Geneva. Takriban watu 7,000 wamepoteza maisha katika kipindi cha Januari hadi jana Jumatatu, Februari 24, 2025, katika mapigano yanayoendelea mashariki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Taarifa ya vifo hivyo, imetolewa jana jijini Geneva, Uswisi na Waziri Mkuu wa DRC, Judith Suminwa alipohutubia mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza la Haki za Binadamu.
Takriban vifo 3,000 vimeshaorodheshwa huko Goma, alisema Judith Suminwa na karibu watu 450,000 wamebaki bila makazi baada ya kambi 90 za wakimbizi kuharibiwa katika mapigano hayo.
Tangu Januari, kundi la waasi la M23, linalotajwa kufadhiliwa na serikali ya Rwanda japo Rais Paul Kagame wa nchi hiyo amekuwa akikanusha madai hayo mara kadhaa, limeyatwaa maeneo makubwa ya mashariki mwa DRC ikiwemo miji ya Goma na Bukavu ambayo inasifika kwa kuwa na utajiri wa madini.
Mapigano ya hivi karibuni na kusonga mbele kwa M23, ni sehemu ya kuongezeka kwa mvutano mkubwa kati ya Serikali ya Rais Felix Tshisekedi wa DRC dhidi ya vikundi vya waasi vinavyozidi kujitanua mashariki mwa nchi hiyo.
Katika hotuba yake, Suminwa aliwaomba washiriki wote duniani wachukue hatua na kuiwekea Rwanda vikwazo ili kukomesha mauaji dhidi ya raia yanayoendelea mashariki mwa nchi hiyo.
“Haiwezekani kuelezea kilio na mpasuko wa mioyo ya mamilioni ya waathirika wa mgogoro huu,” alisema Suminwa.
Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, katika mkutano huko Geneva, alisema haki za binadamu ulimwenguni kote zinapuuzwa huku akitaja kuwapo kwa dhuluma za kutisha katika ardhi ya DRC.
“Ikiwa swali hili la ukiukaji wa uadilifu wa kijiografia halitatatuliwa, hali inaweza kudhoofika zaidi,” Suminwa aliieleza Reuters katika mkutano wa vyombo vya habari baada ya hotuba yake.
Takriban watu 40,000 wamekimbia makazi yao na kukimbilia Burundi, moja ya nchi tisa zinazopakana na DRC, katika kipindi cha wiki mbili ili kuepuka mapigano ilisema ripoti ya Umoja wa Mataifa.
Suminwa ameonya kwamba hali mbaya ya usalama inayosababishwa na M23 na vikundi vingine vyenye silaha inaweza kuenea hadi nchi jirani na kusababisha hali ya mtikisiko wa amani.
Katika mahojiano na Reuters Suzanne Amisi Wilonja alieleza namna waasi walipovamia nyumba yake karibu na uwanja wa ndege kwa lengo la kuiba wakifyatua risasi ovyo na kumpiga kichwani mtoto wake wa miaka 10 Sylvain.
Alisema kutokana na vurugu zilizokuwa zikiendelea nje hawakuweza kumpeleka Sylvain hospitali hadi asubuhi ya siku iliyofuata, na wakati huo mtoto wake alikuwa tayari amefariki.
“Tuliogopa kutoka nje kumpeleka hospitalini kwa sababu wanajeshi walikuwa wamegonga mlango wetu,” Wilonja ameiambia Reuters akitokwa machozi, akielezea jinsi alivyomuona mtoto wake akifariki dunia.
Hata hivyo, Msemaji wa jeshi la nchi hiyo alipotakiwa kutoa maoni kuhusiana na tukio hilo lililotokea mwisho wa Januari huko Goma, hakuwa tayari.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika