Ni jukumu letu kama vijana kujua jinsi ya kuishi kwa kuzingatia maadili.”
Amesisitiza umuhimu wa umoja na mshikamano ndani ya chama hicho ili kiendelee kuimarika.
Kiongozi huyo amesema kutengana ni mwanya wa adui kuingilia na kukidhoofisha chama, hivyo mshikamano ni silaha muhimu kwa ushindi wa CCM.
Aidha, amesisitiza uadilifu miongoni mwa wanachama, akiwataka vijana kuthamini imani inayowekwa kwao na chama.
“CCM inawaamini sana vijana, hivyo msiiangushe imani hiyo. Ukibebwa bebeka, ukisifiwa sifika na ukiaminiwa aminika,” amesema.
Kuhusu uaminifu ndani ya chama, Mwakitinya ameonya dhidi ya usaliti, akiwataka wanachama kutunza siri za chama na kuepuka kutoa taarifa kwa watu wa nje.
Amesema nyakati za uchaguzi ni muhimu zaidi kuwa na mshikamano wa kichama na wanachama wanaopoteza uaminifu wanapaswa kuondolewa kabla ya kukidhoofisha chama.
Hivyo, amewakumbusha vijana wa CCM kuepuka kuwagawa watu kwa misingi ya dini, ukabila au sababu nyinginezo, akisisitiza umuhimu wa mshikamano na kujitoa kwa dhati kwa ajili ya chama chao.
Katika mkutano huo, Mwakitinya amewahamasisha vijana kujitokeza kugombea nafasi za uongozi na kuepuka kutumiwa vibaya kisiasa.
“Msikubali kubebwa kwenye mabegi au mifuko ya watu. CCM inahitaji viongozi vijana, hivyo jitokezeni kugombea, tupo kwa ajili ya kuwaunga mkono,” amesema.

Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro, Ivan Moshi, akizungumza wakati wa ufunguzi wa kambi ya vijana wa chama hicho, mkoani humo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro, Ivan Moshi amewataka vijana wenye sifa na uwezo wa kugombea udiwani au ubunge kujitokeza wakati muafaka ukiika ili kutimiza ndoto zao.
Moshi amesema CCM kinajipanga kushinda uchaguzi, hivyo vijana wanapaswa kushiriki kikamilifu.
Naye Katibu wa UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro, Ahmady Kibamba amesema lengo la kambi hiyo ni kuwajenga vijana katika misingi imara ya kuleta ushindi kwenye uchaguzi mkuu sambamba na kuwaimarisha kiutendaji, kipropaganda, kiukakamavu, kiulinzi, usalama na maadili kwenye kipindi chote cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Mafunzo katika kambi hiyo iliyoanza leo, yatazungumzia mada za nafasi ya kijana katika uchaguzi, athari za dawa za kulevya, ujasiriamali, matumizi ya mitandao ya kijamii, usalama na maadili, falsafa ya ujamaa na kujitegemea, mikakati ya ushindi wa uchaguzi, madhara ya rushwa, fursa za kiuchumi kwa vijana na faida za muungano wa Tanzania.
Mwakitinya amewahimiza vijana kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi na kuhakikisha wanajenga chama chenye mshikamano, uadilifu na ushindi endelevu.

Wakati huo huo, Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini imetakiwa kusimamia maadili ya vijana ili kuhakikisha wanalelewa katika misingi bora ya kitanzania na kuepuka kujiingiza katika makundi yasiyofaa.
Hayo yameelezwa leo na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Anold Makombe, wakati wa kongamano la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuteuliwa kugombea tena nafasi ya urais mwaka 2025 pamoja na mgombea mwenza, Dk Emmanuel Nchimbi.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini Anold Makombe akizungumza na Jumuiya ya wazazi ya chama hicho kwenye kongamano lililofanyika mjini Shinyanga
Makombe amesisitiza kuwa kuporomoka kwa maadili kunatokana na baadhi ya wazazi kusahau wajibu wao wa msingi katika malezi ya watoto.
Hivyo, ameitaka Jumuiya hiyo kuhakikisha inatekeleza jukumu hilo kwa kuwaelimisha wazazi kuhusu umuhimu wa kuwalea watoto wao kwa misingi ya maadili na utamaduni wa Kitanzania.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti Makombe amepokea tuzo ya heshima kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia kutoka kwa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini.

Viongozi wa Jumuiya ya wazazi Wilaya ya Shinyanga mjini wakiwa wameshikilia tuzo ya heshima ambayo wamemtunuku Mwenyekiti wa CCM Taifa Dr Samia Suluhu kwa uongozi wake uliotukuka.
Tuzo hiyo imetolewa kwa lengo la kutambua uongozi wake thabiti na mafanikio makubwa katika maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii nchini.
“Rais Samia ameimarisha amani ya nchi yetu pamoja na utawala bora. Tunawaomba viongozi wa dini waendelee kuiombea nchi yetu, kumuombea Rais wetu na pia kuhakikisha uchaguzi mkuu ujao unafanyika kwa amani, uhuru, na haki,” amesema Makombe.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fue Mrindoko amesema wananchi wa Shinyanga wana kila sababu ya kuipongeza Serikali kwa kuwaletea maendeleo, ikiwamo utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Kwa upande wake, Mchungaji Andrea Salu wa Kanisa la EAGT Ndala, amemwelezea Rais Samia kama kiongozi imara anayepaswa kuungwa mkono kwa jitihada zake za kuleta maendeleo nchini.
Pia amewasihi wazazi kuhakikisha wanawalea watoto wao kwa maadili mema ili kujenga jamii yenye msingi bora wa maadili.