Dodoma. Zaidi ya wakazi 200 wa mtaa wa Mahomanyika uliopo Kata ya Nzuguni jijini Dodoma wameandamana hadi ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo kuwasilisha malalamiko yao kuhusu kuporwa ardhi na kugawiwa watu wengine ambao siyo wazawa wa mtaa huo.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Februari 26, 2025 kwenye ofisi za CCM Mkoa, Mwenyekiti wa mtaa huo, Abraham Mputu amesema mgogoro huo ni wa muda mrefu lakini hakuna kiongozi anayetaka kuutatua.
Amesema kwa muda mrefu sasa wananchi wa mtaa huo wamekuwa wakiporwa ardhi yao na kugawiwa kwa watu wengine.
“Leo tumekuja hapa CCM kuongea na mwenyekiti wa mkoa ili atupe hatima yetu tujue kama sisi ni Watanzania au tunatoka nchi nyingine, tumechoka kunyanyaswa kwenye ardhi yetu wenyewe, kwa sababu hawa ndiyo wenye Serikali na mimi nimetokana na chama hiki sasa wajitokeze wawape wananchi majibu ya maswali yao,” amesema Mputu.
Amedai kuwa mgogoro huo ni wa muda mrefu ambapo viongozi wote wa mkoa wanaujua lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa kuumaliza.

Baadhi ya wakazi wa mtaa wa Mahomanyika, Kata ya Nzuguni Jijini Dodoma wakiwa mbele ya ofisi ya CCM mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kupeleka malalamiko yao yanayohusu mgogoro wa ardhi leo Februari 26, 2025, Picha na Hamis Mniha
“Kama watashindwa kututatulia huu mgogoro tumeazimia kurudisha kadi za chama twende upande wa pili kwa sababu hakutakuwa na maana ya kuwa wanachama lakini yanapokuja matatizo chama kinakuwa hakina msaada,” amesema Mputu.
Richard Madeha amesema kinachoendelea kwenye mtaa huo ni uporwaji wa ardhi ya wananchi bila kushirikishwa na wameshazunguka kwenye ofisi zote kutafuta suluhu, lakini hakuna msaada wowote.
Amesema viongozi walikwenda kwenye mtaa huo na kufanya mkutano na wananchi kuwa washirikiane kupima ardhi yao na kama mtu anapata viwanja ataruhusiwa kuuza, lakini mambo yamebadilika na wanamilikishwa watu wengine tofauti na wenyeji.
Naye Sara Bwanakoo amesema kama mwenyekiti wa CCM Mkoa atashindwa kuwasaidia kwenye mgogoro huo watakwenda kumwona Rais Samia Suluhu Hassani ili awasaidie kupata haki yao ya kumiliki ardhi ambayo wameitunza miaka yote.
“Tumeona anawasaidia wenzetu wengi tu huko na wanapata haki zao na sisi tutakwenda ili atusaidie maana mimi barabara ya mzunguko imechukua heka zangu sita za ardhi lakini sijalipwa chochote, ilihali kwingine ilipopita watu wamelipwa fidia,” amesema Sara.
Hata hivyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Omar Kimbisa na katibu wake hawakuwepo ofisini, hivyo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dodoma Mjini, Charles Mamba alizungumza na watu hao na kuahidi kwenda mtaani kwao kesho Alhamisi Februari 27, 2025 akiwa ameongozana na viongozi wa ngazi zote ili kuona eneo lenye mgogoro.