MICHEZO ya Ligi Kuu Bara inatarajiwa kuendelea leo katika viwanja tofauti itakayokuwa na hesabu kali kutokana na timu kuwania nafasi za kujinasua kushuka na zinazotaka kupanda juu kwenye msimamo.
Kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Manyara vita itakuwa kupanda nafasi na pointi tatu muhimu ndizo zitakazoamua kwa mwenyeji Fountain Gate itakayoikaribisha Tanzania Prisons.
Katika mchezo wa kwanza baina yao Oktoba Mosi, 2024, Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Fountain Gate, Wajelajela ilishinda mabao 3-2 katika mchezo uliokuwa na ushindani mkali.
Endapo Fountain Gate itashinda itafikisha pointi 25 na kupanda hadi nafasi ya nane kutoka ya 13 na kuishusha Coastal Union yenye pointi 24, huku Prison ikishinda itafikisha pointi 21 licha ya kuendelea kusalia nafasi ya 14 kwani haitazifikia za Namungo yenye 22 na ipo nafasi ya 12.
Kutokana na hali ngumu iliyopo Prisons, kocha wa timu hiyo, Amani Josiah alisema hawana njia nyingine ya kujikwamua na hatari ya kushuka zaidi ya kushinda kuanzia mechi hiyo na zinazoendelea.
“Viwango vya wachezaji havitofautiana sana, timu kwa sasa zinapambania kufunga ili kupata pointi tatu, utakuwa mchezo mgumu ambao kila mtu anauhitaji wa pointi,” alisema.
Kwa upande wa kocha wa Fountain Gate, Robert Matano alisema, “Utakuwa mchezo mgumu, unaohitaji mbinu ili kuvuna pointi tatu, tunakutana na timu inayotaka kutoka nafasi za chini kama sisi.”
Mabeki wa Prisons watatakiwa kuwachunga washambuliaji walio na mabao mengi Fountain Gate, Salum Kihimbwa (mabao matano) na William Edgar (mabao matano) wamechangia mabao 10 kati ya 39 ya timu nzima, kwa upande wa Prisons mchezaji mwenye mabao mengi ni beki Berno Ngassa na mshambuliaji Meshack Mwamita wana mawili kila mmoja.
Ili Singida Black Stars iliendelee kuifukuzia Azam FC nafasi ya tatu na kujilinda isishushwe nafasi ya nne na Tabora United ni muhimu kushinda mchezo huo dhidi ya Mashujaa iliyopo nafasi ya tisa nyuma yake ipo KMC iliyolingana nayo pointi 23, huku ikipishana pointi moja na Pamba, Namungo na Fountain Gate ambazo zina pointi 22.
Mchezo huo ni muhimu kwa timu hizo kama wanavyosema makocha kuwa unahitaji zaidi mbinu.
Kocha wa Mashujaa, Abdallah Mohamed ‘Bares’ alisema; “Mechi itakuwa ngumu inahitaji mbinu na kutumia nafasi, tumepishana pointi ndogo na timu zilizopo chini yetu, anayeshinda anapanda nafasi ya juu zaidi, hivyo ni mchezo muhimu kwetu.”
Mzunguko wa kwanza Mashujaa ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Singida Black Stars, mchezo uliopigwa Uwanja Lake Tanganyika, Kigoma.
Mchezo mwingine, Kagera Sugar iliyopo nafasi ya 15 ikishinda dhidi ya KMC haitasogea nafasi yoyote isipokuwa itakuwa imefikisha pointi 18 inazomiliki Prisons ambayo inategemeana na matokeo ya mchezo wake dhidi ya Fountain Gate.
KMC ikiwa nafasi ya 10 na pointi 23, kocha wake Kali Ongalla aliyesema: “Hatupo salama katika msimamo wa Ligi Kuu, tunahitaji kushinda mechi ili tusogee nafasi za juu zaidi, ingawa tunacheza na Kagera Sugar iliyopo chini zaidi, hilo litafanya mchezo uwe mgumu na mzunguko wa kwanza tulishinda bao 1-0 nyumbani.”