Gachagua amuahidi Raila urais Kenya 2027 – Global Publishers



Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua (kushoto) kiongozi wa ODM, Raila Odinga (kulia)

Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, amesema kwamba anaweza kumfanya kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuwa rais wa Kenya iwapo atakubali kuungana naye na vigogo wengine wa upinzani.

Gachagua amesema kwamba wapiga kura wa eneo la Mlima Kenya wako tayari kumuunga mkono Odinga kumshinda Rais Ruto katika uchaguzi wa 2027.Gachagua amedai kuwa anashauriana mara kwa mara na rais wa zamani, Uhuru Kenyatta, kuhusu suala hilo, akidai Odinga bado anasuasua kukubali suala hilo.

Gachagua amemtaka Raila Odinga kuamua ikiwa anataka kuungana na Ruto au kukumbatia Mlima Kenya “na kufanywa rais wa Kenya”.
“Bw Odinga kama mgombeaji wetu wa urais anasisimua zaidi. Huwa anapata takriban kura milioni sita kwa wastani, sisi tuna milioni sita. Kufikia saa nne asubuhi ya siku ya kupiga kura, Rais Odinga atakuwa amepatikana,” amedai Bw Rigathi Gachagua.

Oktoba mwaka jana, Baraza la Seneti nchini Kenya liliidhinisha uamuzi wa kumuondoa madarakani Naibu Rais wa nchi hiyo Rigathi Gachagua kutokana na mashtaka 5 kati ya 11 yaliyowasilishwa dhidi yake, katika hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa.

Gachagua alikabiliwa na msururu wa tuhuma zikiwemo za ufisadi, kukiuka katiba, kumhujumu rais na kushajiisha migawanyiko ya kikabila. Gachagua alikuwa Naibu Rais wa kwanza kuvuliwa mamlaka na Bunge chini ya Katiba ya 2010.


Related Posts