USHINDI wa Yanga wa mabao 5-0, ilioupata juzi dhidi ya Mashujaa, umemfanya kocha wa timu hiyo, Miloud Hamdi kutembelea nyayo za mtangulizi wake, Sead Ramovic aliyeondoka na kutimkia CR Belouizdad ya Algeria, kutokana na rekodi zao za sasa.
Hamdi alijiunga na Yanga Februari 4, mwaka huu kuchukua nafasi ya Ramovic na tangu ajiunge na kikosi hicho ameendeleza rekodi bora katika michezo ya Ligi Kuu Bara msimu huu, jambo linaloonyesha amefuata nyayo za mtangulizi wake kikosini.
Kocha huyo tangu ajiunge na Yanga ameiongoza katika michezo mitano ya Ligi Kuu Bara, ingawa mmoja pekee hakuwa kwenye benchi, wakati kikosi hicho kikiibuka na ushindi wa mabao 6-1, dhidi ya KenGold, mchezo uliopigwa Uwanja wa KMC Februari 5.
Hamdi mwenye uraia pacha wa Algeria na Ufaransa, alijiunga na Yanga akitoka Singida Black Stars aliyojiunga nayo Desemba 30, mwaka jana, akiiongoza katika michezo mitano, ambapo kati ya hiyo ameshinda minne na kutoka sare mmoja tu hadi sasa.
Katika michezo ya ushindi, Yanga ilizifunga KenGold mabao 6-1, (0-0) v JKT Tanzania, (6-1) v KMC FC, (2-1) v Singida Black Stars na (5-0) v Mashujaa FC, ambapo safu ya ushambuliaji imefunga mabao 19 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu.
Kwa upande wa Ramovic raia wa Ujerumani, alijiunga na Yanga Novemba 15, mwaka jana kisha kuondoka Februari 4, mwaka huu, aliiongoza timu hiyo katika michezo sita ya Ligi Kuu na kushinda yote, akifunga jumla ya mabao 22 na kuruhusu mawili tu.
Ramovic aliyeondoka kwa makubaliano ya pande mbili, mbali na Ligi Kuu Bara ila aliiongoza katika michezo sita ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, akishinda miwili, sare miwili na kupoteza pia miwili, akifunga mabao matano na kuruhusu sita.
Kwenye Ligi ya Mabingwa, Yanga ilimaliza nafasi ya tatu kundi ‘A’ na pointi nane, nyuma ya Al Hilal ya Sudan iliyomaliza na pointi 10, huku MC Alger ya Algeria ikimaliza na pointi tisa, wakati TP Mazembe ya DR Congo ilimaliza na pointi tano.
Katika Kombe la FA, Ramovic aliiongoza Yanga kwenye mchezo mmoja tu ambao ulikuwa ni wa hatua ya 64 bora, ambapo kikosi hicho chenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani, kilishinda kwa mabao 5-0, dhidi ya Copco FC kutoka jijini Mwanza.
Kiujumla, Ramovic aliiongoza Yanga katika michezo 13, akishinda tisa, sare miwili na kupoteza miwili, akifunga mabao 32 na kuruhusu manane, huku kwenye Ligi Kuu akiiacha nafasi ya pili na pointi 42, nyuma ya Simba iliyokuwa na 43.
Ramovic alichukua nafasi ya Miguel Gamondi aliyeondoka Novemba 15, mwaka jana ambaye aliiongoza timu hiyo katika michezo 10 ya Ligi Kuu Bara, ambapo alishinda minane na kupoteza miwili mfululizo iliyomfanya kutimuliwa ndani ya kikosi hicho.
Hatua ya Gamondi kufukuzwa ilijiri baada ya timu hiyo kupoteza michezo miwili mfululizo akianza na (1-0) v Azam FC na (3-1) v Tabora United na katika mechi hizo 10, Yanga ilikuwa ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi zake 24.
Gamondi alijiunga na Yanga Juni 24, 2023 akichukua nafasi ya Mtunisia, Nasreddine Nabi aliyeipa mataji mawili ya Ligi Kuu, mawili ya Kombe la Shirikisho (ASFC), mawili ya Ngao ya Jamii na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Tangu ateuliwe kukiongoza kikosi hicho, Gamondi alikiongoza katika jumla ya michezo 40 ya Ligi Kuu Bara kuanzia msimu wa 2023-2024, hadi huu wa sasa wa 2024-2025, ambapo kiujumla kati ya hiyo alishinda 34, sare miwili tu na kupoteza minne.
Katika michezo hiyo 40 ya msimu uliopita na huu wa sasa, safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho cha Gamondi ilifunga jumla ya mabao 85 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 18, ambapo kiujumla kwa misimu miwili alikusanya pointi zake 104.
Gamondi amechukua mataji matatu na timu hiyo akianza na Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2023-2024 na kuifanya Yanga kufikisha mataji 30 tangu mwaka 1965, akachukua Kombe la Shirikisho la FA sambamba na Ngao ya Jamii 2024.