Mwanza. Wakazi wa Kanda ya Ziwa wametakiwa kuongeza ulaji wa samaki, kutokana na ongezeko na upatikanaji wa kitoweo hicho unaochangiwa na ufugaji wa kwenye vizimba.
Kwa mujibu wa hotuba ya makadirio ya bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha wa 2024/25, uzalishaji wa samaki nchini uliongezeka hadi tani 472,579,34 kufikia Aprili, 2024 kulinganisha na tani 426,555.46 zilizozalishwa kwa kipindi kama hicho mwaka 2023.
Hata hivyo, ulaji wa samaki kwa Mtanzania ni kilo nane kwa mwaka ikilinganishwa na mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kula kilo 20.
Akizugumza wakati wa warsha ya siku mbili iliyoanza Februari 24 hadi 25, 2025 kwa wadau wa uvuvi jijini Mwanza, Kaimu Ofisa Uvuvi Wilaya ya Ilemela, Williadius Ruberwa, amesema ulaji wa samaki husaidia kuongeza protini mwilini na hivyo kuboresha afya ya mlaji kutokana na samaki kutoa zaidi ya asilimia 30 ya protini itokanayo na wanyama.
Buberwa ambaye pia ni Meneja wa Soko la Samaki la Kimataifa la Kirumba, amewaambia washiriki wa warsha hiyo iliyoandaliwa Shirika la Maendeleo la ubelgiji (Enabel) kupitia mradi wa ‘Inclusive green and smart cities’ , kuwa ufugaji wa kwenye vizimba umeongeza upatikanaji na unafuu ya bei na kuwashauri Watanzania kuongeza ulaji wa kitoweo hicho.

Meneja Mradi wa nclusive green and smart cities Kikolo Mwakasungula akizungumza kwenye warsha ya wadau wa uvuvi iliyofanyika jijijini Mwanza.
“Gap (pengo la upatikanaji wa samaki) limeendelea kuzibika kupitia ufugaji wa vizimba…. sato wanaofugwa katika vizimba ni salama na wanafugwa kwa usimamizi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia idara ya ufugaji wa samaki, wananchi tutumie samaki hawa,” amesema Buberwa
Kwa mujibu wa tovuti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, sekta ya uvuvi huchangia zaidi ya asilimia 1.7 ya pato ghafi la Taifa huku mnyororo wake wa thamani ukitoa fursa zaidi ya milioni 4.5 za ajira.
Meneja wa mradi huo, Kikolo Mwakasungula amewashauri wakazi wa Mkoa wa Mwanza ambao wengi wao hutegemea sekta ya uvuvi, kuongeza ubunifu utakaowaongezea kipato kitakachosaidia kuboresha maisha yao.
Amesema mradi huo unalenga kuwezesha wadau kutafuta suluhu shirikishi kwa changamoto za mabadiliko zinazosababishwa na ukuaji wa haraka wa miji, ukitekelezwa jijini Mwanza, Tanga na Pemba ili kukuza, kutunza mazingira na shirikishi, kuzalisha ajira mpya kwenye uchumi rejeshi na na kukuza zilizopo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Uvuvi Endelevu Ziwa Victoria, Bakari Kadabi ameshauri kuwa pamoja na kuhimiza ufugaji wa samaki kwenye vizimba, Serikali na wadau wa sekta ya uvuvi wanapaswa kuendeleza uvuvi wa asili ambao pia umetoa ajira kwa makundi ya watu mbalimbali.