Dodoma. Wanafunzi 121 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wameondolewa katika masomo (discontinue) kwa tuhuma za kuchezea matokeo, huku kesi 15 zikiendelea na uchunguzi zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano na masoko cha chuo hicho, jumla ya wanafunzi 170 walituhumiwa kuchezea mfumo wa matokeo (SR2) mwaka 2023/24.
“Serikali iliunda kikosi kazi kilichohusisha wataalamu wa mfumo wa kompyuta kuchunguza tuhuma hizo na kuwasilisha ripoti Chuo Kikuu cha Dodoma,”imeeleza taarifa hiyo.
Imebainisha baada ya kupokea ripoti hiyo hatua za ndani zilianza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwapa wito watuhumiwa kufika chuoni hapo kusikilizwa kabla ya kuoa uamuzi kwa mujibu wa kanuni.
“Jumla ya wanafunzi 148 walisikilizwa, wanafunzi 32 hawakufika kusikilizwa. Katika wanafunzi waliosikilizwa 121 walipatikana na hatia kuhusika na kuchezea matokeo ya mitihani na kikao cha seneti ya chuo kilipitisha kuondolewa masomoni.”
Taarifa hiyo imeeleza kuwa kesi za wanafunzi 15 zinaendelea na uchunguzi zaidi huku wanafunzi wakikutwa hawana hatia.
Imebainisha kwa mujibu wa taratibu za chuo hicho mwanafunzi ambaye hajaridhika na maamuzi ya seneti anapewa nafasi ya kukata rufaa.
“Hivyo wanafunzi ambao hawajaridhika taratibu ziko wazi wana fursa ya kukata rufaa kupitia mifumo iliyowekwa na chuo,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Imeeleza dirisha la rufaa hufunguliwa wiki mbili baada ya matokeo ya mitihani kutoka na kufungwa baada ya wiki mbili na mwanafunzi ambaye yupo nje ya muda anaruhusiwa wakati wowote kuomba kukata rufaa.
“Chuo kinasimamia taratibu, kanuni na sheria za kimtihani ili kulinda ubora wa taaluma na hadhi ya chuo pasipo kumuonea mtu yeyote,”imeeleza.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa UDOM, Muhammad Muhammad amesema Serikali ya wanafunzi ilishiriki katika vikao vyote vya maamuzi vya chuo hicho ambavyo wanafunzi hao waliitwa na kujitetea kuhusu tuhuma hiyo.
“Kwa mujibu wa sheria za chuo wanaweza kukata rufaa kama hawakuridhika na maamuzi ya seneti waliyoyatoa na pia kwa wale walioridhika wanaweza kuomba tena kusoma, lakini si kwa ile kozi ambayo walikuwa wakiisoma awali,”amesema.
Hata hivyo, jitihada za kuwapata wanafunzi walioondolewa katika masomo zimegonga mwamba baada ya ofisi ya Serikali za wanafunzi ya chuo hicho kusema wanawafahamu kwa majina na hawana namba zao za simu.
Kwa siku kadhaa katika mitandao ya kijamii kumekuwa na ujumbe ukitembea kwenye mitandao ya jamii ikielezea kuhusu wanafunzi kadhaa waliotarajiwa kuhitimu masomo yao kati ya mwaka2023/2024, zaidi ya wanafunzi 400 wamefutwa masomo kwa tuhuma za jumla.
Taarifa hiyo ilieleza uongozi wa chuo uliwaambia wanafunzi hao kwamba wameingilia mfumo wa matokeo wa chuo na kubadilisha matokeo yao.
Wanafunzi hao walizuiliwa kufanya mahafali mwaka 2023 na badala yake wakakamatwa na kupelekwa polisi, ambako simu zao zilichukuliwa kwa ajili ya uchunguzi na wamekaa mwaka mzima bila kupewa taarifa ya uchunguzi huo na hawajui imeishia wapi.
Taarifa hiyo ilisema Januari 2025 wanafunzi hao waliitwa kituo cha polisi kutoa maelezo na mpaka sasa hawajawahi kupewa taarifa ya nini, polisi waliona kwenye simu zao ili waweze kujitetea au kutoa utetezi wao kwa ufasaha. Walichoona ni kuwa ‘discontinued’ kwenye mfumo wao wa chuo.
Wanafunzi hao wanalalamika kwamba wamefanya jitihada za kuuliza uongozi wa chuo kuhusu haki yao ya kusikilizwa au ya rufaa na wamejibiwa wakate rufaa kwa seneti ya chuo.
Taarifa hiyo inasema kuwa wanafunzi hao walipokwenda kwa ajili ya kufanya utaratibu wa rufaa kwa seneti kama walivyo elekezwa, seneti wamesema muda wa rufaa umeisha hivyo hawana muda wa kuendelea kupokea wala kusikiliza rufaa.