M23 waiponza Rwanda, Uingereza yaisitishia misaada

Kigali. Rwanda imekuwa ikituhumiwa na Serikali ya Rais Felix Tshisekedi wa DRC na Umoja wa Mataifa (UN) kuwafadhili waasi hao, hata hivyo, Rais Paul Kagame kupitia mahojiano yake na CNN mwezi uliopita alikanusha kulifadhili kundi hilo.

Pia, Rais Kagame alipoulizwa juu ya uwepo wa askari wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) alidai hana taarifa ya uwepo wa askari wa Rwanda ndani ya ardhi ya DRC, huku akisema kinachofanyika ni operesheni zinazolenga kuwakamata waasi wa FDLR wanaotishia amani ya Rwanda.

Shirika la Habari la Associated Press (AP), limeripoti leo Jumatano Februari 26, 2025, kuwa Uingereza imeanza kuiadhibu Rwanda kutokana na uhusika wake katika uvamizi unaoendeshwa na M23 Mashariki mwa DRC na uhalifu dhidi ya haki za binadamu nchini humo.

Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kusitisha misaada ya moja kwa moja ya kifedha ambayo haihusishi misaada kwa wananchi maskini wa Rwanda.

Uingereza pia imetangaza kusitisha ushiriki wa maofisa wa ngazi za juu kwenye hafla zinazoandaliwa na Serikali ya Rwanda,  pamoja na kupunguza shughuli za kukuza biashara na taifa hilo la Afrika Mashariki.

Utekelezaji wa  vikwazo hivyo umeelezwa kupitia taarifa ya Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo ya Uingereza.

Taarifa hiyo iliyoripotiwa na AP, imesema Serikali ya Uingereza pia itashirikiana na mataifa mengine ili kujadili namna ya kuangalia uwezekano wa kuiwekea Rwanda vikwazo vipya.

Hatua nyingine ni pamoja na kusimamisha mafunzo ya kijeshi ya siku zijazo na kupitia upya leseni za mauzo ya nje kwa jeshi la Rwanda.

Haikufahamika mara moja ni kiasi gani cha msaada wa kifedha wa moja kwa moja ambacho Rwanda inapokea kutoka nchini Uingereza.

Hatua hizi zitaongeza shinikizo kwa Rais Kagame, ambaye mara nyingi amekuwa akitetea juhudi za nchi yake kulinda mipaka yake dhidi ya eneo la mashariki mwa DRC, eneo ambalo utulivu wake umetokea kutokana na mapigano kati ya vikosi vya Jeshi la Serikali la FARDC na M23.

Takriban wanajeshi wa Rwanda 4,000 wanadaiwa kuwa wanapigana bega kwa bega na waasi wa M23 mashariki mwa DRC.

Waasi hao hivi sasa wameiteka na kuidhibiti miji mbalimbali ikiwemo wa Goma ambao ni Makao Makuu ya Jimbo la Kivu Kaskazini na Bukavu ambao ni Makao Makuu ya Jimbo la Kivu Kusini, kulingana na ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa.

M23 ni kundi lenye nguvu zaidi kati ya makundi mengi ya waasi yanayopigania udhibiti wa mashariki mwa DRC, eneo lenye utajiri mkubwa wa rasilimali za madini ambazo ni muhimu kwa teknolojia ya kisasa duniani.

Rais Tshisekedi wa DRC, amekataa mazungumzo ya amani na waasi wa M23 licha ya wao kuendelea kuteka maeneo zaidi, akiwatuhumu kuwa jeshi la mamluki la Rwanda lenye njama ya kupora utajiri wa asili wa nchi yake kinyume cha sheria.

Mamlaka za Rwanda zimeelezea hatua za Uingereza kuiwekea vikwazo kama adhabu na zisizofaa.

“Ni jambo lisilo la busara kutarajia Rwanda kuhatarisha usalama wake wa taifa na usalama wa wananchi wake,” ilisema Serikali ya Rwanda katika chapisho lake la mtandao wa X.

“Hatua hizi hazisaidii (Congo), wala hazichangii kufanikisha suluhisho la kisiasa la kudumu kwa mgogoro mashariki mwa (Congo).”

Mbali na Uingereza, Marekani tayari imemuwekea vikwazo mmoja wa maofisa wa Serikali ya Kagame kwa madai ya kuhusika kufadhili uasi wa M23.

Mwanadiplomasia Mkuu wa Umoja wa Ulaya (EU), Kaja Kallas, mapema wiki hii alinukuliwa akisema kuwa  machafuko yanayoendelea nchini DRC, “hayawezi kujadiliwa.”

Alisema mashauriano ya ulinzi kati ya EU na Rwanda yamesitishwa na makubaliano yao kuhusu malighafi muhimu, yaliyotiwa saini mwaka mmoja uliopita yatapitiwa upya.

EU na Rwanda pia hushirikiana katika misheni za kulinda amani nchini Msumbiji na maeneo mengine.

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa mapigano mashariki mwa DRC yanahatarisha usalama wa eneo zima, ambalo limekumbwa na migogoro ya muda mrefu iliyowafanya mamilioni ya wananchi wake kuwa wakimbizi.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Related Posts