Dar es Salaam. Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imezindua mwendelezo wa awamu ya kwanza ya ulipaji fidia ya Sh20 bilioni kwa wananchi 203 kati ya 1,865 wa Mtaa wa Kipunguni waliopisha upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1997.
Ulipaji huo wa fidia, unatarajiwa kupishana mwezi mmoja kwa kila awamu kati ya tatu na kazi hiyo itafanyika nchi nzima, kwa kuwahusisha wote waliopisha upanuzi wa viwanja vya ndege licha ya shughuli hiyo kuanzia Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Februari 26,2025 na Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Abdul Mombokaleo katika hafla ya uzinduzi wa mwendelezo awamu ya kwanza wa ulipaji wa fidia za wananchi hao, zilizodumu kwa takriban miaka 28.
“Mpango huu ni endelevu hata kwa walio katika mikoa mingine, naomba ieleweke, kadri tutakavyokuwa tunahakiki na kujiridhisha tutafanya malipo, kila mmoja atapata stahiki zake,” amesema Mombokaleo.
Mhandisi wa Uendeshaji na Ufundi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Focus Kadeghe amesema ucheleweshwaji wa fidia hizo ulitokana na sheria zilizokuwapo wakati wananchi wanahamishwa kwa ajili ya upanuzi wa uwanja huo.
“Upanuzi wa uwanja huu, ulianza 1997 kabla kuanzishwa kwa TAA na ulifanyika chini ya Wizara ya Uchukuzi, maeneo mawili yalishalipwa tangu mwaka 2009 na la tatu ni hili la Kipunguni,” anaeleza Kadeghe.
Amesema maeneno hayo, yalithamishwa tangu mwaka 1997 kwa kutumia sheria namba 47 ya 1967 ambayo utaratibu wake ulikuwa ni kumlipa mwananchi mwendelezo ambao ni nyumba na mazao pekee.

Mkazi wa Mtaa wa Kipunguni Mikaeli Mwita akitoa Shukuruni kwa uongozi wa mamlaka hiyo kwa kufanikisha ulipwaji wa fidia zao.
“Eneo la Kipunguni kwa mwaka 1997 thamani yake ilikuwa Sh7.7 bilioni, mwaka 2009 thamani ilipanda na kufikia Sh15 bilioni na 2014 wananchi 19 walifanikiwa kulipwa fidia zao zilizogharimu Sh1.2 bilioni,” amesema Kadeghe.
Pia, amesema baada ya malipo hayo kufanyika sheria ilibadilika na kuanza kutumia sheria namba 47 kifungu cha 4 ya mwaka 1999 na baadaye sheria mpya namba 7 ya mwaka 2006 ilianza kutumika huku ikitambua ardhi kama mali.
“Kutokana na mabadiliko hayo ya sheria, Serikali ilithaminisha upya ardhi ya Kipunguni kwa kutumia sheria mpya, wananchi 1,865 wameguswa na fidia ya Sh143.9 bilioni,” amesema Kadeghe.
Aidha, amesema baadhi ya wananchi waliowahi kulipwa mwaka 2014 wa maeneo ya Majohe na Msongola watakatwa kiasi cha fedha kutokana na yale malipo waliyopokea hapo awali.
Sambamba na hilo, Kadeghe amesema wakati wa kuhama, wananchi wanaruhusiwa kuondoka na mali walizonazo na karatasi za malipo watakazokabidhiwa zitakuwa na muda wa kuhama na kuwa muda huo ukiisha taratibu za kuwaondoa zitaendelea.
Aidha, Mikaeli Mwita, mkazi wa Mtaa wa Kipunguni ametoa shukurani kwa Mkurugenzi wa TAA kwa kufanya jitihada mpaka utatuzi wa sakata hilo.
“Japo siko kwenye awamu ya kwanza, ila nuru tunaiona baada ya kupotea kwa miaka 28 huku wakurugenzi saba wakipita katika shirika hili, bila mafanikio,”amesema Mwita.
Pia, Mkurugenzi wa JNIA, Bertha Bankwa amesema eneo hilo, baada ya wananchi kuhama litatumika kuendeleza miundombinu ya kiwanja kutoka daraja la 4C kwenda daraja la 4F.

Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bertha Bankwa wakati wa hafla ya uzinduzi wa mwendelezo wa awamu ya kwanza ya ulipaji fidia kwa wananchi wa Mtaa wa Kipunguni
“Miundombinu hiyo, itawezesha kuhudumia ndege kubwa duniani ambayo ni Airbus 380 tofauti na sasa imekuwa ikipokea ndege hizo kwa dharura, na si kutua kibiashara,” amesema Bankwa.
Pia, amesema mbali na miundombinu hiyo, eneo hilo litatumika kufanya uwekezaji wa hoteli, kumbi za mikutano na kuboresha huduma za uendeshaji wa kiwanja hicho ikiwamo karakana.
“Tutaongeza miundombinu ambayo itainua mapato ya shirika tofauti na mapato ya ndege,” amesema.
Pia, amesema kutegemea mapato ya ndege pekee, kutashindwa kutatua majanga yanayotokea na kusababisha shirika hilo kushindwa kufanya kazi.
Bankwa amesema utendaji kazi wa shirika hilo umeendelea kupanda siku hadi siku, kwa mwaka 2022 walipokea abiria milioni 2.4 mwaka 2023 abiria waliongezeka na kufikia milioni 2.6 na mwaka 2024 abiria milioni 2.8.
“Ndege za kimataifa zimeongezeka sambamba na uwekezaji wote, hii ni kutokana na hali nzuri ya kiusalama katika eneo la kiwanja,” amesema Bankwa.